.

RAIS WA POLAND NA MKEWE WAFARIKI KATIKA AJALI YA NDEGE

Apr 10, 2010


Alikuwa pia na, gavana wa benki kuu,  mnadhimu wa majeshi na waziri
Smolensk, RUSSIA
RAIS wa Poland Lech Kaczynski (pichani) na  mkewe Maria na Mkuu wa Majeshi, Franciszek Gagor wamefariki dunia katika ajali ya ndege iliyotokea kusini mwa Smolensk.
    Maofisa wa jimbo hilo walisema jana kuwa, katika ajali hiyo pia walikuwemo maofisa kadhaa wa serikali yake, akiwemo Gavana wa Benki Kuu, Slawomir Skrzypek na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Andrzej Kremer.
    Walisema kuwa hakuna mtu aliyenusurika katika ajali hiyo iliyotokea wakati ndege hiyo ilipogonga miti ilipokuwa ikitaka kutua.
    Maofisa hao walisema, tukio hilo lilisababishwa na hali mbaya ya hewa iliyotokana na ukungu kutanda katika sehemu mbalimbali za jimbo hilo.
    Maofisa hao waliku wakienda Russia katika sherehe za kuadhimisha miaka 70, tangu kumalizika kwa mauaji ya Katyn. Sherehe hizo huadhimishwa kutokana na mauaji ya halaiki ya polisi zaidi ya 20,000 wa Poland.
   Mauaji hayo yalifanywa na polisi maalumu wa iliyokuwa Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti wakati wa vita vya pili duniani.
   Tukio hilo limewaacha Wapoland katika majonzi, ikizingatiwa kwamba serikali ya Rais Kaczynski imefanikiwa kudhibiti hali ya kisiasa na kiuchumi katika taifa hilo.
   Habari kutoka Warsaw, Poland zilisema Waziri Mkuu Donald Tusk alikuwa katika hali ngumu baada ya kupewa taarifa za msiba huo. Kiongozi huyo alishindwa kuzungumza chochote na alionekana akilia kwa uchungu.
   Msemaji wa Wizara ya Ulinzi wa Russia, Irina Andrianova alisema ndege hiyo ilikuwa ikitokea Moscow kwenda Smolensk, na kwamba haikuwa na matatizo yoyote wakati ilipoondoka.
   Naye Gavana wa Smolensk, Sergei Antufiev alikaririwa na kituo cha televisheni cha Russian akisema hakukuwa na dalili za uhai katika eneo la tukio.
  " Wakati ikijiandaa kutua, ndege hiyo ya Rais haikufanikiwa. Taarifa za awali zinaonyesha kwamba iligonga miti, ikaanguka chini na kusambaa katika vipande. Hakuna mtu aliyenusurika.
   “Kwa sasa tunafuatilia kujua (ndani ya ndege hiyo) kulikuwa na ujumbe wa watu wangapi. Taarifa zinadai walikuwa 85, “ alisema gavana huyo. Hata hivyo, wachunguzi wa Russia walidai kulikuwa na maofisa 132.
   Kaczynski alichaguliwa kuwa Rais mwaka 2005 na kabla ya hapo alikuwa Meya wa mji wa Warsaw kwa miaka mitatu.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª