Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema umoja
huo unawataka viongozi wa nchi duniani kutekeleza ahadi zao za kuongeza
michango yao kwa watu wanaohitaji misaada.
Ban Ki-moon ametoa wito huo sambamba na kukaribia kufanyika
mkutano wa kimataifa wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa huko
nchini Uturuki. Amesema nchi za dunia zinapaswa kuwasaidia watu
wanaohitajia misaada na kwamba Umoja wa Mataifa unahitaji kupata ahadi
ya hakikisho la viongozi wa nchi hizo ya kutekeleza suala hilo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameashiria mapigano ya utumiaji
silaha na mabalaa ya kimaumbile yanayotokea duniani na kueleza kwamba
watu wasiopungua milioni 130 wanahitaji misaada ya kibinadamu ili
kukidhi mahitaji yao ya kila siku. Ban aidha ameongeza kuwa milioni 60
kati yao ni watu waliopoteza nyumba na makazi yao.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa idadi ya watu
wanaohitaji misaada inaongezeka, na umoja huo hauna uwezo wa kudhamini
mahitaji yao.
Maelezo hayo ya Ban Ki-moon yanatolewa katika hali ambayo vita na
umwagaji damu katika maeneo mengi ya dunia yakiwemo ya Asia na Afrika
yamewafanya watu wengi walazimike kuhama na kuwa wakimbizi katika nchi
na maeneo mengine na kuishi katika hali na mazingira mabaya kabisa ya
kibinadamu kwenye kambi na maeneo ya mipakani.
Vita katika maeneo mengi ya Afrika ikiwemo Sudan Kusini na Jamhuri ya
Afrika ya Kati na mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi kama Zimbabwe
na Ethiopia yamesababisha ukame mkubwa na kuteketeza mazao ya kilimo.
Kwa mujibu wa duru za habari barani Afrika zaidi ya watu 50
wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa kwa sababu mazao ya kilimo
yamepungua tena.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo hivi sasa kuna watu wanaokadiriwa kufika
milioni 31 barani humo ambao wanahitaji chakula, na ifikapo mwaka ujao
wa 2017, watu wengine milioni 20 wataishiwa na akiba yao ya chakula na
kutokuwa na chochote cha kukila.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa watu milioni 10 nchini
Ethiopia, milioni sita nchini Sudan Kusini na wengine milioni tano
katika nchi ya Yemen watakabiliwa na baa la njaa katika mwaka ujao
kutokana na kufurika maji na ukame.
Aidha mabadiliko makubwa ya hali ya hewa yaliyotokea mashariki na
kusini mwa Afrika yamesababisha watoto wadogo milioni moja kukumbwa na
hali mbaya ya utapiamlo na kuwaacha pia watu wapatao milioni 32 wakiwa
hawana chakula cha kutosha.
Kitambo si kirefu nyuma, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa
Chakula (WFP) lilitangaza kuwa linatiwa wasiwasi na hali isiyoridhisha
ya maelfu ya wakimbizi Wanigeria ambao wamelazimika kuzihama nyumba na
makazi yao kwa kuhofia mashambulio ya kundi la Boko Haram.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo la kimataifa imeeleza kuwa
kushtadi mashambulio ya kundi la Boko Haram katika maeneo mengi ya
Nigeria kumesababisha mamilioni ya raia wa nchi hiyo kubaki bila makazi.
Hali iko vivo hivyo pia katika eneo la Ziwa Chad.
Na hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa takwimu za Shirika la
Mpango wa Chakula Duniani hakuna chakula cha kutosha na cha kuridhisha
katika kambi za wakimbizi na kwamba uhaba mkubwa wa chakula unasababisha
wakimbizi hao kugombania na kupigania chakula kwa ajili ya kuokoa
maisha yao.
Kwa mujibu wa ripoti ya ofisi ya uratibu wa masuala ya huduma za
kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu elfu 69 kutoka Sudan
Kusini nao pia wamezihama nyumba na makazi yao kutokana na mapigano na
kukosa uhakika wa kupata chakula na kujitafutia makazi katika maeneo
kadhaa ya nchi jirani ya Sudan ikiwemo mikoa ya Darfur Mashariki, Darfur
Kusini na Kordofan Magharibi. Wakimbizi hao wanahitaji misaada ya
haraka ya chakula na dawa.
Hayo yote yanajiri huku viongozi wa nchi za Afrika wakitoa wito wa
kutengwa bajeti ya dola bilioni moja na milioni 500 ili kutatua tatizo
la uhaba wa chakula linalowakabili wananchi wao. Hata hivyo mashirika na
nchi watoaji misaada hiyo ya chakula zimeahidi kuchangia asilimia 25 tu
ya bajeti hiyo.../
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269