Polisi ya Misri amekabiliana vikali na wapinzani wa siasa za
serikali ya Rais Abdulfattah as-Sisi wa nchi hiyo huku ikiwarushia gesi
ya kutoa machozi.
Mamia ya Wamisri jana Jumatatu walifanya maandamano makubwa mjini
Cairo mji mkuu wa nchi hiyo wakimtaka as-Sisi aondoke madarakani.
Waandamanaji hao wanapinga kukabidhiwa Saudi Arabia visiwa viwili vya
Misri vya Sanafir na Tiran. Kufia sasa polisi ya nchi hiyo imewakamata
watu wapatao 23 katika miji tofauti ya nchi hiyo. Kabla ya kufanyika
maandamano hayo, maelfu ya askari kutoka kikosi cha polisi na jeshi la
nchi hiyo walikuwa wamewekwa katika sehemu nyeti na muhimu za mji mkuu
huo, na hasa katika medani ya at-Tahrir ambacho ni kituo muhimu cha
kuanza mwamko na mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011. Maandamano ya jana
ni ya pili kufanyika katika mwezi huu wa Aprili katika kulalamikia
kupewa Saudia visiwa viwili vilivyotajwa na serikali ya as-Sisi. Visiwa
hivyo muhimu vya Sanafir na Tiran viko kwenye lango la Ghuba ya Aqabah.
Wakati huohuo utawala haramu wa Israel na Jordan zina bandari muhimu
katika ghuba hiyo. Kuna nadharia kadhaa zinazotolewa kuhusiana na sababu
za kukabidhiwa Saudi Arabia visiwa hivyo. Tokea kuingia madarakani Rais
as-Sisi hapo mwaka 2013, watawala wa Saudia wamekuwa wakiipa serikali
ya as-Sisi misaada mingi ya kifedha na kisiasa. Jenerali as-Sisi
alinyakua madaraka ya Misri baada ya kuing'oa madarakani serikali halali
ya Muhammad Mursi kupitia mapinduzi ya kijeshi.
Katika safari rasmi ya Mfalme Salman wa Saudia nchini Misri ambayo
ilianza tarehe 11 Aprili visiwa viwili vya Sanafir na Tiran
vilikabidhiwa kwa utawala wa Saudia. Hamdeen Sabahi mpinzani wa pekee wa
as-Sisi katia uchaguzi uliopita ndiye aliyefichua habari ya kukabidhiwa
visiwa hivyo vya Misri kwa Saudia. Alisema ukabidhi huo unakwenda
kinyume na katiba ya Misri ambayo inapiga marufuku kukabidhiwa kwa ardhi
ya nchi hiyo kwa nchi nyingine. Inasemekana kwamba Misri ilikabidhi
visiwa hivyo kwa lengo la kupewa dola bilioni 20 na Saudia. Pamoja na
hali hiyo serikali ya Misri inadai kwamba askari wa Misri walitumwa kwa
muda kwenye visiwa hivyo kwa lengo la kwenda kulinda usalama kutokana na
ombi lililotolewa kwa serikali ya Misri mwaka 1950 na mfalme wa wakati
huo wa Saudi Arabia, Abdul Aziz.
Hata hivyo wapinzani wa serikali ya Cairo wanasisitiza kwamba kwa
mujibu wa mkataba wa 1906 uliotiwa saini kati ya mfalme wa Othmania na
serikali ya Uingereza mipaka ya baharini kati ya Misri na Saudi Arabia
iliainishwa na ufalme wa Othmania, ambapo visiwa viwili vya Sabafir na
Tiran viliwekwa ndani ya mipaka ya Misri. Kuhusu suala hilo Khalid Ali,
mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu anakusudia kuwasilisha
mahakamani faili la kalalamikia kukabidhiwa visiwa hivyo kwa Saudia.
Wataalamu wa mambo wanasema kwamba kwa kuzingatia kuongezeka upinzani
dhidi ya serikali ya Abdulfattah as-Sisi, wanasheria na wanaharakati
wengine wa kisiasa watashirikiana na Khalid Ali katika kufuatilia suala
la kukabidhiwa visiwa viwili vilivyotajwa kwa utawala wa Saudi Arabia.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269