Rais wa Zanzibar ambae pia ni
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amesema uhuru wa
mahkama ni suala la msingi na lenye umuhimu mkubwa katika kujenga
utawala bora nchini.
Hayo ameyasema huko Victoria
Garden Wilaya ya Mjini Unguja katika maadhimisho ya Siku ya Sheria
Zanzibar, Dkt Shein amesema ili Mahkama iendelee kuwa huru mihili
mengine haipaswi kuingilia katika maamuzi yake kama ilivyo hapa nchini
hivyo ni muhimu kwa majaji, wanasheria, mahakimu, mawakili na wahusika
wa kada ya sheria kutekeleza majukumu yao bila ya hofu na upendeleo kwa
kuzingatia katiba na sheria ziliopo.
Rais Shein amesema uhuru huo
utakuwepo pindi patakapokuwa na taasisi zilizo huru zilizowekwa kikatiba
na kisheria zenye kufanya kazi zake kwa uadilifu na mashirikiano.
Amewataka wananchi kufanya jitida
ya kuzielewa sheria mbali mbali zilizopo ambazo ni muhimu katika
kusimamia maisha ya kila siku kwani Mahkama ina dhamana ya kutekeleza
majukumu yake bila ya kuingiliwa kutokana na uhuru uliopewa kwa
kuzingatia sheria.
“Mahkama inatakiwa kuwa chombo au
taasisi huru, uhuru kwa maana ya kuwa huru wale wote waliopewa jukumu na
katiba la kutoa haki ya kuamua mtu kuwa mkosa au hana hatia lazima awe
huru kutokana na shindikizo bila ya kujali anakotoka, Mahkama iwe huru
kutokana shindikizo la Kisiasa, Kiutawala na Kihisia ikiwa inataka
kufanya kazi zake kwa uadilifu unaofuata sheria mama ambayo ni Katiba
pia Mhkama haitakiwi kulazimishwa au kupokea vitisho vya aina yoyote” ,
amefahamisha Dkt Shein.
Akizungumzia kuhusu suala la
Rushwa nchini Dkt Shein amesema kuwa tafiti mbali mbali zilizofanywa
nchini na mashirika ya Kimataifa kuhusu tatizo la Rushwa na Uhujumu wa
Uchumi zinaonyesha kuwa mambo hayo ndio yanayokwamishwa maendeleo ya
nchi zinazoendelea hivyo amewataka wananchi kuongeza kasi ya mapambano
katika kuchukia Rushwa na kuwa mstari wa mbele katika kulinda mali na
maslahi ya Umma.
Nae Waziri wa Katiba na Sheria
Mhe. Abubakar Khamis Bakari amesema ucheleweshaji wa kesi Mahkamani
unasababisha mashahidi na wazee kuwa wagumu katika kutoa mashirikiano
hata hivyo chombo husika kinaendela kufanya mbinu za kulitatua tatizo
hilo.
Mapema Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar
Othaman Makungu amesema uhru wa Mahkama ni kutoa haki bila ya upendeleo,
woga wala kupokea rushwa na kufuata misingi ya sheria katika utoaji wa
haki.
Ametanabahisha kuwa dhana ya
kufuata sheria ndio kigezo muhimu katika utawala bora kwani hupelekea
kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma hivyo amewataka
watumishi hao kufuata sheria kikamilifu katika kuwahudumia wananchi ili
waweze kupata haki zao bila usumbufu wa aina yoyote.
Amesema kuwa wasimamizi wa sheria
watoe haki bila ya upendeleo na kuitumia sheria bila ya kuogopa na
kumhofia mtu yeyote kwani ndiko kutakowafanya watu kuridhishwa na
maamuzi yanayotolewa na Mahakama na kuepusha vurugu jambo
litakalopelekea nchi kuwa yenye amani na usalama.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269