Breaking News

Your Ad Spot

Dec 25, 2015

WANAKIJIJI WA KIJIJI CHA ENGUSEROSAMBU WAFURAHIA MSITU KUREJESHWA MIKONONI MWAO


Mraghbishi Noorkiyengop Mbaima toka kijiji cha Enguserosambu akisimama mbele ya mifugo iliyokutwa msituni  katika eneo lililoruhusiwa la msitu wa  jamii wa Enguserosambu

Ilikuwa ni siku ya shangwe na furaha kwa wananchi wa kata ya Enguserosambu wilayani Ngorongoro. Hii ni baada ya serikali kukubali ombi lao la kusimamia rasilimali  ya msitu wa Loliondo namba 2 unaopakana na vijiji vinne vinavyokadiriwa kuwa na idadi ya wakazi wapatao 20,000 wanaotegemea mahitaji yao toka katika huo msitu.

Huu ni msitu pekee ambao wananchi kwa kushirikiana na Mkuu wao wa wilaya, na mashirika rafiki, wamefanikiwa kuishawishi serikali kuukabidhi msitu huo kwao.  Katika mchakato huo uliochukua miaka kadhaa wanawake toka katika vijiji vya Enguserosambu, Ng’arua, Orkiu na Naan  wamekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha azma hiyo ya kubakiza msitu wao wa enzi mikononi mwao. Akielezea furaha yake aliposikia msitu wa Loliondo namba 2 umekabidhiwa kwa wananchi, mraghbishi mwanamke Noorkiyengop Mbaima alisema

“Mimi mwenyewe nimefurahia, kwa sababu sisi akina mama tunategemea sana msitu huu kwa mahitaji yetu. Huu msitu kama ungeondoka katika mikono ya jamii basi tungeathirika sana sisi kina mama.” Umuhimu wa msitu huu kwa kina  mama ndio uliowapelekea wao kutunga na kuimba nyimbo za hamasa na kutumbuiza, kushiriki kwa wingi katika vikao mbalimbali vya maamuzi wakati wote wa mchakato huo. Kwa kuwa msitu huu ndio tegemeo lao katika kuendesha maisha ya kila siku. Hakuna chochote ambacho kiliamriwa bila ya wao kuchangia na kushirikishwa kuanzia utungaji wa sheria ndogongogo za usimamizi wa msitu hadi kukabidhiwa rasmi msitu huo. “Nikichukulia mfano katika mikutano yote ya vijiji. Kiukweli wanawake wamekuwa wanajitokeza kwa wingi, kuliko makundi mengine yoyote. Hata ile siku ya uzinduzi wa msitu walikuwa wengi zaidi,” anaelezea Jackson Nangiria

Ushiriki huu wa wanawake unatokana na ukweli kwamba wana uhusiano wa karibu na msitu huo wa enzi wa Enguserosambu.Si kwa ajili yao tu pamoja na watoto wao pia. Ni watoto hawa wa kike wenye majukumu ya kujenga nyumba kwa kutumia miti inayotoka ndani ya msitu huu, ndio wanaotembea na punda wakiwabebesha maguduria ya maji kwa umbali mrefu wakitafuta maji ambayo chanzo chake kipo kwenye  msitu huu. Wanapopata watoto wanahitaji dawa za kuwaogeshea na dawa za uzazi ambazo zinatoka kwenye msitu huu. Wao ndio wapishi katika familia zao hivyo wanahitaji kuni zinatokana na miti iliyoanguka na kukauka ambayo inapatikana kwenye msitu huu.  “Kina mama wanafanya mitambiko ndani ya msitu huu wengine ambao hawakupata watoto wanapatia hapo baada ya kuomba ndani ya msitu huu. Si hivyo tu ndani ya msitu huu kuna dawa mbalimbali za asili kwa mfano mtoto akizaliwadawa ya kumwogesha na kumnawisha hupatikana humo humo na nyingine ni za kunywa kama maziwa na nyingine kwa ajili ya mama,” anaeleza mwanamama mraghbishi Noorkiyengop Mbaima.   Uwepo wa wanawake hawa wa Kimasai katika kata ya Enguserosambu kiukweli unatokana na uwepo wa msitu huu.  Huu ndio msitu wa enzi ambao serikali ilipendekeza uwe chini ya usimamizi wake kama ulivyokuwa msitnamba moja wa Loliondo. 

Pendekezo hilo lilitolewa kupitia timu mbalimbali toka wizarani, ofisi za kanda na halmshauri ya wilaya, ambazo zilitembelea kijijini hapo kuomba kupatiwa muhtasari wa kikao cha kijiji kitakachopitisha ombi hilo la serikali.
Ombi hilo linakuja kwa kijiji kwa sababu msitu huo umekuwa chini ya usimamizi wa wananchi wa kata ya Enguserosambu kwa miaka mingi. Ni wananchi hao ndio ambao wameutunza msitu huo pasipo Kuombwa wala Kukabidhiwa  na serikali. Na kwa kweli wameweza kuutunza kwa muda wote huo. Miti haijakatwa, wananchi wamejiwekea sheria ndogondogo na pia kuwakamata wale ambao wamekuwa wakiharibu msitu huo. Hivyo wananchi hawa wamewajibika katika kuhakikisha msitu unabaki katika hali yake ya asili pasipo kushurutishwa na mtu yeyote.
Kwa mantiki hiyo muhtsari uliokuwa unaombwa na serikali ya halmashauri yan wilaya ulihiitaji baraka za wananchi, ambao hawakuwa tayari kutoa sehemu ya uhai wao unaotegemea msitu huo. Hakuna mwanakijiji aliyekuwa tayari kukubali ombi hilo. Na jibu lilikuwa ni wazi kabisa kwamba ombi hilo lilitishia mustakabali wa jamii zinazozunguka msitu huo ambazo ni vijiji vya Enguserosambu, Ng’arua, Orkiu na Naan.  Hivyo wakati serikali ikipendekeza kuusimamia

msitu huo wananchi kwa upande mwingine wakaanza kuiomba serikali iwaruhusu kuusimamia. Ni kama kichekesho pande zote zinaombana kuusimamia msitu huo. Serikalikupitia halmashauri ya wilaya inasema tunahitaji kuusimamia, na wananchi wanaiomba serikali hiyo hiyo kuusimamia msitu huo. “Kwa kweli sisi kama wananchi wa Enguserosambu tumeona kwamba huu msitu ukiondoka chini ya usimamizi wetu tutaathirika. Kwa sababu msitu huu ni uhai wa wananchi wa hapa. Tukikosa huu msitu, hatupati maji wala mvua, tutakosa chakula. Kwa kifupi tutakosa kitu muhimu cha uhai wa jamii,” anaelezea mraghbishi Noorkiyengop
Mbaima.

 Ndani ya msitu huu kuna miti ambayo wazee wanaitumia kwa ajili ya shughuli za kimila pamoja na miti ya kiasili ambayo inatumika kwa shughuli mbalimbali. Baadhi ya miti hiyo ni pamoja na Oroilieni ambao unatumika kwenye shughuli za jadi, ujenzi na kiimani. Akifafanua kuhusu mti huo Robert Kamakia anaelezea, “Huwezi kuingia jando bila kuwa na mti Oroilieni. Kwa kuwa unatumika katika kufanya baadhi ya shughuli za kimila. Mti mwingine ni Orikienyi ambao unatumika kama dawa ya kutibia magonjwa ya aina mbalimbali kama homa, kifua, malaria na kadhalika. Mti mwingine ni Ostiani ambao hutumika kwa ajili ya kivuli na kutunza maji.”  Hivyo msitu huu una maana kubwa sana kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya wazee, wanawake na vijana.  K wa upande wa vijana kwa mfano, mila na desturi

za kimasai zinawataka kujitenga hasa  pale wanapoingia ngazi ya Morani. Ambapo hutakiwa kuweka kambi kwa ajili ya kuchinja ng’ombe na kula nyama. Tukio hili huchukua mpaka mwezi mmoja wakati vijana hao, wanapoazimisha sherehe hizo. Tukio hili linashirikisha matumizi ya miti mbalimbali kwa mujibu wa taratibu zao. Supu wanazokunywa huchanganywa na baadhi ya majani ya miti hiyo. Ni dhahiri ulaji wa nyama kwa mwezi mzima unahitaji pia matumizi ya dawa za asili. Na ndio maana wamasai hawasumbuliwi sana na magonjwa yanayotokana na ulaji mwingi wa nyamba. Si hivyo tu porini hamna vitanda hivyo baadhi ya majani hutumika kwa ajili ya zoezi hilo.   “Kiukweli bila msitu vijana hawawezi kufanya chochote. Kwa kuwa kila kitu kinatoka katika huo msitu,” anafafanua Julius Long’oli. Lakini si hivyo tu, wakati wanaingizwa jando pia kuna miti inayotumika. Vivyo hivyo na katika sherehe za kumaliza jando. Hivyo msitu ni sehemu ya mila na utamaduni wa jamii hizi zinaouzunguka. Ni imani yao pia, ambayo kimsingi ni lazima iheshimiwe. Huu ni msitu wao wa enzi na enzi.  “Huu ni msitu wa jamii kwa Kimasai unaitwa Elieteti yaani ndani ya jamii kwa maana ya jina hilo ni msitu unaosaidia jamii ya sasa na ya kizazi kijacho. Kwamba huu msitu unategemewa na kizazi cha sasa na kijacho,” anafafanua Yohana Tuluni mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya kusimamia msitu.  Mtizamo huu wa wananchi wa kata hii, kwamba wao ndio wausimamie msitu huu, unatokana hali halisi ya msitu namba moja wa Loliondo unaosimamiwa na serikali kupitia halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kuwa katika hali ya kutoridhisha. Miti mingi  imekatwa kwa ajili ya matumizi ya ujenzi na hivyo kutishia uhai wa msitu huo. Kitu ambacho wana Enguserosambu hawakupenda kitokee kwa msitu namba mbili wa Loliondo ambao wanautegemea kwa mustakabali wa maisha yao.  Msitu huu umekuwa ukitegemewa na jamii ya hapa kwa miaka mingi. Ni wao ndio ambao wamekuwa wakiutunza na kwa kweli wamefanikiwa kwa njia moja ama nyingine kuufanya uwe mzuri zaidi kuliko hata ule wa Liliondo moja unasimamiwa na serikali.

“Wazo la kutaka kumiliki msitu lilikuwa kama ndoto, ukiangalia na hali halisi ilivyokuwa. Ni maono ya mtu mmoja aliyewashirikisha wenzake. Mwishowe wazo likatolewa Kwa wanakijiji ambao waliungamkono wazo hilo. Na mwishowe tukamwandikia Mkuu wa Wilaya na kwa kweli alituunga mkono sana,” anafafanua mraghbishi na mjumbe wa Bodi ya Wadhamini Jackso Nangiria   Mchakato wa kuomba hadi kukabidhiwa usimamizi wa msitu umewezesha wananchi wa Enguserosambu kuongeza ufahamu wa mambo mbalimbali juu ya usimamizi wa misitu lakini pia mahusiano baina ya wananchi na viongozi yameboreka zaidi.  Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, hivi ndivyo unavyoweza kusema Wanaenguserosambu wamekuwa wamoja zaidi. Mashirika rafiki yamesaidia sana katika kutoa elimu kwa wananchi na viongozi wao ambao maarifa hayo yamewezesha kujiwekea mikakati na hatimaye kufanikisha jamii kumiliki msitu wake wa enzi kwenye mikono yake. Wakati mchakato unaanza palikuwa na kijiji kimoja tu cha Enguserosambu kilichokuwa kinaundwa na vitongoji vinne vya Enguserosambu, Ng’arua, Orkiu na Naan ambavyo sasa vimepata hadhi ya kuwa vijiji. Kwa sasa sauti yao ni kubwa zaidi kuliko pale Mwanzo
Watendaji wa PALISEP wakiwa pamoja na wanajamii wakishikana mikono kuonesha ushirikiano baina yao. Kuanzia kushoto ni Sarah Saningo, Robert Kamakia, Jackson Nangiria, Norkiyengop Mbaima, Sunde Tutayo na Fredy Samberu 
Hivyo Bodi ya Wadhamini ilichaguliwa na mkutano mkuu wa kijiji, ambacho sasa kina hadhi ya kata. Kwa hiyo usimamizi wa msitu huu kwa sasa umekabidhiwa kwa Kata ya Enguserosambu.   Hivyo wananchi kutoka katika kila kijiji walichagua wawakilishi wao waliounda Bodi ya Wadhamini. Wawakilishi hawa jukumu lao kubwa ni kuratibu mchakato wote wa uombaji usimamizi wa msitu wa Loliondo 2. Baada ya kuchaguliwa wajumbe walipatiwa mafunzo na shirika la PALISEP ambao pia walisaidia uandikishwaji wa bodi tarehe 12/09/2012. Bodi hiyo imeundwa na wajumbe 10 kati ya hao wanawake ni 4.   Bodi hii ilipata mafunzo ya sheria mbalimbali za misitu, usimamizi wa misitu na bodi yenyewe pia kupitia video ya hali ya msitu wa Loliondo 1. Walipata pia ziara za mafunzo kwa kutembelea misitu inayosimamiwa na jamii kwa mfano msitu wa Suledo uliopo Manyara wilaya ya Kiteto. Bila jamii kujitoa kwa hali na mali isingewezekana kufanikiwa kwenye hili. Kwani bodi ya wadhamini imefanya kazi kubwa. Jamii imeshiriki katika kuandika katiba ya bodi na sheria ndogondogo ambazo zimepitishwa katika mikutano ya vijiji.

“Baada ya kuchaguliwa jukumu letu ilikuwa ni kutembelea msitu ili kujua hali yake. Lakini pia tuliweza kutoa elimu kwa wale waliokuwa wanaishi na kufanya shughuli za kilimo ndani ya msitu. Ili waweze kuondoka. Si kazi rahisi,” mjumbe wa Kamati ya Bodi ya Wadhamini Sunde Tutayo.
Kwa sasa mpango ni kuboresha na kutunza vyanzo vya maji. Kupitia bodi hiyo, wananchi wamejiwekea malengo ya kuuongeza zaidi kwa kupanda miti zaidi. Hili linafanywa kwa uangalifu mkubwa kwa kuwa kuna baadhi ya miti si rafiki mzuri kwa vyanzo vya maji inayakausha.  Lakini si hivyo tu Bodi ya Wadhamini inaangalia njia sahii ya kuhakikisha kwamba zinapatika fedha za kununulia miti mipya. Wazo lililopo ni kuwakilisha mtizamo huu kwa wanajamii ili waweze kutaarifiwa na kusikilizwa nini yatakuwa maamuzi yao kwenye uchangishaji huo wa fedha.   Changamoto nyingine ni uboreshwaji wa sheria ndogondogo kwa kuwa hakuna mipaka ya majukumu baina ya Bodi ya Wadhamini na Halmashauri ya serikali za vijiji. Kuna umuhimu wa suala hili kuwekewa utaratibu mzuri wa kiuwajibikaji kwa sababu muda mwingine vyombo hivi vinaweza kugongana kimawazo na kiutendaji na nani anawajibika kwa nani.
“Hapo nje kuna mikaratusi tumeikamata sisi kama Bodi ya Wadhamini. Mtu ameangusha mti mbichi ambao haujakauka. Na ameiyangusha bila idhini. Tumefanya hivi kwa kushirikiana na Mheshimiwa Diwani. Tunachosubili tukae na serikali ya kijiji ili tujue tunafanya nini,” anafafanua mraghbishi na Kaimu Katibu wa Bodi ya Wadhamini Jackson Nangiria.   Kwenye kukabidhiwa msitu mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya na Diwani wa Kata ya Enguserosambu walikuwepo wakati wa kukabidhiwa kwa msitu huo pamoja na wenyeviti wa vijiji vyote vinavyounda kata ya Enguserosambu.  Kwa hakika wenzetu wa Enguserosambu wameweza kujipanga na kuhakikisha kwamba msitu wao wa enzi unabaki mikononi mwao. 
 

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages