Timu ya Azania Group, ndiyo itakayowakilisha Tanzania katika mashindano
ya kikanda ya Afrika Mashariki, ya Benki ya “Standard Chartered-Road to
Anfield” yatakaofanyika uwanja wa Jakaya Kikwete Youth Park Jumamosi,
Machi 4.
Azania walipata ushindi huo kwa kuichakaza timu ya H&R Consultancy
mabao ya 6-5 kwa penati dhidi ya mchezo wa kukata na shoka uliofanyika
mwishoni mwa wiki na kufanikiwa kuipeperusha bendera ya Tanzania.
Kwa maana hiyo, Azania Group wanatarajia kumenyana uso kwa uso na
washindi wa michuano hiyo kutoka nchi za Kenya na Uganda.
Washindi wa michuano hiyo nchini Uganda ni timu ya Cocacola wakati
kidedea wa kombe hilo nchini Kenya ni Radio ya Capital FM.
Mtendaji
Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Tanzania Sanjay Rughani (kushoto)
na Mkuu wa Mahusiano na Masoko wa Benki hiyo, Juanita Mramba wakikabidhi
kikombe kwa Bw Sikaba Hamisi ambaye ni Nahodha wa timu Azania Group,
Mshindi wa kitaifa wa mashindano ya Kombe la Standard Chartered 2017
(Road to Anfield), mashindano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye
viwanja vya JK Youth Park, Gerezani jijini Dar es Salaam.
Akiongea na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutwaa ushindi huo,
Nahodha wa Azania Group, Bw. Shabaka Hamisi alisema maandalizi yao
mazuri ndiyo siri ya ushindi wao na kuongeza kwamba wapo tayari kuwanyoa
hao wageni asubuhi kabisa.
“Katika jambo lolote kama unataka kufanya vyema, maandalizi mazuri
yanasaidia sana. Kwa upande wetu, tulifanya mazoezi yakutosha na ndiyo
maana leo tumeibuka washindi.” Alisema.
Aliongeza, “Siyo kwamba wenzetu walikua wabovu, ila umakini na utulivu
kwa upande wa wachezaji wangu ndiyo kilichotusababishia kupata matokeo
mazuri.”
Alisema mazoezi ya kujipanga kwa ajili ya mechi tayari yameshaanza kwa
ari na nguvu mpya, akiongeza kuwa ushindi kwao ni lazima.
Kwa upande wake, Phillip David, nahodha wa H&R Consultancy alisema
kukosekana kwa ukosefu wa umakini katika ushambuliaji ndiyo
uliosababisha timu yake kupoteza mechi hiyo, hata hivyo alishukuru kwa
kuibuka mshindi wa pili wa mashindano hayo.
Mtendaji
Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Tanzania Sanjay Rughani (kushoto)
na Mkuu wa Mahusiano na Masoko wa Benki hiyo, Juanita Mramba (kulia)
wakifurahi katika picha ya pamoja na timu ya Azania Group wakikabidhi
kikombe kwa timu Azania Group,Mshindi wa kitaifa wa mashindano ya Kombe
la Standard Chartered 2017(Road to Anfield), mashindano yaliyofanyika
mwishoni mwa wiki kwenye viwanja vya JK Youth Park,Gerezani jijini Dar
es Salaam.
“Kama ulivyoona, mechi ilikuwa moja moja hadi tukaingia kwenye matuta.
Wenzetu walipata penati sita wakati sisi tulifunga tano. Nafasi ya
kushinda ilikuwa upande wetu lakini Mungu hakupenda iwe ivyo,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered Tanzania Limited, Sanjay
Rughani aliwaasa wachezaji wa Azania Group kuwa wajiandae kikamilifu ili
waubakishe ubingwa nchini Tanzania.
“Sisi hakuna zawadi nzuri ambayo tunaitaka kutoka kwenu zaidi ushindi.
Fanyeni mazoezi ya kutosha ili Jumamosi inayokuja muweze kushinda mechi
zenu zote dhidi ya hizo timu kutoka Kenya na Uganda. Na sisi kama
wadhamini tutakua pamoja nanyi ili kuhakikisha kwamba mnapata ushindi
hapa nyumbani,” alisema Sanjay.
Naye Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa Benki hiyo, Juanita Mramba,
aliwapongeza kwa ushindi huo lakini akiwatahadharisha kuwa safari yao
ndiyo kwanza imeanza.
“Leo mmeshinda mashindano haya, Jumamosi kazi yenu ni kubwa zaidi kwani
mtacheza na wageni wawili, hivyo jipangeni vizuri zaidi mkiutumia vyema
uwanja wa nyumbani,” alisema.
Ukiachia mbali Azania ambao waliondoka na kombe za dhahabu, washindi wa
pili H&R Consultancy walijitwalia kombe la shaba, huku washindi wa
tatu PWC wakitwaa kombe la Bronze.
Mtendaji
Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Tanzania Sanjay Rughani (kushoto)
akikabidhi kombe kwa Nahodha wa timu ya HR Consultants, Phillip David
ambao ni washindi wa pili wa mashindano ya Kombe la Standard Chartered
2017 (Road to Anfield), yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye viwanja
vya JK Youth Park, Gerezani jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia tukio
hilo ni Mkuu wa Wateja Binafsi wa Benki ya Standard Chartered, Michael
Shio (kulia).
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269