Breaking News

Your Ad Spot

Dec 1, 2013

MMOJA AKUTWA AMEKUFA SHINYANGA

Na Chibura Makorongo, Shinyanga
Mwanamme mmoja aliyejulikana kwa jina la Sabas Jumanne Mlengela (54)mkazi wa kitongoji cha Bugwandege kata ya Ibinzamata mjini Shinyanga amekutwa amekufa kwenye mto wa daraja la Kidaru maarufu Daraja la Ibinzamata huku akiwa na baiskeli yake ndani ya maji.

Walioshuhudia tukio hilo wamesema tukio hilo limetokea leo majira ya saa moja asubuhi  ambapo Sabas Jumanne Mlengela,ambaye ni mkaguzi wa hesabu katika shirika la COASCO Shinyanga alikutwa amekufa maji kwenye mto wa daraja hilo mwili wake ukiwa unaelea juu ya maji.

"Tulipofika katika eneo hili tuliona sikio la mtu ndani ya maji haya kwenye hili daraja,na baadaye tukabaini kuwa kuna mtu amekufa katika mto huu,marehemu akielea akiwa na baiskeli yake ndogo lakini nje ya maji kulikuwa na simu yake,mmoja wa waliokuwepo ndiyo akawapigia simu ndugu zake na marehemu kuwajulisha kilichotokea",alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Aliongeza kuwa kifo cha mzee huyo huenda kinatokana na kuteleza na kisha kutumbukia kwenye daraja hilo lakini pia huenda ni fitina za watu ambao wamemfanyia unyama na kumtupia kwenye maji kwani kama angekuwa ametumbukia kwa kuteleza hata simu yake nayo  ingekuwa kwenye maji .

"Kwa kweli tunashindwa kuelewa nini hasa chanzo cha kifo hiki,nadhani marehemu atakuwa ameuawa na kutupiwa kwenye maji na watu wabaya kwani haiwezekani mwili uwe majini halafu simu yake isiwe majini,na na hawa waliomuua nadhani siyo vibaka kutakuwa na fitina flani tu",alieleza mashuhuda mwingine alijitambulisha kwa jina John.

Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Kihenya Kihenya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mwili wa marehemu ulikutwa umezama kwenye mto huo pamoja na baiskeli yake ingawa simu yake na kalamu vilikuwa vimenguka pembeni mwa mto huo huku mwili wake ukiwa hauna majeraha yoyote.

Kamanda Kihenya alisema kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa ndugu zake na marehemu walisema siku moja kabla ya tukio yaani Novemba 29 mwaka huu majira ya saa tatu usiku walikuwa pamoja na marehemu kwenye kikao cha kuvunja kamati katika bar iitwayo Baelezee iliyopo mjini Shinyanga.

"Ndugu zake na marehemu wameeleza kuwa walikuwa na marehemu jana wakivunja kamati katika bar ya Baelezee na kwamba marehemu aliondoka saa tatu usiku kurudi nyumbani na hakuonekana tena hadi alipogundulika akiwa amekufa chini ya daraja leo asubuhi",Kihenya alieeleza.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages