Breaking News

Your Ad Spot

Jan 28, 2010

TLTC YAKABIDHI MATREKTA YA SH.MILIONI 130 KWA VYAMA VYA TUMBAKU


MKUU wa Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya, Rashid Ndaile (katikati) akijaribu kuendesha moja ya matrekta manne yaliyonunuliwa na Kampuni ya Tumbaku Tanzania (TLTC) kwa ajili kuvikopesha vyama vinne vya msingi vya tumbaku wilayani humo. Hafla hiyo ilifanyika katika kijiji cha Lupa. Kulia ni Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa TLTC, Richard Sinamtwa.

STORY
Kampuni ya Ununuzi wa Tumbaku nchini(TLTC) imechukua hatua nyingine ya kukuza ushirikiano baina yake na vyama vya msingi vya tumbaku wilayani Chunya mkoani Mbeya kwa kuvikabidhi matrekta manne yenye thamani ya zaidi ya milioni 130.
        Akizungumza katika hafla ya makabidhiano yaliyofanyika kijiji cha Lupa, wilayani humo, Mkurugenzi wa Uhusiano kampuni hiyo, Richard Sinamtwa alisema matrekta hayo yatachangia kukuza zao,hivyo kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya umaskini.
       Alisema kuwa kampuni yake itafanyanyakazi bega kwa bega na wakulima wa zao hilo katika kutimiza nguzo zote za Kilimo Kwanza ili kuyafikia mapinduzi ya kijani nchini kwa kuwawezesha wakulima kuachana na jembe la mkono sawa sawa na mpango wa kuendeleza kilimo bora nchini ASDP.
       Sinamtwa alivitaja vyama vinavyonufaika na mpango wa matrekta hayo kuwa ni Majengo, Upendo, Kalangali na Nkung’ungu, ambapo alisema vyama hivyo vitarejesha chini ya nusu ya gharama ya ununuzi wa matrekta hayo katika muda maalum.
       Alisema kampuni yake ikifanya kazi na washirika wake itaendelea kuvisaidia vyama vya msingi vya ushirika vya tumbaku kwa kuvipatia huduma za ughani na mbegu bora zinazolishwa katika mashamba yake ya mfano yaliyoko Urambo,mkoani Tabora, Likenangena mkoani Ruvuma na Lupa yenyewe.
       Simtawa alisema pamoja na mradi huo wa matrekta, kampuni yake imeanzisha mpango umwagiliaji vitalu vya tumbaku pamoja na mazao ya chakula, ambapo tayari imegawa bure pampu 200 kwa wakulima hao.
       Katika hotuba yake, Mgeni rasmi katika hafla hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Chunya,Rashid Ndaile alisema matrekta hayo yamekuja sambamba na mkakati wa kitaifa wa 2025 wa kupunguza umaskini pamoja na kilimo Kwanza ambayo yote inahimiza matumizi ya zana bora za kilimo.
      Alisema miikakati yote miwili ASDP na Kilimo Kwanza inahimiza matumizi ya zana bora za kilimo kunavyoweza kumletea tija bora mkulima,” alisema huku akiwapongeza TLTC ambao kama sekta binafsi wameonesha njia kwa kuwasaidia wakulima na serikali katika kufikia malengo yake ya maendeleo.
      Ndaile aliwaasa wakulima hao kutumia vyema pesa zinazotokana na tumbaku kwa kuhifadhi akiba ya chakula,kusomesha watototo shule, kujenga nyumba bora pamoja na kuwekeza katika miradi ya maendeleo.
      Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake, Alex Mtalisi kutoka chama cha msingi cha Kalangali aliwashukuru TLTC,akisema misaada inayotolewa kwao siku kwa siku itazidi kulikuza zao la tumbaku nchini.
      Aliiomba TLTC izidi kuwasaidia hususani katika ujenzi wa mabanda yanayotumia kuni kidogo wakati wa ukaushaji wa tumbaku.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages