Breaking News

Your Ad Spot

Nov 25, 2016

WATUMISHI WAWILI WASIMAMISHWA KAZI,WANNE WAKALIA KUTI KAVU-KIGOMA

NA MAGRETH MAGOSSO,KIGOMA

WATUMISHI wawili wa Idara ya fedha  kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji,Jimbo la Kigoma Mjini mkoani kigoma,wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za matumizi mabaya  ya  fedha  kiasi cha Sh. Milioni 290 kutoka Akaunti  miradi ya maendeleo  na kuhamishiwa  katika shughuli zingine  kinyume cha sheria,kanuni na taratibu za fedha.
                                                                         
Akithibitisha hilo  jana Ofisini kwake mbele ya Jamboleo Meya wa Manispaa hiyo Hussein Ruhava alisema hatua hiyo imekuja baada ya kikao cha kamati ya fedha  kubaini madudu katika matumizi ya fedha hizo ambazo zilipangwa katika miradi mbalimbali ya wananchi na kamati ya nidhamu ilibariki kusimamishwa kwao ni sehemu ya uwajibikaji .

“watumishi hawa  ni pamoja na mtunza fedha Christina Nyumainzu na Michael Malko ambaye ni mkuu wa idara ,kamati ya fedha na uchumi iligundua hili,washukiwa wakaletwa katika kikao cha baraza la madiwani,kila mmoja alijieleza alivyotumika na kubaini wawili hawa wasimame kuja kazini na wengine kuchunguzwa ” alisema Meya.

Alibainisha kuwa,awali watumishi hao walishiriki katika matukio mawili tofauti  katika kipindi cha Machi-Novemba mwaka huu kwa utoaji wa fedha kinyume cha taratibu kwa  kushirikiana na wenzao wanne ambapo walihamisha fedha kiasi cha sh.milioni 42 kutoka akaunti ya  amana na kuziingiza katika akaunti  ya maendeleo cha kushangaza Christina siku ya uhamishaji wa fedha hizo akaunti yake  iliingizwa sh.milioni 40.

Ruhava alifafanua kuwa mbali na tuhuma hiyo ,kamati  ilibaini kiasi cha sh.milioni 250 zilitumika sivyo ndivyo ambazo zote ni za miradi ya umma na fedha zingine ni za wahisani ambao wana miradi mtambukwa akitolea mfano watu kutoka TSP,ilhali matumizi ya ndani ya manispaa zinatumia fedha za mapato ya ndani.

“kuna mashaka ya watumishi hawa wawili ambao wanadhamana ya kutoa na kuingiza fedha za manispaa ya kigoma ujiji,lakini kuna hawa wanne wanachunguzwa wakiwa kazini kwa kuwa hawawezi kuharibu ushahidi ni pamoja na Eng.Sultan Ndiliwa ,Hamisi Dongwala,Ruth Barnabas na Dkt John  Shauri” alifafanua Ruhava.

Pia wamepewa siku 14 za kujieleza kwa mandishi kwa mujibu wa sheria ya maadili na nidhamu kazini ya mwaka 2002/3 na tume ipo kwa ajili ya kuchunguza undani wa watuhumiwa hao na kupitia mapendekezo ya tume sheria itachukua mkondo wake siku za usoni.

Aliongeza kuwa,uhamishwaji wa fedha katika akaunti ya maendeleo ya jamii inashirikisha walengwa na si watu wachache waliojifungia ofisini,lakini wao hawakushirikisha baraza la madiwani wala utawala wa juu kwa madai ya matumizi ya kawaida ya manispaa hali inayotia shaka kwa ujumla.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages