Kikao cha kila mwaka cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa
Mataifa kimeanza leo Jumatatu mjini Geneva, Uswisi na hafla ya ufunguzi
imehudhuriwa na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki moon.
Mkutano huo wa kila mwaka unafanyika katika hali ambayo dunia
inazidi kushuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika maeneo na
mataifa mbalimbali. Mfano hai wa hilo ni kuendelea uvamizi na mauaji
yanayoendeshwa na Saudi Arabia na nchi waitifaki wa Kiarabu pamoja na
utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Yemen.
Jinai ya hivi karibuni kabisa ya Saudia Arabia na waitifaki wao dhidi ya
Yemen ni lile shambulizi la anga la wavamizi hao dhidi ya soko moja la
umma karibu na mji mkuu, Sana'a ambapo watu kadhaa wakiwemo wanawake na
watoto waliuawa.
Kituo cha haki za binadamu nchini Yemen hivi majuzi kilichapisha
ripoti inayoweka wazi takwimu za kusikitisha kuhusiana na hasara, maafa
na uharibifu uliosababishwa na hujuma za Saudi Arabia ndani ya muda wa
takriban mwaka mmoja uliopita. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangu mwezi
Machi mwaka jana hadi mwezi Januari mwaka huu, watu zaidi ya 8 000
wameuawa huko Yemen ambapo 236 kati yao ni watoto wadogo na 752 ni
wanawake. Ni kutokana na maafa na uharibifu huo wa Saudia dhidi ya Yemen
ndio maana shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International
likataka jamii ya kimataifa isitishe uuzaji silaha kwa serikali ya
Riyadh.
Mbali na vita vya Saudia dhidi ya Yemen, dunia pia inashuhudia
ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu barani Ulaya hususan katika kadhia
ya wakimbizi. Idadi kubwa ya wahajiri wamepoteza maisha kutokana na
kuzuiwa kuingia katika baadhi ya nchi za Ulaya na wengine wamefariki
dunia kutokana na kuwekwa katika mazingira ya kusikitisha barani humo.
Hili linafanyika katika hali ambayo wakimbizi hao wanakimbia vita na
machafuko ambayo yameanzishwa na nchi hizo hizo za Magharibi katika
mataifa yao ya asili. Huku mkutano wa kila mwaka wa Baraza la Haki za
Binadamu la Umoja wa Mataifa ukifanyika, kadhia hiyo ya wahajiri
inatarajiwa kutawala mijadala ya washiriki katika siku kadhaa zijazo.
Washiriki kwenye mkutano wa haki za binadamu mjini Geneva pia
wanatarajiwa kuzamia kadhia ya Palestina na jinai zinazotendwa kila
uchao na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina. kiburi cha
utawala huo kimekuwa kikitokana na ukimya wa jamii ya kimataifa hususan
taasisi za haki za binadamu za Wamagharibi pamoja na Baraza la Haki za
Binadamu la UN mbele ya jinai za Wazayuni.
Kwa maneno machache tunaweza kusema kuwa, utepetevu na mughafala wa
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika kutekeleza
majukumu yake vimepelekea kuongezeka matukio ya ukiukaji wa haki za
binadamu katika maeneo mbalimbali duniani.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269