Breaking News

Your Ad Spot

Dec 31, 2016

WATU 13,626 WALIKAMATWA NA POLISI MA KUFIKISHWA MAHAKAMANI DAR KWA TUHUMA ZA UJAMBAZI NADAWA ZA KULEVYA

KIKOSI cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imekamata jumla ya watuhumiwa 13,626 na kuwafikisha mahakamani kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo dawa za kulevya na ujambazi wa kutumia silaha kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2016.

Aidha, hali ya uhalifu wa kutumia silaha katika jiji la Dar es Salaam umepungua, ukilinganisha na mwaka uliopita wa 2015 na matukio yanayoongezeka kwa wingi ni ya ubakaji na ulawiti.

Akitoa tathmini ya mwaka mmoja, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha yamepungua kutoka 204 mwaka jana hadi 127 mwaka huu.

Idadi hiyo ni pungufu ya matukio 77, sawa na asilimia 37.7 huku matukio ya kutumia nguvu yamepungua kutoka 1,181 mwaka jana hadi 874 sawa na asilimia 26.

Kamishna Sirro alifafanua kuwa matukio ya mauaji, yamepungua kwa asilimia 11 ukilinganisha na mwaka jana, ambapo kulikuwa na jumla ya matukio 327 wakati kwa mwaka huu ni matukio 291 pungufu ya matukio 36.Alisema matukio ya ubakaji, yameongezeka kutoka 972 mwaka jana hadi 1030 mwaka huu, sawa na asilimia sita wakati matukio ya ulawiti yameongezeka kutoka 310 mwaka jana hadi 383 mwaka huu sawa na asilimia 23.5.

‘’Kwa matukio ya ubakaji yaliyoongezeka ni 58 na ulawiti matukio yaliyoongezeka ni 73. Lakini wizi wa watoto umepungua kutoka 26 mwaka jana hadi matukio 19 mwaka huu sawa na asilimia 27,’’ aliongeza.

Kwa mujibu wa Sirro, matukio ya uvunjaji yamepungua kwa asilimia 5.7 ambapo kwa mwaka jana kulikuwa na matukio 5,677 na mwaka huu matukio 5,355 sawa na upungufu wa matukio 322.Kwa upande wa wizi wa magari, umepungua kwa asilimia 18.1 kutoka matukio 392 hadi 321 mwaka huu huku wizi wa pikipiki ukipungua kutoka pikipiki 2,644 mwaka jana hadi 2,191 ambapo matukio 453 yamepungua sawa na asilimia 17.1.

Wizi wa mifugo umepungua kutoka 197 mwaka jana hadi 163 mwaka huu sawa na asilimia 17.3 ikiwa ni pungufu ya matukio 34.

“Sababu za kuongezeka au kupungua kwa matukio hayo kumetokana na juhudi za polisi wa kuzuia na kupambana na uhalifu kwa kufanya doria pamoja na misako mbalimbali iliyosaidia kukamatwa kwa wahalifu wa makosa mbalimbali pamoja na raia wema ambao wametoa taarifa za siri ili kugundua makosa hayo,’’ alieleza Sirro.

Akielezea watuhumiwa hao, Sirro alisema kuwa kati yao 52 walikutwa na silaha za kivita 67 na risasi 1,076, na watuhumiwa 126 walikutwa na dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 75 na gramu 254.

Pia alisema kuwa watuhumiwa 7,625 walikutwa na bangi kilo 2,843 na gramu 78 huku watuhumiwa 269 walikutwa na cocaine kilo tatu na gramu 255 na heroine kilo moja na gramu 654.

‘’Watuhumiwa 5,627 walikutwa na pombe haramu ya gongo lita 8,547 na mitambo 34 na tuliwafikisha mahakamani. Pia tumekamata wahamiaji haramu 105 kutoka mataifa mbalimbali ambao hawana kibali cha kuingia na kuishi nchini,’’ alisema Sirro.

Katika hatua nyingine, Sirro alisema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watu wanne wakiwa na gari moja aina ya Noah lenye namba za usajili T 188 CZN rangi nyeupe ambalo liliibwa mkoani Kilimanjaro.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Erasto Edward (36), mkazi wa Kawawa Moshi, Wilson Kapori (37) mkazi wa Njia Panda Himo mkoani Kilimanjaro, Hussein Issah (32) mkazi wa Chanika na David Marwa mkazi wa Pugu Kajiungeni.


Watuhumiwa hao walikamatwa Desemba 21 mwaka huu, saa 5 asubuhi katika misako maeneo ya Tabata Bima. Watuhumiwa walitumia ufunguo bandia kuiba gari hiyo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages