Kutokana na kushtadi ukatili na unyama wa Saudi Arabia dhidi ya
wananchi wa Yemen taasisi mbalimbali za kimataifa na shaksia wakubwa
wametaka vikwazo vya silaha vipitishwe mara moja dhidi ya utawala wenye
kupenda vita wa familia ya Aal Saud.
Katika kile kinachonekana kama ushaidi wa wazi kwamba Riyadh ni
miongoni mwa nchi zenye kupenda vita Mashariki ya Kati, utawala huo
umekithirisha manunuzi yake ya silaha kwa asilimia 279. William Hartung,
mtaalamu wa masuala ya silaha katika kituo kinachofuatilia sera za
kimataifa (CIP) ameandika makala ndefu akizungumzia mwenendo wa manunuzi
ya silaha ya Saudia Araba. Anasema kati ya mwaka 2011 hadi 2015, Riyadh
imeongeza mrundikano wake wa silaha mbalimbali kwa zaidi ya asilimia
275. Hartung anasema asilimia kubwa ya silaha hizo zinatoka Marekani na
Uingereza.
Taasisi nyingine ya kimataifa iliyozungumzia kuongezeka bajeti ya
silaha ya Saudi Arabia katika miaka ya hivi karibuni ni ile
inayofuatilia misaada ya kiusalama maarufu kama SAMM. Taasisi hiyo
imesema uagizaji silaha wa Saudi Arabia kutoka Marekani umeongezeka kwa
asilimia 96 katika kipindi cha uongozi wa Rais Barack Obama
ikilinganishwa na kipindi cha George W. Bush. Pia taasisi hiyo ya
kimataifa imesema Wasaudi wasiopungua 2 500 wamepata mafunzo ya kijeshi
nchini Marekani katika kipindi hicho.
Umoja wa Ulaya kupitia bunge lake umezitaka nchi wanachama
kusimamisha uuzaji wa silaha kwa serikali ya Riyadh kutokana na silaha
hizo kutumika kuwaua kinyama wananchi wasio na hatia wa Yemen. Takwa la
kusimamishwa uuzaji wa silaha kwa Saudia pia limetolewa na Muungano wa
mashirika na taasisi za kutoa misaada ya kibinadamu (Oxfam) ambao
umesema Riyadh imepelekea hali ya kibinadamu nchini Yemen kuwa mbaya
kupindukia. Oxfam imesema kwenye ripoti yake ya hivi karibuni kwamba
viongozi wa dunia wanaokutana mwezi Aprili nchini Uswisi kujadili
biashara ya silaha wanapaswa kupitisha kwa kauli moja vikwazo vya silaha
dhidi ya Saudia na waitifake wake ambao wanaendeleza uvamizi na mauaji
dhidi ya raia wa Yemen.
Saudi Arabia imeongeza bajeti yake ya silaha katika miaka ya hivi
karibuni sambamba na kukithirisha vitendo vya uvamizi na uingiliaji wa
mambo ya ndani wa baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati kama vile Bahrain
na Yemen.
Amnesty international ni taasisi nyingine ya kimataifa ambayo imetoa
ripoti maalumu inayoonyesha uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu
inayofanywa na Saudi Arabia na waitifaki wake dhidi ya Yemen. Kwa
mantiki hiyo, taasisi hiyo ya kutetea haki za binadamu imetoa wito wa
kuchukuliwa hatua za haraka na kivitendo za kusimamisha uuzaji wa silaha
kwa watawala wa Riyadh.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269