Breaking News

Your Ad Spot

Feb 11, 2010

RUFANI YA BABU SEYA NA WANAYE LEO, JIJINI DAR

MAHAKAMA ya Rufani Tanzania leo inatarajiwa kuisoma rufani ya Mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi hapa nchini , Nguza Viking 'Babu Seya' (Pichani) na wanawe watatu akiwemo Papii Kocha.

Nguza  na wanawe wapo jela wakitumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kulawiti.
      Kwa mujibu wa notisi waliyopatiwa jana mawakili wa serikali na wa walalamikaji, majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Nathalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk na Salum Massati, wataisoma rufani hiyo ambayo ni  namba 59 ya mwaka 2005. Watu wengi wakiwemo mashabiki wa wasanii hao wanasubiri matokeo ya rufaa hiyo.
     Juni 25, mwaka 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu, Dar es Salaam, Addy Lyamuya, aliwatia hatiani Babu Seya na wanawe Papii Nguza ‘Papii Kocha’, Nguza Mbangu na Francis Nguza.
    Wasanii hao walituhumiwa kutenda makosa kumi ya kubaka watoto wa wenye umri kati ya miaka sita na minane na makosa mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri huo huo kati ya April na Oktoba 2003 katika maeneo ya Sinza kwa Remmy, Dar es Salaam.
     Wakili wao, Mabere Marando, amedai kuwa, Hakimu Lyamuya, aliingiza maslahi yake binafsi na hakuwa akizingatia ushahidi uliokuwa ukitolewa na upande wa washitakiwa.
     Marando amedai kuwa, hakimu huyo alitoa kipaumbele kwa mashahidi wa upande wa Jamuhuri na kupuuza mashahidi wa upande wa washitakiwa hivyo kuwanyima haki.
     Kwa mujibu wa Marando, watoto wote waliokwenda mahakamani kuthibitisha kwamba walibakwa au kulawitiwa na washitakiwa walitoa ushahidi bila kiapo isipokuwa mmoja kati ya 10 waliotoa ushahidi.
    Amedai kwamba, watoto hao pia hawakurekodiwa ushahidi wao kabla ya kutoa ushahidi mahakamani jambo ambalo linakiuka sheria.
     Marando amedai kuwa, baadhi ya watoto waliotoa ushahidi walikiri kutomtambua Babu Seya na washitakiwa wengine na kwamba, ripoti ya Daktari ilionyesha kwamba miongoni mwa watoto hao walikuwa ni bikira hivyo kumaanisha kwamba walikuwa hawakufanya kitendo chochote kilichohusiana na mashitaka hayo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages