Na Mwandishi Maalum, New York
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC) imetamka bayana kuwa, inajivunia mchango wake kupitia Force Intervention Brigade (FIB) inayoundwa na majeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi katika ulinzi wa wananchi wasio kuwa na hatia , urejeshwaji wa hali ya Amani na utulivu pamoja na kuling’oa kundi la waasi la M-23.
Siku ya Jumatano, Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilikuwa na mjadala wa wazi ulioandaliwa na Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa June ambaye ni URUSI.
Dhima ya mjadala huo wa wazi ililenga katika kuwapa fursa wajumbe wa Baraza hilo na wale wasio wajumbe kubadilishana mawazo kuhusu mwelekeo mpya wa Operesheni za ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Akizungumza kwa niaba ya SADC, Mwenyekiti wa SADC ambaye ni Muwakilishi wa Kudumu wa Malawi katika Umoja wa Mataifa, Balozi Charles Peter Msosa amesema, SADC ilikubali ombi Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa la kupeleka FIB ambayo iko ndani ya MONUSCO pamoja na matumizi ya mamlaka nguvu kama ilivyoainishwa kupitia Azimioa namba 2098 la mwaka 2013 la Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa.
“ Ni kwa ushirikiano wa karibu kati yetu (SADC) na Baraza Kuu la Usalama, ushirikiano uliotufanya tukakubali ombi la kutoa majeshi yetu kuunda FIB. Sisi SADC tunajivunia mchango wetu huo na tunajivunia FIB akasema Balozi Msosa.
Na kusisitiza. “Mamlaka nguvu ya FIB si tu yamechangia katika kuling’oa kundi la M-23, kundi ambalo lilikuwa likiendesha mambo yake bila pingamizi lolote,hata ikafikia mahali pachukua baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa chini ya dhamana ya MONUSCO. Lakini pia FIB imeweza kurejesha imani ya wananchi kwa MONUSCO. Tunajivunia kazi yetu hiyo nzuri na tutaendelea kushiriki kikamilifu” . Akasisitiza Balozi wa Malawi.
Aidha SADC kupitia msemaji wake huyo, imesema inatambua fika kuwa matumizi ya nguvu si suluhisho pekee la kumaliza vita vya muda mrefu katika eneo hilo la Mashariki ya Kongo.
Na kwamba michakato ya kisiasa ukiwamo mpango mpana wa amani, usalama na ushirikiano wa kiuchumi katika Eneo la Maziwa Makuu na ambao umeasisiwa na Umoja wa Mataifa ndiyo njia sahihi ya hatimaye kurejea kwa amani ya kudumu katika eneo hilo.
Aidha akasema, wakati SADC ikiwakumbuka walinzi wake wa amani waliopoteza maisha wakati wakitekeleza jukumu la ulinzi wa Amani, itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha amani na usalama katika eneo la Maziwa Makuu.
Wajumbe karibu 50 walizungumza wakati wa majadiliano hayo ambayo yalifunguliwa na Katibu Mkuu Ban Ki Moon. wengi wao licha ya kuzungumzia mwelekeo mpya wa mzima wa Operesheni za Ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa na changamoto zake, walioonyesha wazi kuunga mkono na kusifu kazi nzuri ya FIB chini ya MONUSCO.
Mjumbe wa Marekani Bw. Jeffrey Delaurentis katika mchango wake alisema, matumizi ya mamlaka nguvu kama ilivyofanya MONUSCO kupitia FIB imedhihirisha kuwa yanaweza kuleta mafanikio.
Naye mzungumzaji wa Malaysia Siti Hajjer Adrin alisema kutokana na changamoto kubwa inayowakabili walinzi wa Amani, pengine matumizi ya mamlaka nguvu yanaweza kuwa suluhisho la namna si tu ya kukabiliana na mabadiliko ya mwenendo mzima wa operesheni za ulinzi lakini pia kuwawezesha walinzi wa Amani kujilinda wao wenyewe dhidi ya mashambulizi.
Naye Muwakilishi wa Jordani alieleza kwamba uamuzi wa matumizi ya mamlaka nguvu si ya kwanza kufanywa katika shughuli za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa. Kwa kile alichosema imeshawahi kufanyika katika operesheni kadhaa huko nyuma na akaelezea kushangazwa wake na wale wanaoona kama jambo hilo ni geni kwa kuwa tu FIB ndo wamepewa mamlaka hayo.
Your Ad Spot
Jun 13, 2014
Home
Unlabelled
SADC YAJIVUNIA KAZI NZURI YA FORCE INTERVENTION BRIGADE (FIB)
SADC YAJIVUNIA KAZI NZURI YA FORCE INTERVENTION BRIGADE (FIB)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269