Picha ya kihistoria ya waasisi wa Uwahabi karne kadhaa zilizopita
Ni yangu matumaini kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni
kutegea sikio kipindi cha 24 cha makala yanayozungumzia chanzo cha
utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu.
Katika kipindi kilichopita tuliangazia macho namna ambavyo Ibn
Taymiyyah ambaye jina lake halisi ni Taqiyyud-Din Abul-Abbas Ahmad Ibn
Taymiyyah, alijikita katika kuwatusi Ahlul-Bayti wa Mtume hususan Imam
Ali (as) na kubuni hadithi bandia dhidi ya watukufu hao, huku
akiwasafisha watu wa ukoo wa Abu Sufiyan sanjari na kudhoofisha hadithi
sahihi na kinyume chake kuzifanya sahihi hadithi dhaifu katika
kukabiliana na ubora wa familia ya Mtume (as). Kwa hakika kile
kilichotawala katika Usalafi wa Ibn Taymiyyah ulikuwa ni Uislamu wa Bani
Umayyah tu. Ni Uislamu ule ambao Bani Umayyah walikuwa wakiulingania,
katika kuwachukia watu wa familia ya Mtume Muhammad (saw). Ni katika
fremu hiyo ndio maana naye Ibn Taymiyyah akajikita tu katika kuunga
mkono Uislamu huo sanjari na kuwapigia debe kwa kiasi kikubwa watu wa
ukoo wa Abu Sufiyan, huku akiyasafisha maovu yao na kupambana wazi wazi
na watu wa familia ya Mtume (saw) hususan Imam Ali (as) na watoto wake
wema. Hii ni katika hali ambayo, Imam Ahmad Ibun Hanbali si tu kwamba
alikuwa akiwapenda Ahlul-Bayti wa Mtume (saw), bali alijikita katika
kueneza mitazamo na mafundisho yao matukufu baina ya Waislamu. Ndugu
wasikilizaji mnapaswa kufahamu kwamba, Ibn Taymiyyah alisimama na
kupambana na madhehebu zote za Kiislamu kwa kuwatuhumu Waislamu kuwa
watu wa bidaa, ambapo aliwataja pia kuwa ni makafiri, na hivyo akawa
amepandikiza mbegu ya unafiki na mfarakano baina yao. Hii ni katika hali
ambayo katika maisha yake Imam Ahmad Ibn Hanbali, alijitahidi sana
kuweka misingi ya pamoja katika kuiunganisha mirengo tofauti ya watu wa
hadithi licha ya tofauti kubwa zilizokuwepo baina yao. Kiujumla ni
kwamba, Ibn Taymiyyah aliasisi mrengo wa kufurutu ada katika uga wa
itikadi ambapo athari yake hasi ilidhihiri katika karne ya 11 kupitia
linganio la Muhammad Ibn Abdul-Wahhab, mwasisi mkuu wa Uwahabi. Mrengo
huo wa kizushi wa Ibn Taymiyyah sanjari na kuimarishwa zaidi na wafuasi
wa Uwahabi karne kadhaa baadaye, uliwekewa rasmi jiwe la msingi la
kufurutu ada na ukufurishaji katika kipindi cha mwasisi wake Ibn
Abdul-Wahhab, mambo ambayo yalienda sambamba na utekelezaji wa umwagaji
mkubwa wa damu za Waislamu wa enzi hizo. Pamoja na kwamba Ibn Taymiyyah
katika zama zake hakufanikiwa kuibua kivitendo tofauti na mpasuko baina
ya Waislamu, lakini kwa upande wake Muhammad Ibn Abdul-Wahhab, aliweza
kutumia mafundisho na fikra ghalati za kuibua farqa na fitina za
shakhsia huyo (yaani Ibn Taymiyyah) na kwa uungaji mkono wa dola la
Aal-Saud lililosimama kwa upanga chini ya himaya kamili ya Uingereza,
kupandikiza mbegu hiyo chafu ya fitina baina ya umma wa Kiislamu na
hivyo kuusababishia hasara na maafa makubwa katika ulimwengu wa
Kiislamu. Mitazamo ya genge la Kisalafi ambalo liliwekewa jiwe la msingi
katika karne ya 11 na Ibn Taymiyyah, ilisambaratika baada ya kufariki
kwake dunia, licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na wanafunzi wake pinde
baada ya kufariki kwake dunia. Hata hivyo mitazamo hiyo iliibuka rasmi
katika karne ya 12 kwa aina na utaratibu mpya kwa jina la Uwahabi. Jina
la Uwahabi linatokana na mwasisi wa kundi hilo, Muhammad Ibn
Abdul-Wahhab. Kinyume kabisa na watu waliomtangulia, Ibn Abdul-Wahhab
aliweza kueneza mafundisho na fikra zake potofu katika maeneo ya Najdi
na Hijazi (Saudia) kupitia nguvu ya kisiasa na uungaji mkono kamili wa
Uingereza kwa upande mmoja na nguvu ya upanga kwa upande wa pili. Ni
katika kipindi hicho ndipo itikadi za Usalafi wa kitakfiri zilishika
kasi sanjari na kushuhudiwa mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu wa
Kisuni na Kishia wa maeneo hayo.
*************************************
Muhammad Ibn Abdul-Wahhab, alizaliwa mwaka 1115 Hijiria, katika mji
wa ‘Uyainah’ huku baba yake Sheikh Abdul-Wahhab, akiwa ni mmoja wa
masheikh maarufu wa dhehebu la Uhanbali na pia kadhi wa mji huo. Uyainah
ni eneo katika mji wa Najd ambao uko umbali wa kilometa 70 kutoka mji
mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh. Allamah Aaluusi, ambaye ni mmoja wa watu
waliokuwa na misimamo ya kufurutu ada na mfuasi wa Muhammad Ibn
Abdul-Wahhab anaeleza kuwa, katika mwaka ambao Sheikh Muhammad,
alitangaza wazi itikadi zake, alikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa
watu na maulama wa enzi hizo. Anaendelea kusema kuwa, muda fulani Sheikh
Muhammad Ibn Abdul-Wahhab alielekea mjini Makkah kwa ajili ya
kutekeleza ibada ya Hija, na baada ya hapo, akaelekea mjini Madina kwa
ajili ya kujiendeleza kielimu. Akiwa mjini hapo, na bila ya kuwa na
elimu ya kutosha, alianza kuwakataza Waislamu kwenda kuzuru kaburi la
mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kudai kuwa eti jambo hilo ni ushirikina.
Baada ya kutoka mjini Madina, Ibn Abdul-Wahhab alielekea Najdi na kisha
mjini Basra, Iraq. Watu wa mji wa Basra ambao tayari walikuwa wamepata
habari juu ya itikadi potofu za shakhsia huyo yaani Ibn Abdul-Wahhab,
walimfukuza mjini humo. Kwa hakika maisha ya Muhammad Ibn Abdul-Wahhab
yaliyojaa matatizo mengi, yalienda sambamba na kuibua fikra za utakfiri
ambazo zilisababisha mauaji ya watu wengi.
****************************************
Karne ya 12 Hijiria ambayo ni sawa na karne ya 18 na 19 Miladia,
ilikuwa karne maalumu ambapo Waislamu walishuhudia matatizo chungu
nzima. Hii ni kwa kuwa katika kipindi hicho kulishuhudiwa wimbi la
ukoloni wa madola ya kibeberu dhidi ya nchi za Kiislamu. Uingereza
ambayo kwa miaka mingi ilikuwa ikiikalia bara Hindi, ilitaka kuendeleza
ukoloni na kujizatiti kwake katika eneo hilo kwa kutumia mabadiliko ya
mitaala ya masomo. Kwa kutumia mbinu hiyo, Uingereza iliweza kujitanua
na kuidhibiti jamii ya Kiislamu ya India na vizazi vya baadaye nchini
humo. Huku hali ikiwa ni hivyo huko India, Ufaransa nayo chini ya
uongozi wa Napoleon, ilizikalia kwa mabavu nchi za Misri, Syria na
Palestina, nayo Urusi ya zamani sanjari na kutekeleza hujuma mtawalia
dhidi ya Iran na dola la Othmania, ikafanya njama za kutanua wigo wake
wa kisiasa na kijografia kupitia mikataba yake ya kikoloni katika nchi
hizo.
Mfalme wa Othmania ambaye alikuwa amevaa vazi la Kisuni, alikuwa
akipitia kipindi kigumu kufuatia kudhoofika utawala wake huku
akikabiliwa na hatari kuporomoka kabisa utawala huo. Katika mazingira
hayo, ulimwengu wa Kiislamu uliokuwa unakabiliwa kwa kiasi kikubwa na
hatari ya kuporomoka, ulikuwa unahitajia sana umoja na mshikamano kwa
ajili ya kukabiliana na changamoto hizo za mabeberu. Uislamu ulikuwa
unahitajia nguvu ya pamoja ya Waislamu kwa ajili ya kuwaandalia uwezo wa
kukabiliana na adui wao wa pamoja. Hata hivyo katika mazingira hayo
hatari, Mawahabi si tu kwamba hawakusaidia kwa aina yoyote katika kuunda
umoja wa Waislamu, bali ndio kwanza walipandikiza mbegu ya unafiki,
farqa na uadui baina ya Waislamu, sanjari na kushirikiana bega kwa bega
na wakoloni na hivyo kuwafungulia mlango wa kupenya zaidi katika nchi za
Kiislamu, suala ambalo lilitoa pigo kubwa kwa Waislamu. Ni katika
kipindi hicho hicho ndipo Muhammad Ibn Abdul-Wahhab, kwa kutumia misaada
ya mtawala wa ukoo wa Aal-Saud kwa upande mmoja na msaada wa Uingereza
kwa upande wa pili, akafanikiwa kueneza mafundisho na fikraza zake
potofu katika ardhi ya Hijaz (Saudi aya leo).
Wapenzi wasikilizaji kitu kinachomtambulisha mtu msomi, ni athari
zake za kielimu, au walimu na wanafunzi wanaojinasibisha na msomi huyo.
Hata hivyo kwa upande wake Muhammad Ibn Abdul-Wahhab, kinyume na
alivyokuwa mtangulizi wake, (yaani Ibn Taymiyyah), alipitia hali ngumu
ya umasikini wa elimu na mali. Hii ikiwa na maana kwamba, Ibn Taymiyyah
alikuwa mwandishi mkubwa huku akiwa na wanafunzi kama vile, Ibn Qayyim
na Ibn Kathir, ambao walikuwa mashuhuri katika zama hizo. Hata hivyo
Muhammad Ibn Abdul-Wahhab, si tu kwamba hakuwa mwandishi, bali pia hata
vitabu na athari zinazonasibishwa kwake, zimeendelea kutiliwa shaka na
maulama wa Kiislamu juu ya usahihi wake. Kwa hakika kitu ambacho
kilifanikisha kuenea kwa fikra potofu za Ibn Abdul-Wahhab, haikuwa hoja
zake za kielimu, hekima, wala busara, bali ilikuwa ni upanga, na nguvu
ya kisiasa ya Aal-Saud na kadhalika Waingereza.
******************************************
Wapenzi wasikilizaji muda uliotengewa kipindi hiki umefika ukingoni.
Msikose kuungana nami katika sehemu ya 25 ya mfululizo wa vipindi hivi.
Mimi ni Sudi Jafar Shaban, hadi wiki ijayo ninakuageni kwa kusema:
Kwaherini.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269