Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akisalimiana na wananchi waliojitokeza kumsalimia aliposimama
Nangurukuru, wilaya ya Kilwa mkoani Lindi wakati akiwa njiani kuelekea
mkoa wa Mtwara ambapo atakuwa na ziara ya kikazi ya siku nne.
Sehemu ya Wakazi wa Nangurukuru mkoani Lindi wakishangilia ujio wa Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akisalimiana na wananchi waliojitokeza kumsalimia alipowasili kwenye
ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambapo atakuwa na ziara ya kikazi ya
siku nne.
..........................................................
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema
serikali itatuma kikosi maalum cha kukabiliana na uvuvi haramu
unaoendelea katika bahari ili kudhibiti na tatizo hilo ambalo limeathiri
sana mazalia ya samaki na kuchangia kupungua kwa samaki baharini.
Makamu wa
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo 7-Sept-2016 wakati
akisalimiana na wananchi wa Nangurukuru wilayani Kilwa mkoani Lindi
ambao walijitokeza kumsalimia wakati akielekea mkoani Mtwara katika
ziara yake ya kikazi ya siku NNE mkoani huo.
Makamu wa
Rais amesema katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika vizuri serikali
pia itatuma wataalamu wa mazingira ambao watafanya tathmini ya uharibifu
wa mazingira katika bahari ili kujua uharibifu uliofanyika na kuchukua
hatua ya kukabiliana na hali hiyo.
Ameeleza
kuwa serikali itachukua hatua hizo ili kuinusuru bahari kwa sababu
imekuwa ni chanzo kizuri ya mapato kwa wananchi kutokana na shughuli za
uvuvi na shughuli nyingine zikiwemo za utalii.“Bahari yetu ndio mapato
yetu, bahari yetu ndio maisha yetu tumeitumia vibaya mapato yamepungua
na maisha hayawi mazuri hivyo ni muhimu tuitunze ili iendelee kutulea
kwa manufaa mazuri.”
Kuhusu
uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Kilwa, Makamu wa Rais Samia
Suluhu Hassan amesema serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti
zinazolenga kuhakikisha wananchi wote nchini wanapata huduma bora za
afya katika ngazi zote.
Amesema
mpango huo wa uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi nchini utaenda
pamoja na utoaji wa elimu bora wa wanafunzi kote nchini chini ya mkakati
wa serikali wa kutoa elimu bure kuanzia wanafunzi darasa la kwanza hadi
kidato cha nne.
Katika
ziara yake mkoani Mtwara, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Samia Suluhu Hassan kesho 8-Sep-16 atazindua jengo la ofisi za
Tume ya Maadili ya Uongozi wa Umma Kanda ya Kusini na kukagua miradi
mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.
Makamu wa
Rais tayari amewasili mkoani Mtwara na kupokelewa na Viongozi
mbalimbali wa mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima
Dendego pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Angela Kairuki.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269