Katibu
Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kushoto) akitoa
maelezo ya kumkaribisha Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na
Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Kulia) wakati alipofanya ziara ya
kujitambulisha kwa Tume ya Mipango.
Waziri
wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu
(Wapili kushoto) akizungumza na baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Rais,
Tume ya Mipango alipotembelea na kujitambulisha Tume ya Mipango.
Wanaomsikiliza ni Katibu Mtendaji, Dkt. Philip Mpango (Kushoto), Naibu
Katibu Mtendaji (Miundombinu na Huduma), Mhandisi Happiness Mgalula
(Wapili kulia) na Naibu Katibu Mtendaji (Biashara za Kimataifa na ya
Kiuchumi), Bw. Paul Sangawe (Kulia). Baadhi
ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakimsikiliza Waziri wa
nchi (Ofisi ya Rais) na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Hayupo pichani)
alipotembelea na kujitambulisha Tume ya Mipango. Mwenyekiti
wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) Tawi la Mipango, Bw. Stephen Katemba
(aliyesimama) akizungumza wakati Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais)
Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu alipofanya ziara ya
kujitambulisha kwa Tume ya Mipango. Katibu
Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kushoto) akimkabidhi
zawadi za vitendea kazi Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na
Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Tume
ya Mipango. Naibu
Katibu Mtendaji (Miundombinu na Huduma), Mhandisi Happiness Mgalula
(Kushoto) akimkabidhi zawadi Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na
Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa
Tume ya Mipango.
…………………………………………………………………
Na Saidi Mkabakuli
Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt.
Mary Nagu amefanya ziara ya kujitambulisha kwa Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango ambayo ni moja taasisi anazoziratibu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Dkt. Nagu alitoa wito kwa Tume
ya Mipango ijielekeze katika kujibu changamoto kuu za kiuchumi
zinazowakabili watanzania kwa sasa ikiwemo umaskini miongoni kwa
Watanzania walioko vijijini, ukosefu wa wa viwanda vya kuongeza thamani
mazao hasa kipindi hiki Tanzania inapoelekea kwenye uchumi wa gesi.
Dkt. Nagu aliasa Tume ya Mipango kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi na kijamii zitakazotoa majibu ya changamoto hizo.
“Kwa kuwa moja ya majukumu ya Tume ya Mipango ni kuandaa mipango
ya maendeleo ya muda mrefu, kati na ile ya kila mwaka na pia kufanya
tafiti mbalimbali za kiuchumi na kijamii, napenda kusisitiza kuwa
mipango inayoandaliwa ijielekeze katika kujibu changamoto hizo kubwa
zinazowakabili wananchi wetu ili kuhakikisha kuwa tunafikia malengo ya
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025,” alisema Dkt. Nagu.
Kwa mujibu wa malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025,
serikali imejipanga kuhakikisha maisha bora na mazuri kwa kila
mtanzania, utawala bora unaozingatia sheria, na kujenga uchumi imara, wa
kisasa na ushindani.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Dkt. Nagu, Katibu Mtendaji wa
Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kuwa majukumu ya msingi ya
Tume ya Mipango ni kutoa dira na mwongozo wa uchumi wa Taifa pamoja na
kubuni sera za uchumi na mikakati ya mipango ya maendeleo ya Taifa;
usimamizi wa uchumi na kufanya utafiti katika nyanja za uchumi na
maendeleo ya jamii.
Dkt. Mpango aliongeza kuwa kwa sasa Tume ya Mipango inafanya
kazi ya kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15
pamoja na uandaaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2015/16 na
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.
“Vilevile, Tume ya Mipango tumejidhatiti katika kuandaa Mpango
wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambao utajikita
katika kuifikisha tanzania kuwa ni nchi ya viwanda,” alisema Dkt.
Mpango.
Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, tangu kuundwa upya kwa Tume ya
Mipango mwaka 2008, imefanikiwa kukamilisha kazi kubwa za kitaifa
ikiwemo kufanya mapitio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, kuandaa
Mpango Elekezi wa Miaka 15 (2011/12 – 2025/26 pamoja na kuandaa Mpango
wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) na kuratibu
utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu 2006.
Kazi nyingine ni pamoja na kuandaa Mipango ya Maendeleo ya Taifa
kila Mwaka, kuandaa mfumo wa ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya
Matokeo Makubwa Sasa na kuratibu uanzishwaji wa President Delivery Bureau
(PDB), Kuandaa Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma
(Public Investiment Management – Operational Manual – PIM-OM), na
kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269