.

KENYA YAHATADHARISHA MADOLA YA KIGENI KUHUSU KUFADHILI VYAMA VYA UPINZANI

Oct 23, 2016

Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya Justin Muturi ametahadharisha kuhusu mpango wa baadhi ya madola ya kigeni kufadhili kampeni za vyama vya upinzani kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Akizungumza Jumamosi katika mji wa Fort Ternan Kaunti ya Kericho, Muturi amebaini kushtushwa na baadhi ya wafadhili wa kimataifa ambao wanapanga kutoa kiwango kikubwa cha fedha kufadhili vyama vya upinzani.
Ametahadharisha kuwa, mpango kama huo una maana kuwa wafadhili wa kimataifa wataingilia uchaguzi wa Kenya. Muturi amesema nchi nyingi duniani, ikiwemo Marekani, zimepiga marufuku vyama vya kisiasa kupokea misaada ya kigeni na kwa msingi huo Kenya pia inapaswa kuwa na sheria kama hiyo.
Kiongozi wa muungano wa CORD nchini Kenya, Raila Odinga
Hivi karibuni akiwa mjini London, kiongozi wa muungano wa upinzani wa CORD, Raila Odinga alitoa wito kwa madola ya magharibi kufadhili vyama vya upinzani. Tayari Naibu Rais wa Kenya William Ruto amemkosoa vikali Odinga kwa kile alichokitaja kuwa ni 'kusafiri nje ya nchi kuomba misaada ya kufadhili kampeni zake za uchaguzi'. Amesema Wakenya watapinga mpango wowote wa madola ya kigeni kuingilia uchaguzi wa nchi hiyo.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช