JAMII YATAKIWA KUWASAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM – MAMA SALMA KIKWETE
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimpongeza mtoto Mohammed Hashim mara baada ya kuimba wimbo wa Taifa.
……………………………………………………………………………………..
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama
Salma Kikwete ameitaka jamii kutumia sauti zao kuwasemea watoto wenye
mahitaji maalum kwani watoto hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali
na hawana mtu wa kumwambia matatizo yao.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo jana alipotembelea kitengo
cha wanafunzi wenye mahitaji maalum kilichopo shule ya Msingi Mpilipili
wilaya ya Lindi mjini.
Alisema watoto wenye mahitaji
maalum wanakabiliwa na changamoto nyingi ukilinganisha na watoto
wengine pia matatizo yao hayafanani hivyo basi ni jukumu la kila mtu
katika jamii kuwasaidia watoto hao ili waweze kuishi kama watoto
wengine.
“Katika kitengo hiki kuna watoto
wenye tatizo la usonji (Autism) na wasiosikia (viziwi), kila mtoto
anahitaji lake na pale anapokabiliwa na tatizo anatakiwa kusaidiwa kwa
haraka ili asijisikie kunyanyapaliwa. Nawapongeza walimu mnaowafundisha
watoto hawa kwani kazi hii ni ngumu na inahitaji moyo wa ziada”,
alisema Mama Kikwete.
Akisoma taarifa ya kitengo cha
wanafunzi wenye mahitaji maalum mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Mpilipili Fadhili Mtitima alisema kitengo hicho kilianzishwa mwaka 1993
kikiwa na wanafunzi watano na hivi sasa kuna wanafunzi 20 wenye tatizo
la usonji 16 kati yao wavulana ni 16 na wasichana wawili na wasiosikia
(viziwi) wawili msichana mmoja na mvulana mmoja.
Mwalimu Mtitima alisema njia
zinazotumika kuwapata wanafunzi hao ni wanafunzi wa kawaida kutoa
taarifa ya uwepo wa watoto wenye mahitaji maalum katika mitaa yao kwa
walimu, wazazi ambao wamehamasika huwaleta watoto kujiunga na shule,
kutoa hamasa na matangazo kwa jamii katika maadhimisho ya wiki ya elimu
kwa wote na kupitia sensa ya watoto inayofanyika kila mwaka.
“Changamoto zinazotukabili ni
watoto wengi wanaoishi mbali na kitengo wanakosa fursa ya kupata elimu
kutokana na umbali uliopo, baadhi ya wazazi wa watoto wenye ulemavu
hawawaandikishi watoto wao wakiwa na imani kuwa watoto hawa
hawafundishiki, idadi ya walimu haitoshelezi kwani kuna walimu wawili
kati ya wanne wanaohitajika kufundisha watoto wenye tatizo la usonji.
“Kitengo hakina mwalimu mtaalamu
wa elimu ya walemavu wasiosikia na walimu kutojitokeza kujiendeleza
katika mafunzo ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum”, alisema
Mwalimu Mtitima.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269