TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI
Inspekta
Jenerali wa Polisi IGP Ernest Mangu anatarajia kukabidhiwa uenyekiti wa
Shirikisho la wakuu wa Majeshi ya Polisi kusini mwa Afrika (SARPCCO)
katika mkutano unaotarajiwa kufanyika tarehe 16 Septemba, 2016 jijini
Arusha. IGP Mangu atakabidhiwa uenyekiti huo kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la
Polisi wa nchi ya Msumbiji ambapo atadumu katika nafasi hiyo kwa
kipindi cha mwaka mmoja.
Mkutano
huo utatanguliwa na mkutano wa kamati tendaji za SARPCCO amabazo
zitakutana Septemba 14 na 15 mwaka huu ili kuandaa ajenda na
mapendekezo ambayo yatawasilishwa katika mkutano wa wakuu wa Polisi
ambao unatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Katika
mkutano huo mambo mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu yatajadiliwa
ikiwemo uhalifu wa kuvuka mipaka, pamoja na kuweka mikakati na maazimio
ya kufanya Oparesheni za pamoja zinazojumuisha nchi zinazounda
shirikisho hilo.
Vilevile,
mkutano huo utajadili kwa kina utekelezaji wa maazimio mbalimbali
kupitia kamati tendaji za wakurugenzi wa upelelezi, kamati tendaji ya
sheria, kamati tendaji ya mafunzo na kamati tendaji ya mtandao wa Polisi
wanawake.
Aidha, suala la michezo baina ya Majeshi ya Polisi kwa nchi wanachama nalo litajadiliwa katika mkutano huo.
SARPCCO
iliundwa mwaka 1995 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa Majeshi ya
Polisi kwa nchi za kusini mwa Afrika katika kukabiliana na uhalifu.
Mpaka hivi sasa umoja huo unaundwa na Nchi kumi na tano ambazo ni
Tanzania, Angola, Botswana, Malawi, Lesoto, Mauritius, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo(DRC), Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia,
Zimbabwe, Swaziland, Madagascar na Seychelles.
Imetolewa na:-
Advera John Bulimba – ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Makao Makuu ya Polisi. (P.T)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269