Breaking News

Your Ad Spot

Jul 12, 2016

SERKALI YATANGAZA LEO KUMFUNGIA DK. MWAKA KUTOA TIBA ASILIA

Na Ally Daud-Maelezo
Serikali imefungia kituo cha tiba asilia cha Foreplan kinachomilikiwa na Tabibu Juma Mwaka Juma kwa kudaiwa kukiuka masharti ya kibali alichopewa kwa kujitangaza kuwa anatoa tiba za kisasa badala ya matibabu ya asilia.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti Wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Dk. Edmund Kayombo amesema kuwa kituo hiko kimefutiwa usajili na hakiruhusu kutoa huduma za tiba asilia na Tiba mbadala kwa jamii kwa kutokidhi masharti ya usajili na kufanya kazi kinyume cha usajili wake.

“Kuanzia hivi sasa tumekifutia usajili kituo cha tiba asili na tiba mbadala cha Foreplan kwa kukiuka masharti ya usajili na hivyo hakiruhusiwi kutoa huduma kwa jamii  na watanzania kwa ujumla”, alisisitiza Dkt. Kayombo.

Aidha Dkt. Kayombo ameongeza kuwa vituo vingine vilivyofungiwa kutoa huduma ni pamoja na Tabibu Abdallah Mandai wa Mandai Herval Clinic na kituo cha Fadhaget Sanitarium Clinic kinachomilikiwa na tabibu Fadhil Kabujanja.

Dkt. Kayombo aliendelea kwa kusema kuwa, ukiacha waliofungiwa kutoa huduma pia vipo vituo vilivyofungiwa kwa miezi sita kila kimoja kama vile tabibu Simon Rusigwa wa kituo cha Sigwa Herbal Clinic na Tabibu John Lupimo wa kituo cha Lupimo Sanitarium Clinic.

Mbali na hayo Dkt. Kayombo amesema kuwa huduma za tiba asili na tiba mbadala zinagusa zaidi maisha na afya za wananchi moja kwa moja na hivyo sio vyema zikaachwa ziendeshwe kiholela bila utaratibu wa kitaalamu na kimaadili.

“Kutokana na huduma hizo kutolewa kiholela, waratibu wote mnatakiwa kufuatilia na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waganga wote ambao hawajajisajili na kutoa taarifa katika Ofisi ya Msajili wa Baraza la tiba asili na tiba mbadala kwa kila hatua iliyochukuliwa” aliongeza Dkt. Kayombo.

Aidha Dkt. Kayombo amesisitiza kwamba kila mtoa huduma lazima asajiliwe yeye mwenyewe, wasaidizi wake pamoja na kituo chake cha kutolea huduma kupitia ofisi za Mganga Mkuu wa Halmashauri husika.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages