Mivutano ya kisiasa ya baada ya uchaguzi wa
rais nchini Gambia ingali inaendelea huku Mahakama Kuu ya nchi hiyo
ikisubiriwa kutangaza uamuzi wake kuhusiana na malalamiko
yaliyowasilishwa na Rais Yahya Jammeh ya kupinga matokeo ya uchaguzi
huo.
Jammeh
ametangaza kuwa hatokabidhi madaraka; lakini rais mteule wa nchi hiyo
Adama Barrow ametoa wito tena kwa kiongozi huyo kumtaka angátuke
madarakani na kueleza kwamba hata dola la kikoloni la Uingereza nalo
lilikubali kukabidhi mamlaka ya nchi hiyo kwa njia ya amani.
Rais
mteule wa Gambia ameongeza kuwa: "Wakati muda wa urais wa Jammeh
utakapomalizika, mimi nitapaswa kula kiapo. Sitaki kushika hatamu za
uongozi wa nchi kukiwa hakuna amani. Ninatoa wote kwa wananchi wote
wapenda amani wa Gambia kufanya jitihada za kuhakikisha makabidhiano ya
madaraka yanafanyika kwa njia ya amani.
Sambamba
na hayo, Adama Barrow amesema kuna timu ya wataalamu ambayo ameipa kazi
ya kufuatilia suala hilo na kwamba tayari ameunda tume maalumu ya
kufanya maandalizi ya makabidhiano ya madaraka.
Japokuwa kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini Gambia,
wachambuzi walikuwa tayari wameshatabiri kwamba mivutano ya kisiasa
itaibuka katika kipindi cha baada ya uchaguzi huo, lakini hatua Rais
Yahaya Jammeh ya kutangaza kuwa amekubali kushindwa hata kabla ya
kutangazwa matokeo rasmi ya uchaguzi iliwashangaza watu wote hususan
waangalizi wa kimataifa.
Baada
ya kupita siku chache tangu kiongozi wa upinzani kutangazwa mshindi,
huku kila mtu akiutathmini uamuzi wa rais Jammeh kama hatua ya
kufanikisha demokrasia nchini Gambia na kuhakikisha amani na uthabiti
unatawala, katika hali isiyotarajiwa, kiongozi huyo alibadilisha ghafla
msimamo wake na kutangaza kuwa hakubaliani na matokeo ya uchaguzi na
hatokabidhi madaraka kwa rais mteule aliyechaguliwa na wananchi. Msimamo
huo mpya wa Rais Jammeh uliwashangaza tena Wagambia na jamii ya
kimataifa. Alingángánia msimamo wake huo na kutaka kuitishwa tena
uchaguzi wa rais.
Nchi
nyingi za eneo la magharibi mwa Afrika pamoja na taasisi za kimataifa
zimechukua msimamo juu ya suala hilo kwa kumtaka Jammeh aheshimu matokeo
ya uchaguzi na kukabidhi madaraka, lakini hatua zote za mashauriano
zilizochukuliwa hadi sasa zimeshindwa kuwa na tija.
Hii ni katika hali ambayo hapo kabla pia Rais wa Gambia alikuwa
akikabiliwa na lawama mbalimbali kwa sababu ya kutoheshimu haki za
binadamu, kubinya uhuru wa kisiasa, kujenga mazingira ya vitisho na hofu
na kutumia mabavu na mkono wa chuma dhidi ya wapinzani.
Hivi
sasa wasiwasi umezidi kuongezeka wa kushtadi hali hiyo na kutumika tena
mkono wa chuma na ukandamizaji dhidi ya wapinzani na hatimaye
kuitumbukiza Gambia kwenye lindi la vita vya wenyewe kwa wenyewe. Na hii
ni katika hali ambayo nchi za magharibi mwa Afrika zinapigania
kurejesha amani na uthabiti katika kwa kupambana na makundi ya kigaidi
yanayotishia amani na usalama wa eneo hilo. Hivi sasa juhudi za
kidiplomasia na mashauriano ya jumuiya na taasisi za kisiasa za eneo
zimeongezeka ili kumshawishi Jammeh abadilishe tena msimamo wake lakini
jibu analotoa ni kwamba atakabidhi madaraka endapo tu Mahakama Kuu
itamwamuru kufanya hivyo. Mahakama hiyo inatazamiwa kutangaza uamuzi
wake mnamo siku kadhaa zijazo; lakini wapinzani wengi wanasema uamuzi
utakaotolewa utakidhi matakwa ya Jammeh.
Pamoja na yote hayo, juhudi za kisiasa na kidiplomasia zinaendelea
kufanywa ili kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Gambia na kuhakikisha
Rais Yahya jammeh anakabidhi madaraka kwa rais mteule Adama Barrow. Hii
ni kwa sababu kuzuka vita vingine vya ndani katika eneo la magharibi mwa
Afrika kunaweza kusababisha madhara mengi kwa nchi jirani na eneo zima
kwa jumla…/
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269