Breaking News

Your Ad Spot

Jun 20, 2015

CHILE YAIUA BOLIVIA 5-0, SANCHEZ KAMA KAWAIDA

Chile imetoa kipondo cha mbwa mwizi kwa Bolivia baada ya kuichakaza kwa jumla ya bao 5-0 ikiwa ni mchezo wa kundi A kwenye michuano ya kombe la Mataifa ya bara la America Kusini almaarufu kama Copa America mchezo uliomalizika alfajiri ya leo huko nchini Chile.
Charles Aranguiz alianza kuipatia Chile bao la mapema ikiwa ni dakika ya tatu tangu mchezo huo kuanza kabla ya winga wa Arsenal Alexis Sanchez kufunga goli la pili dakika ya 37 na kuifanya Chile iende mapumziko ikiwa mbele kwa goli 2-0 dhidi ya Bolivia.
Kipindi cha pili kilikuwa kibaya zaidi kwa Bolivia kutokana na Chile kulisakama lango lao kwa muda mwingi wa mchezo hali iliyopelekea wafanye makosa mengi kwenye safu yao ya ulinzi na kutoa mianya kwa Chile kufunga mabao.
Aranguiz alipachika pao la tatu kwa Chile dakika ya 66 lakini likiwa ni bao lake la pili kwenye mchezo huo, kabla Gary Medel hajatupia nyavuni goli la nne dakika ya 80. Zikiwa zimebaki dakika nne ili mwamuzi amalize pambano hilo, Raldes wa Bolivia alijifunga na kuufanya mchezao huo kumalizika kwa wenyeji wa mashindano (Chile) kuibuka na ushindi mnono wa goli 5-0.
Aturo Vidal alikuwepo kwenye kikosi kilichoifanyia mauaji Bolivia akitokea kwenye sekeseke la ajali ambayo aliipata kutokana na kuendesha gari kwa spidi kali huku akiwa amelewa. Lakini tofauti na matarajio ya wengi, Vidal bado alipata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wa Chile ambao wamefurahia pia timu yao kusonga mbele kwa hatua ya robo fainali kwenye michuanon hiyo.
Kwenye mchezo wa awali uliozikutanisha Mexico dhidi ya Ecuador kwenye mchezo wa kundi A, timu ya Mexico imetupwa nje ya mashindano ya Copa America baada ya kukubali kichapo cha goli 2-1 kutoka kwa Ecuador kwenye mechi ya mwisho ya timu za kundi A.
Miller Bolanos alianza kuipatia Ecuador bao la kuongoza dakika ya 26 kabla ya mshambuliaji wa West Ham Enner Valencia kuongeza goli la pili dakika ya 57 kwa upande wa Ecuador. Mexico walipata goli lao la kufutia machozi dakika ya 64 kwa mkwaju wa penati uliowekwa kambani na Raul Jimenez.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages