Breaking News

Your Ad Spot

Aug 11, 2014

CHADEMA WAMTWANGA MJUMBE BUNGE LA KATIBA


 Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta akimjulia hali Mjumbe wa Bunge hilo kutoka kundi la 201, Thomas Mgoli aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma  baada ya kujeruhiwa na watu wasiojulikana wakati akipata huduma katika duka moja lililopo karibu na mahali anapoishi Mjini Dodoma. (PICHA NA OWEN MWANDUMBYA)
Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa, akimjulia hali Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kundi la 201,Thomas Mgoli ambaye amelazwa katika Hospital ya Mkoa Dodoma baada ya kupigwa na vijana anaodai kuwa ni washabiki wa Chadema  eneo la Area D anakoishi akitokea kupata huduma dukani.Lowassa na Mgoli wako kamati na 12 ya bunge hilo.

WAKATI Bunge Maalumu la Katiba likiendelea mjini hapa, mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo anadaiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana huku tukio hilo likihusishwa na masuala ya kisiasa.

Mjumbe huyo aliyetambulika kama Thomas Mgori anayewakilisha kundi la wajumbe 201 anadaiwa kushambuliwa na kundi la watu watatu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Watu hao wanadaiwa kumshambulia mjumbe huyo wakimtuhumu kuwa ni kibaraka wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hali inayotafsiriwa kuwa ni mwiba kwa Chadema ambayo pamoja na vyama vingine viwili inaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akizungumza akiwa kitandani amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma (General), Mgori alidai kuwa alipigwa na kundi la watu ambao alidai aliwatambua kuwa ni wa jinsi ya kiume ambapo aliripoti polisi.

Alidai kuwa amekuwa akishutumiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema kwa hatua yake ya kutounga mkono Ukawa na hatimaye siku hiyo wakiwa sehemu ya kuburudika huko maeneo ya Area A mjini hapa akapatwa na masahibu hayo.

Akizungumza hospitalini hapo alikokwenda kumjulia hali mjumbe huyo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta alionya kuwa hivi sasa tunakwenda mahali pabaya hadi kufikia hatua ya kushambuliana.
Sitta alisema kuwa si jambo jema kwa watu kuanza kushambuliana na kuumizana kwa sababu tu ya mchakato wa Katiba mpya kwani jambo hili linashtua sana hasa kipindi hiki muhimu cha mstakabali wa taifa.

Alisema kuwa isifikie hatua ya kuanza kushambuliana hadi kuumizana tukiwa nje ya Bunge kwa sababu tu tunapingana kwa hoja na badala yake tunapaswa kufanya mijadala hiyo hata tukipingana kwa hoja tukiwa ndani ya Bunge.

Akitoa pole kwa mjumbe huyo, alisema kuwa kwa vile suala hilo tayari limefikishwa polisi hivyo anaamini watalifanyia kazi na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake dhidi ya watuhumiwa wakibainika.

Mjumbe huyo anayedaiwa kushambuliwa anatoka Kamati namba 12 ya Bunge Maalumu la Katiba ambalo hivi sasa kamati kamati hizo zimekuwa zikikutana kwa ajili ya kupitia Rasimu ya Pili ya Katiba.

Tayari Jeshi Polisi mkoani hapa kupitia kwa Kamanda wake, David Misime ilithibitisha kutokea kwa tukio hilo katika eneo hilo ambapo alisema kuwa tayari wanawashikilia watu hao kwa mahojiano.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages