Bunge la Afrika Mashariki EALA limeanza vikao vyake mjini Arusha nchini Tanzania hii leo, huku mjadala kuhusu bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ikiwa moja ya ajenda kuu katika vikao hivyo.
Hotuba juu ya bajeti ya EAC inatazamiwa kuwasilishwa katika bunge hilo la kieneo na Dakta Augustine Mahiga, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo siku ya Alkhamisi. Baada ya hapo wabunge wa EALA chini ya muongozo wa Spika Daniel Kidega wanatazamiwa kujadili na kupasisha bajeti hiyo, ikiwa ni moja ya majukumu ya taasisi hiyo ya kikanda. Bunge la Afrika Mashariki mwaka jana lilijadili na kupasisha bajeti ya dola milioni 110.6 za Marekani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Mgao mkubwa wa fedha hizo zilienda katika utekelezaji wa Protokali ya Soko la Pamoja hususan kuanzishwa mfumo wa paspoti za kieletroniki kwa lengo la kurahisisha usafiri kwa wananchi wa eneo hilo, kuimarisha mifumo ya malipo ya ada mbali mbali na kuboresha biashara na uwekezaji miongoni mwa nchi wanachama.
Mbali na swala la bajeti, Bunge la Afrika Mashariki litaandaa kikao maalumu Mei 31, ambapo wabunge wa bunge hilo la kieneo watapata fursa ya kukutana na kutangamana na Mama Ngina Kenyatta, mke wa rais wa zamani wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta, Mama Miria Obote, mke wa rais wa zamani wa Uganda Milton Obote na Mama Maria Nyerere, mke wa aliyekuwa rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269