Kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek Machar amewasili katika mji
mkuu wa nchi hiyo, Juba na kuapishwa kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo.
Machar ameapishwa kuwa makamu wa rais katika serikali inayoongozwa na
hasimu wake wa muda mrefu, Rais Salva Kiir. Machar alichelewesha
kuwasili Juba kwa miezi kadhaa jambo ambalo liliikasirisha jumuiya ya
kimataifa ambayo imehusika katika kuwaleta mahasimu hao wawili pamoja
ili wagawane madaraka katika nchi hiyo changa zaidi duniani.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha
mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa
wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais
Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake za zamani, Riek
Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua
serikali yake.
Kwa mujibu wa mapatano ya amani yaliyotiwa saini Addis Ababa
Ethiopia, kutakuwa na serikali ya mpito itakayodumu kwa muda wa miezi
30. Kiir atachukua asilimia 53 ya viti serikalini huku upande wa Machar
ukipata asilimia 33 na wafungwa wa zamani wa kisiasa na vyama vingine
vya kisiasa vikipata asilimia 7 kila mmoja
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269