Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kutuma
kikosi cha maafisa wa polisi wa umoja huo nchini Burundi kwa lengo la
kudhibiti hali ya mambo nchini humo.
Nchi 15 wanachama wa baraza hilo kwa kauli moja zimepasisha
rasimu ya azimio iliyoandaliwa na Ufaransa ya kutuma maafisa wa polisi
ambao hawajajizatiti kwa silaha kwenda nchini Burundi kudhibiti hali na
kuzuia ukiukaji wa haki za binadamu.
Azimio hilo limemtaka Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu wa umoja huo kwa
ushirikiano na viongozi wa Umoja wa Afrika pamoja na serikali ya
Bujumbura kuandaa orodha ya kikosi hicho cha polisi katika muda wa siku
15 zijazo.
Wakati huo huo, Tume Huru ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Burundi
imeeleza wasi wasi kuhusiana na hali ya kiusalama na kisiasa nchini
humo.
Jean-Baptiste Baribonekeza, Mwenyekiti wa tume hiyo amesema watu
zaidi ya 380 wamekwishauawa kufikia sasa tangu mgogoro wan chi hiyo
uanze Aprili mwaka jana. Baribonekeza amesema hadi kufikia sasa
wamepokea kesi 747 za ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu tangu
mwaka jana 2015. Kadhalika Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kutetea Haki za
Binadamu nchini Burundi amesema kuwa watu 19 wametekwa nyara
wasijulikane waliko na kwamba wengine 27 wamefanyiwa ukatili na dhulma
za kutisha wakiwa kizuizini.
Aidha Jean-Baptiste Baribonekeza amefichua kuwa watu zaidi 31,200
wanazuiliwa na vyombo vya usalama nchini humo tangu mwaka jana.
Zaidi ya watu 400 wameripotiwa kuuawa na wengine karibu laki mbili na
40 elfu wamekuwa wakimbizi tangu Burundi ilipotumbukia kwenye machafuko
yaliyotokana na Rais Nkurunziza kuamua kugombea tena urais nchini humo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269