Meli
kubwa MSC Martina yenye urefu wa mita 244 na upana wa mita 32.2 ikiwa na
uwezo wa kubeba makontena 2,411 imefanikiwa kutia nanga katika Bandari
ya Dar es Salaam.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka, Mhandisi Madeni Kipande amesema, mafanikio
hayo ni juhudi zilizofanywa na Mamlaka kuzitangaza bandari zake pamoja
na uboreshwaji wa huduma.
“Ujio huu
wa meli kubwa za mizigo kama hizi ni faraja kubwa sana kwetu kwani pia
utaongeza uingiaji wa mizigo kwa wingi na hatimaye kuleta unafuu kwa
mtumiaji wa mwisho,” alisema Mhandisi Kipande. MSC Martina Kampuni ya
Mediterranean Shipping Company (MSC) ni miongoni mwa meli kubwa na za
kisasa ambazo zimefanikiwa kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam
na kupakia na kupakua mzigo.
Meli
nyingine kubwa na ya kisasa kuja nchini kwa mara ya kwanza ilikuwa ni
Maersk Cubango mali ya Maersk Line iliyokuwa na urefu wa mita 250 na
upana wa mita 38 ikiwa na uwezo wa kubeba kontena 4,500.
Mhandishi
Kipande ameomba ushirikiano uliopo kati ya Mamlaka na mawakala wa meli
uendelee ili kuleta ufanisi zaidi na amewataka mawakala wengine kuleta
meli kubwa kama walivyofanya, Maersk and Mediterranean.
Kwa
upande wake Nahodha aliyeingiza meli hiyo ndani ya Bandari ya Dar es
Salaam, Abdulah Mwingamno alisema mabadiliko ya teknolojia yameongeza
uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia meli kubwa zaidi.
“Tuliweza
kuingiza meli yenye urefu wa mita 250 ya kampuni ya Maersk iitwayo
Maersk Cubango na sasa tumeingiza meli nyingine kubwa ya kampuni ya MSC
iiitwayo MSC Martina yenye urefu wa mita 244, haya ni mafakio makubwa
kwetu,” alisema.
Nahodha
Mwingamno aliongeza kwamba meli hiyo ya mizigo iliingia salama katika
lango la Bandari ya Dar es Salaam bila tatizo lolote kama ziingiavyo
meli nyingine. Alisema kwamba ujio wa meli hiyo na kufanikiwa kutia
nanga katika bandari yetu bila tatizo lolote ndio kumefungua milango kwa
meli hiyo na nyingine za aina hiyo kuanza safari zake kuja Dar es
Salaam.
“Tunatarajia
ujio wa meli kubwa zaidi ya hii yenye urefu wa mita zipatazo 260 katika
bandari yetu kwenye miezi ya Machi na Aprili mwaka huu,” alisema. Naye
mwakilishi wa kampuni ya meli hiyo ya MSC nchini, Ndugu Ahmed Kamal
alisema kwamba wanatarajia kuleta meli kubwa zaidi nchini, kwani kampuni
yao ina meli kubwa zaidi zinazotia nanga katika bandari nyingine
Duniani.
“Hii ni
meli kubwa ya kwanza ya kampuni yetu kuja nchini lakini lengo letu ni
kuleta meli kubwa zaidi ya hii nchini,” amesema Kamal.
Meli
nyingine kubwa zaidi zilizowahi kutia nanga katika Bandari ya Dar es
Salaam zilikuwa na urefu wa mita 220 na mita 234, zikiwa na uwezo wa
kubeba makontena kati ya 2800 na 3000. Awali meli zilizokuwa
zinaruhusiwa kuingia katika bandari ya Dar es Salaam hazikutakiwa kuzidi
urefu wa mita 234.
Imetolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) S.L.P. 9184
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269