Breaking News

Your Ad Spot

Jul 10, 2017

HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA CHINI YA RC MAKONDA WANUFAISHA WAKAZI 80, 000 DAR

NA MWANDISHI MAALUM
Aakiitikia agizo la Rais John Pombe Magufuli alilowataka wateule wake kuwa wabunifu na kujituma ili kuwaondolea wananchi shida mbalimbali , Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametatua migogoro takribani 8, 000 iliyowahusisha zaidi ya watu 80, 000 ndani ya takribani miezi minane kati ya Disemba mwaka jana na Mwezi Juni mwaka huu.

Makonda ametekeleza jukumu hilo kupitia timu ya wanasheria 35 wanaojitolea kutoa huduma ya msaada wa kisheria bure kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam.

Kiongozi wa timu ya Wanasheria hao, Georgia Kamina, aliitaja baadhi ya migogoro ambayo timu yake imekuwa ikisuluhisha kupitia Ofisi za Wakuu wa Wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni ile ya umiliki wa ardhi na michakato ya mirathi mahakamani na katika ngazi ya familia,
Migogoro mingine ambayo timu hiyo ya wanasheria imekuwa ikimsaidia Makonda kuitatua kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya ya Ilala  (Sofia Mjema), Kinondoni (Ally Hapi), Temeke (  Felix Lyaniva ), Ubungo (Kisare Makori ) na Kigamboni (_Hashimu Mgandilwa ) ni pamoja na  ndoa na matunzo ya watoto kwa ndoa zilizo sambaratika,  ajira na mikataba ya ajira, ubakaji, faili kupotea mahakamani, ucheleweshwaji wa kesi mahakamani, umiliki wa nyumba,  umiliki au mauziano ya ardhi, mikopo kutoka mabenki ya biashara, uuzwaji mali mbalimbali kwa kukiuka sheria au makubaliano na hata ukosefu wa uaminifu.

Akizungumza kwa niaba ya Makonda, katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Ilala Boma, Kamina, alitaja migogoro wanayopokea na  inayotia fora katika mkoa wa Dar es Salaam  kuwa ni ile inayohusisha masuala ya mirathi, umiliki wa ardhi, ajira na mikataba kati ya waajiri na waajiriwa, ndoa na matunzo ya watoto kwa ndoa zilizo sambaratika na baadhi ya wananchi kuingia mikataba mibovu na mabenki katika harakati za kupata mitaji ya biashara.

Sehemu ya Jiji la Dar es Salaam
"Mheshimiwa Paul  Makonda alichukua jukumu la kuanzisha huduma ya msaada wa  kisheria bure kwa wananchi kutokana na uzoefu alioupata katika ziara ya kukutana na wananchi aliyofanya mkoa mzima mwezi Novemba mwaka jana," alibainisha Kamina na kuongeza kuwa ili kuwaepusha wananchi na mchakato mrefu na unaoumiza wa kumaliza migogoro yao mahakamani aliamua kuunda timu ya wanasheria wa kujitolea ili kutekeleza dhamira hiyo ya kuwasaidia wananchi wenye migogoro mbalimbali ya kisheria.

Kiongozi wa timu ya wanasheria hao aliongeza kwa kusema kuwa Mkuu wa Mkoa aliguswa na namna baadhi ya wananchi walivyokuwa wakipoteza mashamba, nyumba, mali na hata kufukuzwa kazi kwa uonevu kwa kukosa uelewa wa sheria.

“Ili kupata suluhisho la matatizo hayo hapo juu na kwakuwa yeye binafsi akiwa msaidizi wa Rais kwa mkoa wa Dar es Salaam basi ndio akaja na wazo la kuanzisha kitengo cha kutatua migogoro ya kisheria kwa njia ya kutoa huduma ya msaada kisheria bila malipo kwa wananchi katika kila wilaya ya mkoa wa Dar es Salaam.

"Tupo jumla ya wanasheria 35 ambao tumegawanyika katika Wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam yaani  Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo na Kigamboni. Tukiwa katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya nilizotaja tunafanya kazi nao kwa karibu sana na pengine wakati mwingine tunajumuika na  Makatibu Tawala  wa Wilaya husika (DAS) na hata wakati mwingine Wakurugenzi Watendaji wa manispaa za mkoa wa Dar es Salaam katika kutatua migogoro hiyo kisheria,” alifichua Mkuu huyo wa Timu ya Wanasheria.

Akizungumzia uzoefu waliopata katika kipindi cha miezi saba walichofanya kazi ya kutoa huduma ya msaada wa kisheria bure  kwa wananchi kwa kusuluhisha migogoro mbalimbali wamegundua wananchi wengi ama hawana au wana uelewa mdogo wa sheria na kila wakati wanafanya makosa makubwa ya kisheria yanayoishia kuwaumiza kimaisha.

"Kuna kina baba na kina mama wengi tu wamekuja mara baada ya kunyang'anywa nyumba zao na mabenki kutokana na kukubali kutoa hati za nyumba hizo kudhamini mikopo ya jamaa zao wakiamini kuwa kama kutakuwa na kutokuelewana kati ya mabenki na ndugu zao nyumba hizo hazitauzwa jambo ambalo sio kweli," alisimulia Kamina.

Akitaja baadhi ya migogoro iliyowagharimu muda na juhudi za ziada kuisuluhisha, Kamina alitaja mgogoro wa umiliki wa ardhi ya hekari 28 unaomhusisha Ogwari Nashon na wakazi wa kijiji cha Viwege, Mbondela eneo la Chanika katika Wilaya ya Ilala.

“Mgogoro huu ulifika mahala ukahatarisha maisha ya ndugu Nashon kwani baadhi ya wanakijiji wasioheshimu sheria walivamia eneo lake, kuchoma moto majengo na kuharibu mazao kama mihogo, mananasi na michungwa.

Mara baada ya Nashon kuja ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Ilala alikutanishwa na wanasheria wa  Mkuu wa Mkoa  wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria  bure kwa wananchi walioko wilayani hapo na kueleza tatizo lake ambapo timu yetu iliingilia kati  kwa kushirikiana na Mkuu wa wilaya ya Ilala Sofia Mjema, ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huo.

Ni jambo la kutia faraja kwa sasa tumepiga hatua kubwa kuelekea kutatua mivutano iliyokuwepo kwani Nashon ana vielelezo halali vya nyaraka za kiserikali zinazothibitisha umiliki wa eneo hilo," alibainisha Kamina.

Licha ya kujitokeza picha nzuri iliyojaa mafanikio ya huduma hii ya msaada wa kisheria kwa wananchi   katika  Mkoa wa Dar es Salaam, Habari Leo imearifiwa juu ya changamoto lukuki zinazowakabili watoa huduma hiyo katika kutekeleza majukumu yao.
Baadhi ya changamoto hizo ni wananchi kutokuwa na uelewa wa sheria, kanuni na taratibu za kukopa fedha kwa watu binafsi na katika taasisi za fedha, wananchi hawana uelewa wa sheria na taratibu za mirathi na hata wasimamizi wa mirathi hawajui wajibu wao kwa warithi na kwa mahakama jambo ambalo linapelekea warithi kuchelewa au kutopatiwa haki zao hata baada ya mchakato wa mirathi kukamilika katika Mahakama.

“Katika eneo la ajira huko ndio kunatisha kwa uvunjaji wa sheria za ajira na nchi uliokithiri kwani makampuni mengi hasa ya ujenzi na ulinzi hayatoi mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, wakati mwingine mikataba inakuja kutolewa baada ya mwajiriwa kuwa amekwisha fanya kazi muda mrefu na inapotolewa inakuwa inakiuka makubaliano ya awali,” alisema na kuwanyooshea kidole viongozi wa serikali za mitaa na kata, katika baadhi ya maeneo kwa kuwa chanzo cha migogoro kwa kufanya majukumu ambayo si yao kisheria na uendeshwaji wa kesi mahakamani kuchukua muda mrefu pasipo na sababu za msingi huku Mabaraza ya kata nayo kuwa dhaifu katika kutekeleza majukumu yake ya kimsingi katika kuwahudumia wananchi na hasa wale wa kipato cha chini.
Akizungumzia huduma hiyo, Makonda alisema aliamua kuanzisha huduma ya msaada wa kisheria kupitia wanasheria hawa (35) katika kila wilaya ya mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoagiza kusikiliza na kutatua kero au malalamiko ya wananchi.

Mkuu huyo wa Mkoa alifafanua kuwa katika ziara ya mkoa wa Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka 2016 aligundua  wananchi wengi hawakuwa na uelewa wa sheria jambo lililowafanya kupoteza haki zao aidha kwa kutapeliwa, kuonewa au kutojua mahala sahihi pa kupeleka matatizo hayo.

"Pamoja na changamoto nyingi zinazoambatana na huduma hii ya kutafuta suluhu ya matatizo ya wananchi kwa kuzileta pande husika mezani kuongea bado nina dhamira ya kuendelea kuwasaidia Watanzania wenzangu kwa juhudi na maarifa yangu yote.
Na hii ndio gharama ya kuteuliwa na Rais, unapoteuliwa na Mkuu wa nchi anakuwa na matarajio mengi kutoka kwako. Mimi nimeamua kufanya ninayoweza kwa nguvu na juhudi zote ili kumuondolea Rais John Pombe Magufuli na mashinikizo juu ya shida mbalimbali za Wana Dar es Salaam," alimaliza Makonda.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages