Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Uongozi wa
Wizara ya Kilimo na Mali Asili wakati alipotembelea eneo liloathirika
kwa moto kwenye Hifadhi ya Msitu wa Jozani Mkoa wa Kusini Unguja. Mwanzo
kushoto ni Waziri wa Kilimo na Mali Asili Zanzibar Dr. Sira Ubwa
Mwamboya na Katbu Mkuu wa Wizara hiyo Nd. Afan Othman Maalim.
Baadhi
ya sehemu za miti iliyoathirika kwa moto kwenye msitu wa Hifadhi ya
Jozani ambao kwa sasa umedhibitiwa baada ya juhudi za vikosi vya ulinzi
kwa kushirikiana na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja.
Baadhi
ya sehemu za miti iliyoathirika kwa moto kwenye msitu wa Hifadhi ya
Jozani ambao kwa sasa umedhibitiwa baada ya juhudi za vikosi vya ulinzi
kwa kushirikiana na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja.
Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Nd. Afan Othman Maalim akimueleza
Balozi Seif aliyepo kati kati yao jinsi vikosi vya ulinzi na wananchi
walivyofanikiwa kuudhibiti moto ulioibuka ndani yam situ wa Jozani.
Balozi
Seif akiwapongeza askari na Makamanda wa vikosi vya ulinzi
walivyofanikiwa kuuzima moto ulioibuka ndani ya msitu wa Hifadhi ya
Jozani Mkoa wa Kusini Unguja.
Na Othman Khamis Ame
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa pamoja na Waziri wa
Kilimo na Mali Asili Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya wakitembelea baadhi
ya maeneo yaliyoathirika kwa moto kwenye msitu wa Hifadhi wa Jozani. (Picha zotea na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/2/2015.
VIKOSI
vya ulinzi na Uokozi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Wizara ya
Kilimo na Mali Asili pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja
wamefanikiwa kuuzima moto katika Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Jozani
ulioibuka upande wa magharibi ya msitu huo maarufu Jozani Kovu.
Hekta
zipatazo 17 kati ya elfu 5,000 zilizomo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya
Msitu huo zimeathirika kwa moto unaodhaniwa kuibuka juzi jioni
kutokana na wavunaji haramu wa Asali.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika eneo la tukio
kuangalia athari iliyotokea kwenye msitu huo wenye hadhi ya Kimataifa
kutokana na mazingira yake ya miti pamoja na wanyama adimu Duniani.
Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar Nd. Afan Othman Maalim
alimueleza Balozi Seif kwamba juhudi za vikosi vya ulinzi kwa
kushirikiana na wananchi wa Vijiji Jirani imesaidia kuudhibiti moto huo
usiingie kwenye msitu mkubwa.
Katibu
Mkuu Afan alisema unyevunyevu uliopo kwenye eneo hilo { Maarufu kwa
jina la Kigeni Ground Water Floor } nao umechangia kuepusha athari zaidi
za kuenea kwa moto huo kwa kutoathiri miti mikubwa.
“
Tumepata faraja kubwa baada ya kuona moto huo uliunguza majani ya chini
bila ya kuathiri ile miti mikubwa. Hii inatokana na mazingira ya eneo
lenyewe kuwa na unyevunyevu “. Alisema Nd. Afan Othman Maalim.
Alifahamisha
kwamba wakulima wa Bonde la Cheju wamekuwa wakitegemea vianzio vya
maji vilivyomo kwenye msitu wa Jozani ambavyo vinastahiki kulindwa kwa
njia yoyote.
“
Hadhi ya Kimataifa iliyopo katika hifadhi ya Msitu wa Jozani inaweza
kupotea iwapo uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo hautadhibitiwa “.
Alisisitiza Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar.
Alisema
kuathirika kwa msitu huo mbali ya kuchafuka kwa mazingira katika eneo
hilo la hifadhi ya Taifa lakini pia kilimo cha mpunga katika Bonde la
Cheju kinaweza kuwa hatarini kutoweka kwa kukosa rasilmali ya maji.
Akitoa
shukrani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na uongozi wa Serikali ya
Mkoa wa Kusini Unguja kuchukuwa hatua za kukabiliana na wagemaji haramu
wa asali ili kujaribu kuzuia uharibifu wa mazingira.
Balozi
Seif alisema kwa niaba yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
amevipongeza Vikosi vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi kutokana
na juhudi kubwa walizochukuwa za kufanikiwa kuuzima moto huo.
Alifahamisha
kwamba Jozani ikiwa ni miongoni mwa Misitu miwili mikubwa katika Visiwa
vya Zanzibar Ukiwepo sambamba na ule wa Ngezi Kisiwani Pemba lazima
iendelee kudhibitiwa kwa nguvu zote.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa Idara ya Maafa kwa
kushirikiana na Taasisi za Kimataifa itaangalia njia za kufanya utafiti
utakaosaidia kutoa taaluma kwa Jamii juu ya kuendelea kuhifadhi
rasilimali hiyo ya Taifa.
Naye
Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar Mkoa wa Kusini
Unguja { SSF } Shaaban Ramadhan Ali alisema kikosi hicho bado
kinaendelea kukumbwa na changamoto ya vifaa na usafiri katika
utekelezaji wa majukumu yake.
SSP
Shaaban Ramashan alisema yapo matukio ya maafa yanayotokea katika
baadhi ya sehemu ambayo Kikosi chake kinakuwa na mazingira magumu
kukabiliana nayo kutokana na miundo mbinu duni.
“
Tunapata matatizo wakati tunapokabiliana na majanga kama moto katika
maeneo kama haya kwa kukosa gari zenye kiwango cha maji kinachotosheleza
nguvu za kukabiliana na janga halisi “. Alifafanua SSF Shaaban
Ramadhan.
Hifadhi
ya Taifa ya Msitu wa Jozani imekuwa maarufu kimataifa kutokana na
maumbile yake ya kuwa na viumbe mchanganyiko wakiwemo wanyama adimu
kama kima punju, Paa Nunga, nguruwe, Vipepeo na aina mchanganyiko ya
ndege.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269