Breaking News

Your Ad Spot

Dec 28, 2016

MIILI YA WAHAJIRI 11 YAPATIKANA UFUKWENI MJINI TRIPOLI, LIBYA

Shirika la Hilali Nyekundu la Libya limesema miili 11 ya wahajiri waliokufa maji wakijaribu kuelekea barani Ulaya imepatikana katika fuo za mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Mohannad al-Fallah, afisa wa Hilali Nyekundu ya Libya amenukuliwa na shirika la habari la AFP leo Jumatano akisema kuwa, baadhi ya miili hiyo imepatikana katika operesheni iliyofanyika jana katika ufuo wa Hay al-Andalus mjini Tripoli na mingine imepatikana katika fuo zilizoko kilomita 15 magharibi mwa mji mkuu Tripoli.
Habari zaidi zinasema kuwa, wahajiri hao walikuwa wanakusudia kuelekea nchini Italia kwa kutumia boti ndogo za plastiki, kupitia Bahari ya Mediterranea.


Wahajiri wa Kiafrika wakielekea Italia
Hivi karibuni, Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) lilisema wakimbizi na wahajiri wapatao 5,000 wamepoteza maisha mwaka huu wa 2016 wakijaribu kuingia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea.
Joel Millman, msemaji wa shirika hilo amesema idadi hiyo imeongezeka baada ya watu 100 kufa maji Alkhamisi iliyopita, baada ya boti mbili walizokuwa wakisafiria kuzama katika Lango la Sicily, kati ya Italia na Libya.
Naye William Spindler, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amesema kiwango hicho cha vifo baharini mwaka huu kimevunja rekodi na kwamba hakuna mwaka ambao umewahi kushuhudia vifo vya wahajiri baharini kiasi hiki.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages