Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza utaratibu wa uteuzi
wa wagombea wake watakaokiwakilisha chama hicho katika Uchaguzi Mkuu,
Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es salaam leo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar,
Salum Mwalim amesema kuwa utaratibu huo wa uteuzi katika ngazi ya
ubunge na uwakilishi utahusisha hatua tatu katika ngazi ya jimbo/wilaya
husika na hatua moja katika ngazi ya kitaifa huku ule wa udiwani ukiwa
na sehemu mbili katika kata na moja wilayani/jimboni.
Aidha,
kupitia mkutano na waandishi wa habari, Chadema pia imetangaza namna
watia nia wa nafasi mbalimbali watakavyochukua na kurejesha fomu huku
pia kikiweka wazi gharama za fomu kwa kila ngazi ya uteuzi yaani
udiwani, uwakilishi, ubunge na urais
“Kupitia mkutano wetu nanyi
ndugu wanahabari, tunapenda kuutarifu umma wa Watanzania hususan
wanachama wetu, wapenzi na wafuasi wote wenye sifa za kuwania uteuzi
kupitia CHADEMA kuwa kwa kuzingatia matakwa ya katiba ya chama na kukuza
demokrasia tukilenga kuhakikisha tunapata wagombea waadilifu, wenye
uwezo wa kuwatumikia watu na wanaokubalika na wapiga kura, chama
kimepanua wigo wa kupata maoni ya uteuzi,”alisema Mwalim.
Akirejea maazimio ya kikao
cha Kamati Kuu ya Chama kilichoketi Mei 3 na 4 jijini Dar es salaam,
NKMZ Mwalim amesema kuwa chama kimepitisha utaratibu huo utakaotumika
kupata maoni na hatimaye kufanya uteuzi wa wagombea watakaosimama
kugombea nafasi hizo tajwa kupitia CHADEMA katika ushirikano wa vyama
vinavyounda UKAWA.
Mwalim ameutaja utaratibu huo utakaotumika katika nafasi za ubunge/uwakilishi na udiwani, kuwa ni:
Ubunge/Uwakilishi
1. Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo
Mkutano huu utafanyika
kwenye kila jimbo la uchaguzi na utafanyika siku moja kwenye eneo moja
ambalo ni makao makuu jimbo au eneo ambalo litaamuliwa na vikao vya
chama.
Washiriki watatakiwa kuwapigia kura moja wagombea ambao wamejitokeza ndani ya chama na kura hiyo itakuwa ya siri .
NKMZ amesema kuwa
wasimamizi wa mikutano hiyo maalum ya kura ya maoni watatakiwa kuwa watu
ambao hawana ‘maslahi’ kwenye uchaguzi huo yaani wasiwe wagombea au
wasiwe na mgombea ambaye wanamuunga mkono kati ya wanaogombea nafasi
hiyo.
Kila mgombea atapewa fursa
ya kujieleza mbele ya wapiga kura kwa dakika tano (5) na ataulizwa
maswali yasiyozidi matatu kutoka kwa washiriki.
Kura zitapigwa mwishoni
baada ya wagombea wote kumaliza kujieleza mbele ya Mkutano Maalum wa
Kura ya Maoni , na kila mgombea atakuwa na haki ya kuweka wakala wa
kuhesabu kura zake.
Matokeo ya kura hizi yatawasilishwa kwenye Kikao Cha Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya kabla ya kufanya kikao chake cha uteuzi
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269