NA HAMZA TEMBA - WMU
"Haiwezekani
maliasili yetu ikawa inapotea hovyo hovyo kwasababu ya watu wachache
wenye tamaa ya kupata utajiri wa harakaharaka, hakuna wa kumbakiza, awe
mkubwa, awe nani, shikeni, wala msijali mtu cheo chake, umri wake, dini
yake, kabila lake, umaarufu wake, sheria ni msumeno, watafuteni wote
mpaka wakiona tembo wawe wanakimbia wenyewe".
Hiyo ilikua ni kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipofanya ziara ya kushtukiza katika makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii (Mpingo House) Jijini
Dar es Salaam tarehe 29 Oktoba, 2016 kwa lengo la kufuatilia
utekelezaji wa operesheni ya kukabiliana na ujangili inayofanywa na
kikosi kazi kilichoundwa na Wizara hiyo.
Katika
ziara hiyo, Rais Magufuli akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja
Jenerali Gaudence Milanzi alishuhudia meno ya tembo 50 yaliyokuwa
yamekamatwa katika kipindi cha siku mbili zilizopita Jijini Dar es
Salaam, alioneshwa pia gari lililokuwa limebeba meno hayo na watuhumiwa
wanane wanaotuhumiwa kujihusisha na mtandao wa biashara haramu ya meno
ya tembo.
Rais
Magufuli aliwapongeza askari wote waliopo katika kikosi cha kupambana
na ujangili pamoja na raia wema wanaotoa ushirikiano katika mapambano
hayo na kwamba anatambua kazi nzuri wanayofanya na anawaunga mkono.
Katika
hotuba yake ya kwanza ya kulihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mjini Dodoma, Rais Magufuli alitoa vipaombele kadhaa vya
kutekelezwa na wizara zake huku Wizara ya Maliasili na Utalii akiipa
majukumu makuu matatu; kupambana na ujangili, kutatua migogoro ya mipaka
kwenye maeneo ya hifadhi na kuongeza mapato ya Serikali.
Wizara
hiyo inayoongozwa na Waziri Prof. Jumanne Maghembe; Naibu Waziri,
Mhandisi Ramo Makani; Katibu Mkuu, Meja Generali Gaudence Milanzi na
Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Aloyce Nzuki imejipanga kutekeleza majukumu yake
makuu ya uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Kuendeleza Utalii pamoja na
vipaombele ilivyoelekezwa.
Mara
tu alipoteuliwa kuingoza wizara hiyo, Prof. Maghembe alitangaza vita na
majangili na kubainisha kuwa kipaumbele chake kikubwa kitakuwa ni
kupambana nao. “Niwaambie majangili sasa wakafanye kazi nyingine ama
wakae nyumbani, kiama kinakuja huko”, alisema.
Alisema
kuwa atasimamia kwa uhakika maliasili za Watanzania kwa sababu mambo ya
maliasili ndiyo eneo alilobobea kwenye usomi wake.
“Tutajitahidi
pia kutangaza utalii na kuongeza mapato ya sekta hii kama tulivyofanya
kwenye miaka ya 2006 hadi 2008, tuliongeza bei za vitalu na ada kwa
mnyama mmoja mmoja anayewindwa,” alisema Profesa Maghembe siku
aliyoapishwa.
Mikakati ya Wizara kukabiliana na ujangili
Ni
takribani mwaka mmoja na miezi miwili tangu uongozi wa Serikali ya
awamu ya tano uingie madarakani, taarifa iliyotolewa na Idara ya
Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii, inaonyesha kuwa katika
kipindi cha mwezi Novemba, 2015 hadi mwezi Oktoba 2016 Wizara hiyo
imefanikiwa kuweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ujangili
ikiwemo kuanzisha kikosi kazi maalum cha kupambana na ujangili.
Kikosi
kazi hicho cha kudhibiti uhalifu wa Misitu na Wanyamapori
nchini(Wildlife and Forest Crime Unit),kinasimamiwa na Watendaji wa
Sekta ya Wanyamapori kwa ajili ya kukabiliana na majangili katika ngazi
za juu za uwezeshaji (Facilitators) kwa kushirikiana na vyombo vingine
vya ulinzi na usalama nchini.
Kikosi
hicho kiliundwa mwezi Julai, 2016 na Katika kipindi cha miezi mitatu
(Agosti hadi Oktoba, 2016) kimefanikiwa kukamata majangili 107 na kesi 9
ziko mahakamani, upelelezi wa kesi nyingine unaendelea. Nyara mbali
mbali, silaha na vifaa vya kufanyia ujangili pia vimekamatwa na kikosi
kazi hicho.
Wizara
imefanikiwa kuimarisha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania
(TAWA) ambayo ilizinduliwa rasmi mwezi Novemba, 2015 na Rais wa awamu ya
nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na kuanza majukumu yake rasmi tarehe 1
Julai, 2016.
Mamlaka
hii yenye jukumu la kuendeleza shughuli za ulinzi na uhifadhi wa
wanyamapori nchini kwa maeneo yote yaliyopo nje ya Hifadhi za Taifa na
Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kudhibiti ujangili kwenye maeneo hayo.
Mabadiliko
ya mfumo wa utendaji kutoka ule wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu
umenzishwa na Wizara kwa ajili ya kuimarisha nidhamu, ufanisi wa
utendaji kazi za uhifadhi pamoja na mapambano dhidi ya ujangili. Katika
kipindi hicho mafunzo kadhaa yametolewa kwa watumishi 425 wa TANAPA
katika kuelekea mabadiliko hayo.
Watumishi
wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania pia pia wamepatiwa mafunzo hayo. Lengo ni kutoa
mafunzo hayo kwa watumishi wote wa taasisi za uhifadhi nchini zikiwemo
za wanyamapori na misitu.
Pamoja
na mafunzo hayo, matumizi ya teknolojia ya ndege zisizokuwa na rubani
(drones) kwa ajili ya doria na ulinzi wa mipaka na wanyamapori yamepewa
kipaombele katika hifadhi mbalimbali za taifa na Pori la Akiba la Selous
kama mkakati wa kukabiliana na ujangili.
Mkakati
mwingine ulioanzishwa na kuimarishwa ni ukaguzi wa nyara katika viwanja
vya ndege na bandari kwa kutumia mbwa maalum wa kunusa ili kutambua
nyara na kufuatilia majangili.
Taarifa
hiyo imeeleza kuwa ushirikiano na nchi jirani katika kutatua changamoto
za uhifadhi na biashara haramu ya ujangili umeimarishwa. Katika eneo
hili Tanzania inashirikiana na nchi ya Msumbiji, Zambia, Uganda na Kenya
kukabili ujangili unaovuka mipaka ya nchi hizo.
Ushirikishwaji
wa wananchi katika uhifadhi na vita dhidi ya ujangili ni moja ya
mkakati uliowekwa na wizara. Elimu ya uhifadhi kwa wananchi imeendelea
kutolewa katika wilaya 11 na vijiji 57 vinavozunguka Pori la Akiba la
Selous, Mapori ya Akiba ya Lukwika/Lumesule na Msanjesi na eneo la
Ardhioevu la Ziwa Natron.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa;
Katika
kipindi cha mwezi Novemba, 2015 hadi Oktoba 2016, taarifa ya Idara ya
Wanyamapori inaeleza kuwa Sekta ya Wanyamapori imefanikiwa kukamata
jumla ya watuhumiwa 5,894 kwa makosa mbalimbali ya uvunjaji wa Sheria za
Uhifadhi na kuwafungulia mashitaka. Jumla ya kesi 859 zilifunguliwa.
Kesi 136 zenye watuhumiwa 248 zilihukumiwa kifungo cha jumla ya miezi
8,295 na kesi 198 zenye watuhumiwa 234 walilipa faini jumla ya shilingi
387,985,063/=.
Imeeleza
kuwa silaha 254 za aina mbalimbali zilikamatwa katika kipindi hicho,
Nyara za aina mbalimbali zilikamatwa ikiwemo meno ya tembo vipande 848
vyenye uzito wa kilo 2,664.48, nyamapori yenye uzito wa kilo 7,790 za
wanyama mbalimbali, meno 8 ya kiboko, magunia 67 ya magamba ya
kakakuona, ngozi 16 na mikia 33 ya wanyamapori mbalimbali.
Miongoni
mwa watuhumiwa waliokamatwa katika kipindi hicho ni watu sita akiwemo
mfanyabiashara Yusuf Ally (34) aliyewahi kutajwa na Rais John Magufuli
kwa jina maarufu la ‘Mpemba’ kuwa ni kinara wa ujangili, watuhumiwa hao
ambao kesi yao bado inaendelea walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na
mashtaka ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya
shilingi milioni 785.6.
Mtuhumiwa
mwingine maarufu wa ujangili aliyewahi kukamatwa nchini ni mwanamke wa
China anayedaiwa kuongoza genge kubwa zaidi la usafirishaji wa pembe za
ndovu barani Afrika. Akipewa jina la utani “Ivory Queen”, Yang Feng Glan
anadaiwa kusafirisha pembe za ndovu 706 kutoka nchini kwenda Mashariki
ya mbali. Glan, 66, anadaiwa kuwa na ukaribu na majangili wa Afrika
Mashariki na walanguzi wa China, kesi yake bado ipo mahakamani.
Ujangili waripotiwa kuanza kupungua;
Januari
17 mwaka huu (2017), akizungumza kwenye kikao cha kamati ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Utalii mkoani morogoro, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Meja Generali, Gaudence Milanzi alisema ujangili
hapa nchini kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba nyara
zinazokamatwa kwa sasa ikiwemo meno ya tembo ni za zamani zilizokuwa
zikisubiria kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Aliongeza
kuwa mizoga ya wanyamapori imepungua ikilinganishwa na kipindi cha
nyuma ambapo ni dalili pia ya kupungua kwa ujangili nchini, “mafanikio
hayo yametokana na kazi kubwa inayofanywa na vikosi maalum vya Askari wa
wanyamapori vya kudhibiti ujangili kwa kushirikiana na vyombo vingine
vya ulinzi na usalama nchini”, alisema Milanzi.
Katika
hatua nyingine alieleza kuwa kitendo cha Serikali ya China kupiga
marufuku biashara ya meno ya tembo nchini humo ni jambo la kupongezwa na
kwamba uamuzi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msukumo wa
vitendo vya ujangili nchini kwa kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa masoko
makubwa ya meno hayo duniani.
Ujangili
haukubaliki kwa kuwa unatishia kuathiri faida kubwa inayopatikana
kupitia sekta ya utalii ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea uwepo wa
wanyamapori katika hifadhi zetu, Sekta hii inachangia asilimia 17.5 ya
pato la taifa na ni sekta inayoongoza kwa miaka mitatu mfululizo kwa
kutoa mchango wa asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni nchini.
Ni
jukumu la kila Mtanzania kuona umuhimu wa rasilimali hizi na kuunga
mkono juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa Maliasili zetu zinaendelea
kuwepo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo, Tanzania bila Ujangili
inawezekana, kila mmoja akitimiza wajibu wake.
Rais
Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi alipofanya ziara ya
kushtukiza makao makuu ya hiyo (MPINGO HOUSE) jijini Dar es salaam
Oktoba 29, 2016. (Picha na Ikulu)
Rais
Dkt John Pombe Magufuli akikagua pembe za ndovu 50 zilizokamatwa katika
operesheni maalum ya kusaka majangili alipofanya ziara ya kushtukiza
makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii (MPINGO HOUSE) jijini Dar
es salaam Oktoba 29, 2016.(PICHA NA IKULU)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269