Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Tickson Nzunda |
Na Kitengo cha
Mawasiliano WAMJW
Wataalam wa Maendeleo
ya Jamii wana jukumu la kuhamasisha wananchi kubadili fikra zao ili wawe na
mtazamo chanya unaowapa hamasa ya kushiriki kazi za kujitolea ili kujiletea
maendeleo yao wenyewe na Taifa lao.
Hayo yamezungumzwa
Mjini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu kutoka OR TAMISEMI Bw. Tickson Nzunda wakati
wa Mkutano wa Mwaka kwa Wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii na kuwataka
washiriki kufanya kazi zao kwa umahiri, kujenga uelewa kwa viongozi wa Halmashauri,
kuchochea mabadiliko sehemu za mitaani na vijijini, kuelimisha jamii kubadili
mitazamo na fikra, na hivyo kukuza ari ya wananchi kushiriki maendeleo ili
kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
Pamoja na mambo
mengine, Naibu Katibu Mkuu amewataka Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kuratibu
shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
taratibu ili kuhakikisha kuwa mashirika hayo yanakuwa na mchango unaokusudiwa
katika kufanikisha mipango ya Halmashauri, Mikoa na Taifa ili kuboresha ustawi
na maendeleo ya watu.
“Tunatarajia kuwa
Mashirika Yasiyo ya Kiseriklali yangehakikisha kuwa yanasaidia kutoa mchango
katika kuwekeza kwenye uwekezaji wa vipaumbele vya kitaifa vilivyoainishwa ikiwemo
kuboresha miundo mbinu ya elimu mashuleni ili kuwa na mazingira wezeshi ya
kufundishia na kujifunzia, jambo ambalo halifanyiki ipasavyo” alisema Bw. Nzunda.
Naye Katibu Mkuu
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi Sihaba Nkinga amefafanua kuwa
watumishi wa maendeleo ya jamii ndiyo washawishi na waragibishi wakuu katika
kuamsha ari ya wananchi kushiriki mipango ya maendeleo kwa ajili ya mabadiliko
ya watu wenyewe.
“Tutambue dhamana
tuliyonayo lakini pia umahiri wenu utumike kusaidia watu masikini, wananchi wa
vijijini na makundi maalumu katika kuwaongoza kupata haki na fursa sawa”
alisema Bibi Sihaba.
Akizungumza katika
mkutano huo Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Nyasa Bw. Protas Sule amesema kuwa
wataalamu wa maendeleo ya jamii wanajukumu la kuhimiza wananchi, Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali kwa kusaidiana na Serikali na jamii kutatua matatizo haya bila
kusubiri Serikali kutekeleza kila kitu.
“Afisa Maendeleo ya Jamii akifanikiwa kubuni
mradi utatoa majawabu ya kero za vikundi vya vijana na wanawake atakuwa
amefanya kazi kubwa ya kuaminisha jamii kwa Serikali na kuamsha ari yao kufanya
kazi za maendeleo” alisema Bw. Sule
Maafisa Maendeleo ya
Jamii wanatakiwa kuonesha utumishi uliotukuka katika kuhamashisha na kuamsha ari
ya wananchi kushiriki shughuli za maendeleo yao bila kutegemea Serikali
kuwafanyia kazi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269