.

MDAHALO WA MWISHO WA TRUMP NA CLINTON, MBIO ZA UCHAGUZI WA RAIS MAREKANI

Oct 21, 2016

Mdahalo wa tatu na wa mwisho wa televisheni wa wagombea uchaguzi wa rais Marekani kwa mara nyingine tena umegubikwa na utata huku mada kuu zikiwa ni kufichuliwa nyaraka za WikiLeaks zinazomhusu mgombea wa chama cha Democrat Hillary Clinton, wahamiaji, sera za kigeni na kashfa za kimaadli za Donald Trump, mgombea wa chama cha Republican.
Mdahalo huu, kama ile iliyotangulia, umekumbwa na majibizano makali baina ya Clinton na Trump hasa katika masuala ya sera za kigeni na wahajiri. Akizungumza katika mdahalo huo uliofanyika Jumatano katika Chuo Kikuu cha Nevada huko Las Vegas, Hillary Clinton alidai kuwa: "Russia inafanya ujasusi ili kujipenyeza katika uchaguzi, na Trump amekuwa akihimiza jambo hilo."Clinton alisema kuwa, Russia inataka Rais wa Marekani ambaye atakuwa kibaraka wake.
Katika kujibu tuhuma hizo, Trump amesisitiza kuwa hana ukuruba wala urafiki na Rais Vladimir Putin wa Russia na kuongeza kuwa, kinyume na Obama, Rais Putin amefanikiwa katika sera zake za kieneo ikiwa ni pamoja na nchini Syria.
Katika wiki za hivi  karibuni Trump amekumbwa na kashfa za kuwadhalilisha kijinsia wanawake na jambo hilo limeibua makelele mengi ndani na nje ya Marekani. Tump amesema madai hayo hayana msingi na kwamba yamezushwa na idara ya hasimu wake. Vilevile Trump amedai kuwa wafuasi wa Hilary Clinton wamevuruga  mikutano yake ya kampeni. Trump pia amegusia tena suala la uwezekano wa kutokea wizi wa kura katika uchaguzi ujao wa rais nchini Marekani. Amesema Clinton hapaswi kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani kutokana na kashfa ya baruapepe au Email zake.
Clinton na Trump
Masuala mengine ambayo yaliashiriwa katika mdahalo huo ni kuhusu utumiaji wa mabomu ya atomiki, uchumi wa Marekani, kodi, misaada kutoka Saudi Arabia na sera za Marekani huko Syria na Iraq.
Kwa kumalizika mdahalao huo wa wagombea urais wa Marekani, katika kipindi cha wiki tatu zijazo, Wamarekani watamchagua mmoja kati ya Trump na Clinton kuelekea Ikulu ya White House. Midahalo mitatu ya urais ambayo imefanyika baina ya wagombea hao wawili imebaini changamoto ambazo Marekani inakabiliana nazo.
Matatizo ya kiuchumu, mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira, mishahara duni na utozaji kodi ni maudhui ambazo wagombea hao wawili waligusia. Wawili hao waliafikiana kuwa umasikini na matatizo ya kiuchumi ni nukta mbili zinazowasumbua Wamarekani. Aidha ukosefu wa usalama na ongezeko la mauaji mitaani ni tatizo kubwa ambalo Wamarekani wanakabiliana nalo kwa sasa. Takwimu zinaonyesha kuwa, watu elfu 33 huuawa kila mwaka nchini Marekani kutokana na silaha ambazo hubebwa na raia nchini humo.
Wagombea wawili wa urais Marekani wamesisitiza ulazima wa kufanyika marekebisho katika sheria za kumiliki silaha. Ubebeji silaha na polisi kuwalenga na kuwaua kiholela Wamarekani wenye asili ya Afrika ni kati ya matatizo makubwa nchini Marekani. Trump amesisitiza kuhusu kupitishwa sheria ya kuwazuia wahajiri wa kigeni kuingia Marekani. Matatizo hayo yote yanaikumba Marekani ambayo inadai kuwa ni mbeba bendera ya demokrasia duniani.
Wamarekani weusi wanabaguliwa Marekani
Weledi wa mambo ya kisiasa wanasema mdahalo wa Jumatano iliyopita ulikuwa wa aina yake kutokana na kiwango cha kuvunjiana heshima na kufichuliwa kashfa za ufisadi wa kimaadili, na kwamba mambo hayo ni changamoto kubwa ya kitaifa na kimataifa kwa taifa la Marekani.
Kila mgombea amejaribu kulaumu chama cha mwenzake kuwa ndio chanzo cha matatizo ya sasa ya Marekani. Hivi sasa inasuburiwa kuona ni yupi kati ya wagombea hao wawili ataweza kuchaguliwa katika uchaguzi wa Novemba 8 ili kukabiliana na changamoto chungu nzima za Marekani.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช