NA GEORGINA MISAMA – MAELEZO
SERIKALI imewataka wamiliki wa ardhi kuhakikisha wanalipia
kodi ya pango la ardhi kwa wakati ili kuepuka kunyang’anywa umiliki wa ardhi
zao.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino
kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Mboza Lwandiko wakati
akizungumza na waandishi wa habari, Jijini Dar es Salaa.
Mboza alisema kwamba Wizara inakusudia kufanya mnada wa
viwanja takribani 10 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Temeke na
Kinondoni ambavyo havijalipiwa kodi ya pango la ardhi mpaka Machi 24, 2017.
“Usipolipa Kodi ya Pango la Ardhi kwa wakati, utanyanganywa
umiliki wa ardhi yako, kutokana na sheria ya Ardhi, Na. 4 ya mwaka 1999, katika
kifungu cha 49 na 51”, alisema Mboza.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Kodi kutoka Wizara hiyo Bw. Denis
Masami alitoa ufafanuzi wa utaratibu unaotumika kuwasiliana na
wamiliki wa ardhi walioshindwa kulipa kodi kwa wakati na kusema kwamba
wadaiwa wanapewa hati ya madai na kupewa muda wa kukamilisha madeni yao.
Muda wa kukamilisha malipo ukipita, amri ya mahakama ya
kukamata mali hufuata, ambapo mmiliki wa ardhi atatakiwa kuikomboa ardhi yake
kwa kulipa deni mara moja, akishindwa Mahakama hutoa amri ya kuuza mali.
Mahakama imetoa amri ya kwanza tarehe 27/01/2017 ya
kukamata mali kwa wadaiwa sugu na tarehe 24/01/2017 mahakama ilitoa kibali kwa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuuza kwa mnada wa hadhara
viwanja ambavyo havijalipiwa kodi ya pango la ardhi.
“Tarehe 20 Machi, 2017 Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi ilitoa tangazo la mnada wa hadhara wa kuuza viwanja ambavyo
havijalipiwa kodi ya ardhi unaotarajiwa kufanyika Machi 26, 2017”, alisema
Denis.
Denis aliongeza kwamba Wizara imeandaa orodha ya wadaiwa
sugu, mpaka sasa katika orodha hiyo baadhi ya viwanja vimelipiwa sehemu ya kodi
inayodaiwa baada ya wamiliki kuomba kukamilisha sehemu iliyobaki kabla ya
kumalizika kwa muhula huo.
Wizara inatoa rai kwa watanzania wanaomiliki ardhi
kujifunza utamaduni wa kulipia kodi pasipo shurti. Kodi ya ardhi hulipiwa kila
ifikapo Julai Mosi ya kila mwaka katika Manispaa au Halmashauri husika na
katika Ofisi za Malipo ya Kodi-Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269