.

MAMIA WAKAMATWA MISRI KWA 'KUITISHA MAANDAMANO'

Nov 14, 2016

Vyombo vya usalama nchini Misri vimewasweka mbaroni mamia ya wafuasi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin, kwa tuhuma za kuitisha maandamano dhidi ya serikali.
Duru za habari zinaarifu kuwa, watu 229 wamekamatwa na polisi ya Misri tangu Ijumaa iliyopita, kwa 'kuitisha na kuonyesha kuwa tayari' kutekeleza wito wa maandamano uliotolewa na wanaharakati wa Ikhwan.
Habari zaidi zinasema kuwa, 78 miongoni mwao walikamatwa katika mji mkuu Cairo, 104 kutoka mkoa wa Beheira Kaskazini na 21 kutoka eneo la Minya, kusini mwa mji mkuu Cairo.
Polisi wakitumia mabomu ya kutoa machozi kuzima maandamano mjini Cairo
Alkhamisi iliyopita, idadi kubwa ya askari usalama na wajeshi wa Misri walionekana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kwa shabaha ya kukabiliana na maandamano ya wananchi dhidi ya serikali ya Rais Abdul Fattah al-Sisi.
Tangu siku kadhaa zilizopita wanaharakati wa Misri walianzisha kampeni kubwa katika mitandao ya kijamii wakitoa wito wa kushiriki kwa wingi wananchi katika maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Ijumaa kwa jina la 'Mapinduzi ya Watu Maskini'. Sababu kuu ya wito huo ni kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi na kijamii nchini Misri.
Rais wa Misri, Abdul Fattah al-Sisi
Aidha misikiti ya mikoa yote 27 ya nchi hiyo ilifungwa mara tu baada ya kumalizika swala ya Ijumaa kwa amri ya Waziri wa Wakfu wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช