Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya
Amnesty International na Human Rights Watch yamemjia juu Malkia
Elizabeth II wa Uingereza kwa kumualika Mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa
Al-Khalifa katika sherehe za kuadhimisha miaka 90 ya kuzaliwa kwake,
licha ya kufahamu dhulma na ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Manama
dhidi ya wananchi.
Nicholas McGeehan, Mtafiti wa Shirika la Human Rights Watch
katika eneo la Ghuba ya Uajemi amekosoa namna Mfalme wa Bahrain
alivyokuwa ameketi pambizoni mwa Malkia wa Uingereza katika sherehe za
kuadhimisha siku ya kuzaliwa Malkia huyo, katika uwanja wa Windsor mjini
Berkshire, kulikofanyika mashindano ya farasi yanayopendwa na Malkia
huyo. Amesema ni jambo la fedheha namna Uingereza inavyodhihirisha wazi
wazi juu ya uhusiano na ushirikiano wake wa karibu na utawala dhalimu wa
Bahrain, licha ya kufanya ukandamizaji na umwagaji damu.
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International na mashirika
mengine ya kutetea haki za binaadamu, yamekuwa yakikosoa kimya cha Umoja
wa Mataifa mbele ya ukandamizaji mkubwa unaofanywa na utawala wa
Manama. Shirika la Human Rights Watch lilitoa ripoti hivi karibuni na
kusema kuwa, mfumo wa mahakama nchini Bahrain ni wa kidhulma,
kiukandamizaji na usiokuwa huru.
Chama kikuu cha upinzani nchini humo cha al-Wefaq karibuni hivi
kilitoa ripoti iliyosema kuwa, vyombo vya usalama vya Bahrain vimekamata
watu 1,765 wakiwemo watoto wadogo 120 tokea mwaka jana 2015 hadi sasa,
kwa lengo la kukandamiza maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga
dhulma za utawala wa Manama.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269