Mkurugenzi
wa shirika la Compassion Tanzania,Mchungaji Joseph Mayala alipokuwa
akizindua miradi mbalimbali Iringa. (picha na Denis Mlowe)
====== ====== =======
Na Denis Mlowe,Iringa.
SHIRIKA
la kimataifa la Compassion linalofanya kazi na madhehebu ya Kikristo
nchini linatarajia kutumia zaidi ya sh. Bilioni 41.8 hadi Juni mwaka huu
katika kutekeleza miradi yake ikiwemo kuwasomesha wanafunzi 70,087
wanaosoma shule na vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi wa shirika hilo Joseph Mayala, wakati
akizungumza katika ufunguzi wa nyumba ya mtoto Chris Kadege(3)
iliyofadhiliwa kwa msaada wa shirika hilo kwa kushirikiana na Kanisa la
Kianglikana Dayosisi ya Ipogoro mwishoni mwa wiki mjini hapa,
alisema kuwa miradi hiyo inalenga kutekeleza malengo ya maendeleo ya
millennia (MDG) na dira ya taifa 2025.
Alisema
kuwa mkazo mkubwa ukiwa ni kuwatoa na kuwakomboa watoto hao kutoka
kwenye hali za umasikini wa Kiuchumi, kiroho, Kijamii, na Kimwili na
hatimaye kuwawezesha kuwa watu wazima wanaoujua wajibu wao, na
wanaojitosheleza.
“Imekuwa
kasumba ya watanzania waliowengi kulalamika bila kufanya kazi kwa
bidii, maarifa na uadilifu hivyo ni lazima tuwe na mkakati na tunataka
tuwe na kizazi sio cha wanung’unikaji na walalamikaji tunataka tuwe na
kizazi chenye kutafuta suluhisho ufumbuzi wa matatizo na suala ya
kuwasaidia watoto yatima ni jukumu letu sote kuanzia ngazi ya familia
hadi taifa” alisema Mawala.
Aidha
Mch.Mayala alisema kuwa malengo waliyonayo ni pamoja na kuendelea kutoa
huduma kwa kushirikiana na makanisa yenye ushirika wenza katika misingi
ya uadilifu,utu,na kuwa mawakili wema wa rasilimali za watoto na jamii
na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika vituo vyao vyote.
Alisema
Watoto na vijana ni talanta na rasilimali kwa taifa ambayo Mwenyezi
Mungu ametupa sisi Serikali, Makanisa na jamii kwa ujumla ili tuwekeze
kwao kwa namna ambayo inafaa na inayotambua mpango mkamilifu wa Mwenyezi
Mungu kwa kila mtoto mmoja mmoja ili afikie kule ambako Mungu
alimkusudia. Watoto na vijana tulio nao leo ndio pekee wanaoweza
kubadilisha chanya kesho ya Taifa letu kama tukiwaandaa na kuwasimamia
kikamilifu.
Alisema
shirika hilo linazidi kukua kwa kasi kutokana na kufanya kazi zake kwa
uadilifu kwa kutekeleza miradi mbalimbali na taarifa zake kurudishwa
makao makuu ya shirika hilo nchini Marekani hivyo kusababisha kuendelea
kupata misaada zaidi. Aliongeza kuwa licha shirika hilo kumjengea nyumba
mtoto Chris Kadege anayeishi katika mazingira magumu limewajengea
watoto wanaolelewa na kanisa la Kianglikana dayosisi ya Ipogoron
ukumbi wa mkutano na madarasa mawili yenye thamani ya shilingi milioni
49 na nyumba iliyogharimu shilingi milioni 7.8
Alizitaja
programu mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo ni kupamba na UKIMWI,
Majanga, Afya , Watoto walio katika mazingira hatarishi na Miundombinu
. Miradi mengine ni kutoa vifaa vya Mafunzo kwa watoto,
Matibabu , Ujasiriamali , Elimu isiyokuwa rasmi, Elimu kwa Wazazi, Maji
na Usafi. .
“Kwa
kuzingatia uadilifu huwa tunatoa taarifa kwa serikali kwenye ofisi
mbalimbali zikiwemo ofisi za wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya sehemu
ambazo huduma hii ipo kila robo mwaka na taarifa ya mwaka zikiwemo
taarifa za wakaguzi wa hesabu wa nje (External Auditors) hivyo
tunamshukuru Mungu kuwa mpaka sasa Shirika la Compassion International
Tanzania limekuwa na mahusiano mazuri na kushirikiana na Serikali,
makanisa na jamii ya watu wote wanaotuzunguka na kushirikiana nao katika
malezi, makuzi na maendeleo ya kiujumla ya watoto na vijana” alisema
Mayala.
Alisema
katika Afrika Mashariki ukiondoa Tanzania shirika hilo lipo Rwanda,
Kenya, Uganda na Ethiopia na tayari limezalisha wasomi wengi wakiwemo
madaktari na wauguzi wahasibu, wanasheria na askari ambao kwa sasa
wamekuwa tegemeo kubwa kutokana na ufadhili unaotolewa na shirika hilo.
Shirika
hilo la compassion internation Tanzania lilianzishwa rasmi tarehe
30/4/1999 lengo ikiwa ni kuhudumia watoto wahitaji ili kuwatoa katika
umasikini wa kiroho,kiuchumi,kijamii na kimwili na baadae lilianzisha
ushirika wenza na baadhi ya makanisa ya kiinjili katika mikoa ya lindi
,mtwara,Iringa na Arusha ambapo ndio makao makuu.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269