Mmoja wa mabinti wa shule ya wasichana ya
Chibok waliotekwa nyara na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram
kaskazini mashariki mwa Nigeria yapata miaka miwili iliyopita ameokolewa
kutoka kwenye makucha ya magaidi hao.
Kwa mujibu wa jeshi la Nigeria na viongozi wa baadhi ya
mashirika ya kijamii nchini humo, binti huyo kwa jina Amina Ali Darsha
Nkeki ambaye ni mmoja wa wanafunzi wa kike 276 waliotekwa nyara mwaka
2014 na matakfiri wa Boko Haram katika kijiji cha Chibok, alipatikana
akiwa salama salmin pamoja na bintiye mdogo wa miezi minne usiku wa
kuamkia jana, viungani mwa msitu wa Sambisa, kaskazini mashariki mwa
jimbo la Borno. Hata hivyo mazingira ya kupatikana au kukombolewa
msichana huyo, mwanawe mdogo wa kike na mshukiwa mmoja wa kundi la Boko
Haram ni ya kutatanisha.
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF hivi karibuni ulisema
kuwa, wasichana wanaoshikiliwa na kundi la Boko Haram wanabakwa na
kudhalilishwa kijinsia na wanamgambo wa kundi hilo. Kwa mujibu wa
wasichana hao, makamanda wa genge hilo walikuwa pia wakiwapatia mafunzo
ya kujiripua kwa mabomu. Hii ni katika hali ambayo, ripoti zilizotolewa
mwezi Mei mwaka jana zilieleza kuwa, robo tatu ya mashambulio
yaliyofanywa na kundi la Boko Haram kuanzia mwaka 2014, yalifanywa na
watoto wadogo waliopatiwa mafunzo na magaidi hao.
Ni miaka miwili sasa imepita tangu magaidi hao walipowateka nyara
wasichana wa shule moja ya serikali katika mji wa Chibok, kaskazini
mashariki mwa Nigeria, huku jamii ya kimataifa ikitaka kuachiliwa huru
mara moja wasichana hao.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269