Breaking News

Your Ad Spot

Apr 23, 2011

UJENZI MAKAO MAKUU MAPYA YA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI ( EAC) KUKAMILIKA AGOSTI MWAKA HUU

Bw. Phil-Makini Kleruu

Na Bernard Natha wa EANA, ARUSHA
Ujenzi wa jengo jipya la kisasa la makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.


Kwa mujibu wa ofisa anayesimamia ujenzi huo, Phil-Makini Kleruu, shughuli za ujenzi zinaenda kama zilivyopangwa."Takribani asilimia 59 ya kazi ya ujenzi iliyoanza Aprili mwaka jana imekamilika; ujenzi unafanyika kwa kasi," alisema Phil-Makini Kleruu, akizungumza na Shirka Huru ya Habari ya Afrika Mashariki (EANA).


Jengo hilo ,ambalo linajengwa kuhimili matetemeko ya ardhi , linagharamiwa na serikali ya Ujerumani kwa gharama za Euro milioni 14 na lmradi huo utakapokamilika utaokoa zaidi ya dola ya merekani 500,000 zinazotumika sasa kwa ajili ya pango.


Makao makuu ya EAC yapo ndani ya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC) uliopo mjini hapa na taratibu za ujenzi wa makao makuu zilianza mwaka 2005 wakati serikali ya Tanzania ilipotoa  bure eka 10 za ardhi karibu na makao makuu ya sasa kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu hayo mapya. 

 Kleruu alisema kwamba thamani ya ardhi hiyo iliyotolewa na serikali ya Tanzania  ni Euro milioni 1.8 ambapo mwaka 2005, Ujerumani ilitoa Euro milioni 8 kuanza ujenzi  na bajeti yake ilibadilika mwaka 2007 baada ya nchi za Rwanda na Burundi kujiunga na EAC na hivyo mradi huo kuonekana kustahili kupanuka zaidi.
.
Kwa kuwa ujenzi wa jengo hilo unafanywa kwa fedha za Ujerumani , mataifa wanachama wa EAC-- Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda,  zitatakiwa kuweka samani na kutengeneza bustani za makao makuu hayo.


Kwa mujibu wa meneja wa kazi wa mradi huo, Jeus Neuhaus, makao makuu ya EAC yametengenezwa kiasi ya kwamba yanaweza kutumiwa na wanachama wengine kwa kadri watakavyoongezeka."Ubunifu wa jengo hilo unatoa nafasi ya kuingiza nchi zaidi," alisema Neuhaus.


Jumuiya ya EAC pia imetwaa  eka 126 za ardhi huko Kisongo, karibu na uwanja wa  ndege wa  Arusha, kwa lengo la kuwa na nafasi kubwa ya kutanuka kama ikibidi katika siku za usoni.


Makao makuu mapya ya EAC yatakuwa na nafasi za ofisi 250, eneo kubwa la kuegesha magari, vyumba vya mikutano, vyumba maalumu vya watu mashuhuri, huduma za kibenki, maeneo ya masoko na ukumbi wa mikutano. Vyumba vingine ni vya habari na migahawa.


Pia kuna vyumba maalumu vya mikutano isiyozidi watu 100.Sehemu ya kuegesha magari itakuwa kwa ajili ya watu mashuhuri 40 kwa mkupuo na watu 400 kwa ajili ya wageni na wafanyakazi wa EAC.


Jiwe la msingi la ujenzi wa jengo hilo liliwekwa na viongozi wa EAC Novemba 20 mwaka 2009 wakati wa mkutano wa kumi wa  viongozi wa Jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages