WINGA
Shiza Ramadhani Kichuya, kwa mara nyingine leo ameibuka shujaa wa
Wekundu wa Msimbazi baada ya kutokea benchi na kuisaidia Simba kushinda
2-1 dhidi ya mahasimu, Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara.
Kichuya
aliyempokea beki Novatus Lufunga dakika ya 55, kwanza alimsetia
mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo kuifungia bao la kusawazisha Simba
dakika ya 66 kabla ya yeye mwenyewe kufunga la ushindi dakika ya 81.
Ikumbukwe
Kichuya ndiye aliyeifungia Simba bao la kusawazisha dakika ya 86 Oktoba
1, mwaka jana timu hizo zikitoka sare ya 1-1 baada ya Amissi Tambwe
kutangulia kuifungia Yanga dakika ya 26 kwa makosa ya Lufunga tena.
Na leo
Yanga SC walitangulia kwa bao la mapema tu dakika ya tano la Simon Msuva
kwa mkwaju wa penalti, baada ya kiungo Mzambia, Obrey Chirwa kuangushwa
kwenye boksi na Lufunga.
Shiza Kichuya akiwa amebebwa juu baada ya kuifungi Simba bao la ushindi
Obrey Chirwa akimtoka beki Novaty Lufunga leo kabla ya kuangushwa na kusababisha penalti
Laudit Mavugo akimiliki mpira mbele ya beki wa Yanga, Kevin Yondan
Haruna Niyonzima akigombea mpira na Janvier Bokungu
Amissi Tambwe akiwa chini baada ya kugongana na Lufunga
Refa
asiyejiuliza mara mbili katika maamuzi yake, Methew Akrama wa Mwanza
alimtoa nje kwa kadi nyekundu beki Mkongo wa Simba, Janvier Besala
Bokungu dakika ya 55 baada ya kumuonyesha kadi ya pili ya njano kufuatia
kumchezea rafu Chirwa.
Akrama
alikuwa mwiba kwa timu zote mbili leo kutokana na maamuzi yake ya
kufuata sheria 17 za soka bila kusita pale tu linapotokea kosa, hali
ambayo ilisababisha wachezaji wenyewe waamue kuwa na nidhamu uwanjani.
Yanga
ndiyo waliuanza vizuri mchezo huo wakitawala sehemu ya kiungo, iliyokuwa
ikiundwa na wageni watupu, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mzimbabwe
Thabani Kamusoko na Mzambia Justin Zulu.
Na Simba
iliyonza na washambuliaji watatu, Mavugo, Juma Luizio na Ibrahim Hajib
ikajikuta imeelemewa mno katika dakika 30 za mwanzo za mchezo.
Yanga
watajilaumu wenyewe kwa kucheza mchezo wa ‘kibishoo’ zaidi, wakigongeana
pasi zisizo na tija badala ya kusaka mabao moja kwa moja.
Kibao
kilianza kuigeukia Yanga baada ya kocha Joseph Omog kumpunguza
mshambuliaji mmoja, Luizio na kumuingiza kiungo Said Hamisi Ndemla
dakika ya 27 aliyekwenda kuipa uhai timu yake.
Na Yanga ikapata pigo baada ya kiungo wake tegemeo, Kamusoko kuumia na kumpisha Said Juma ‘Makapu’.
Kipindi
cha pili, Simba SC ilirudi na maarifa mapya na pamoja na mabadiliko
mengine yaliyofanywa na Omog, akiwatoa Lufunga na Mohammed Ibrahim na
kuwaingiza Mkude na Kichuya mambo yakawa mazuri upande wao.
Pamoja na kumpoteza Bokungu aliyetolewa kwa kadi nyekundu, lakini Simba wakatoka nyuma na kushinda 2-1.
Kikosi
cha Yanga kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Haji,
Andrew Vincent, Kevin Yondan, Justine Zulu/Juma Mahadhi dk78, Simoni
Msuva, Thabani Kamusoko/Said Juma ‘Makapu’ dk45, Amisi Tambwe/Deus
Kaseke dk70, Obrey Chirwa na Haruna Niyonzima.
Simba SC;
Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty
Lufunga/Shiza Kichuya dk51, Abdi Banda, James Kotei, Ibrahim Hajib,
Muzamil Yassin, Juma Luizio/Said Ndemla dk27, Laudit Mavugo na Mohammed
‘Mo’ Ibrahim/Jonas Mkude dk57.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269