Na Daudi Manongi-MAELEZO
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
amewataka wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Mashirika ya Umma na Mamlaka za
udhibiti kuwa wabunifu na kutumia fursa na rasilimali zilizopo nchini
ili kuleta maendeleo chanya.
Amebainisha hayo leo Ikulu Jijini Dar es
Salaam wakati akifungua mkutano wa kujadili nafasi ya Mashirika ya Umma
katika utekelezaji wa mpango wa pili wa Taifa wa maendeleo wa miaka
mitano.
“Rai yangu leo ni kwamba kwenye
majadiliano yenu pendekezeni na kufanya mashirika ya umma yawe
endelevu,yapanuke zaidi na kuliongezea Taifa mapato na ndio maana
nafarijika sana kuona mkutano huu unajumuisha wadau wote muhimu ili
pamoja na kuweka mikakati ya namna mashirika ya umma ya Tanzania
yanavyoweza kushiriki kwenye utekelezaji wa mpango wa Maendeleo,”Alisema
Majaliwa.
Akielezea hali ya mashirika ya umma
nchini,Waziri Mkuu amesema kuwa utegemezi wa mashirika unaendelea
kupungua na mchango na gawio kutoka kwenye mashirika hayo unaendelea
kuongezeka na kuhimiza kuongezeka kwa ubunifu na matumizi mazuri ya
rasilimali chache zilizopo na kuongeza kati ya mashirika 65 ya
kibiashara,mashirika 8 yanaendeshwa kwa Ruzuku ya Serikali,wakati
mashirika 57 hayategemei ruzuku ya Serikali.
Ameagiza kuboreshwa kwa mwongozo wa
kupata wajumbe wa Bodi na kuwaagiza kuweka mwongozo rasmi wa namna ya
kupata wajumbe hawa kwani ni sehemu inayolalalmikiwa sana na wananchi.
Amesema kuwa wameyashirikisha mashirika
ya umma kwenye utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa sababu vipaumbele
vya mpango wa pili wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano ambayo ni
ujenzi wa viwanda vya kuimarisha kasi ya ukuaji wa uchumi,miradi mikubwa
ya kielelezo na miradi wezeshi kwa maendeleo ya viwanda ikiwemo
barabara,reli,nishati,bandari maji na mawasiliano.
Aidha ameagiza kuondolewa kwa urasimu
katika shughuli za mashirika ya umma kwani unakwamisha uboreshaji na
maendeleo ya mashirika ya umma.
Waziri Mkuu pia ametoa rai kwa viongozi
wote wa mashirika ya umma kutosaini mikataba isiyo na tija kwa Taifa
ambayo inapelekea kupata hasara kubwa na kuhimiza mashirika haya
kushirikiana na mashirika ya nje pamoja na sekta binafsi ili kupata
nguvu ya pamoja katika kukuza uchumi.
“Ni lazima mashirika ya umma yakafanya
kazi kwa pamoja na kwa kushirikiana ikiwemo kubadilishana mbinu na
utaalamu ili kulifikisha Taifa hili katika azma yake ya kukuza Uchumi wa
viwanda kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu”,Alisisitiza
Mh.Majaliwa.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269