Dada
Neema Mwita Wambura (32) akizungunza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kupitia njia ya Simu akimshukuru kwa
msaada aliompatia wa kufanyiwa tena uchunguzi wa afya yake katika
hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Pia Rais Dkt. Magufuli ameahidi
kumpatia hifadhi mama huyo pamoja na watoto wake watatu ambao kwa sasa
wapo Bunda mkoani Mara. Pia Rais Dkt. Magufuli alimpatia msaada Dada
huyo kiasi cha Shilingi laki tano. Dada
Neema Mwita Wambura aliungua Vibaya mara baada ya kumwagiwa uji wa moto
uliokuwa unachemka jikoni na mume wake katika kijiji cha Kyagata,
Tarime mkoani Mara.
Mama
Mjane Mariam Amir ( Bibi Mwaija ) ambaye amempa hifadhi Neema Mwita
Wambura nyumbani kwake Tandika Davis Corner akiomba dua kumuombea Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kupitia njia
ya Simu kumshukuru mara baada ya kuzungumza naye kuhusiana na kumsaidia
Dada Neema Mwita Wambura (32). Rais Dkt. Magufuli amempongeza Mama huyo
Mjane ambaye ameonesha moyo wa kizalendo na kumpa hifadhi Dada huyo
aliyemwagiwa uji wa moto na mumewe katika kijiji cha Kyagata, Tarime
mkoani Mara. Pia Rais Dkt. Magufuli alimpa Mjane huyo kiasi cha Shilingi
laki tano.
Dada
Neema Mwita Wambura (32) wakwanza kulia akiwa pamoja na Mama Mjane
Mariam Amir ( Bibi Mwaija ) wakiwa ndani ya gari mara baada Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kumsaidaia ili
aweze kufanyiwa tena uchunguzi wa afya yake katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Wauguzi
wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakimpokea Dada Neema Mwita Wambura
(32) na kuanza mara moja kumfanyia tena uchunguzi wa afya yake katika
majeraha aliyoyapata mara baada ya kumwagiwa uji wa moto uliokuwa
ukichemka jikoni kitendo kilichofanywa na mume wake.
Mkurugenzi
Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Profesa Lawrence Museru
akimjulia hali Dada Neema Mwita Wambura (32) mara baada ya kufikishwa
tena hospitalini hapo. Dada Neema Mwita alifanyiwa upasuaji mara nne
katika siku za nyuma hospitalini hapo Muhimbili ili kutibu majeraha yake
hayo ya moto.
Daktari
Bingwa wa magonjwa ya dharura na Ajali katika hospitali ya Taifa ya
Muhimbili Dkt. Juma Mfinanga akizungumza kuhusu hali ya mgonjwa Dada
Neema Mwita Wambura (32) aliyefikishwa tena katika Hospitalini hapo kwa
ajili ya uchunguzi wa Afya yake.
Dada
Neema Mwita Wambura (32) akiwa katika hali ya majonzi kufatia majeraha
makubwa mwilini mwake kufatia kumwagiwa uji wa moto na mume wake mkoani
Mara.
Daktari Bingwa wa upasuaji wa ngozi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt.
Ibrahim Mkoma akizungumzia historia ya mgonjwa huyo ambaye yeye pamoja
na jopo la madaktari bingwa walimfanyia upasuaji ili kutibu majeraha
yake ya ngozi katika kipindi cha nyuma. (PICHA NA IKULU).
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amewapongeza Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa juhudi kubwa
walizofanya kunusuru maisha ya Neema Mwita Wambura ambaye alijeruhiwa
kwa kuunguzwa na maji ya moto kifuani, shingoni na mkononi.
Pongezi
hizo za Mhe. Dkt. Magufuli zimetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais, Ikulu Bw. Gerson Msigwa muda mfupi baada ya kumfikisha Neema Mwita
Waitara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako Rais Magufuli
ameagiza apelekwe kwa mara nyingine kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa
maendeleo ya afya yake.
Katika
Pongezi hizo Mhe. Dkt. Magufuli amesema Madaktari wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili wamefanya kazi kubwa na ya kizalendo kuhakikisha Neema
anapona licha ya majeraha makubwa aliyoyapata miaka miwili iliyopita na
ambayo yalitishia uhai wake.
Pia
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mama Mariam Amir (Bibi Mwanja) kwa upendo
wake wa kumchukua Neema na kisha kumpa hifadhi nyumbani kwake huko
Tandika Devis Kona Jijini Dar es Salaam.
“Nakushukuru
sana Mama na ninakupongeza, umeonesha mfano mzuri wa kujali umoja na
upendo kwa Watanzania wenzako bila kujali dini, kabila wale kanda
unayotoka na hivi ndivyo Watanzania wote tunapaswa kufanya” amesema Mhe.
Rais Magufuli.
Kabla
ya kutoa pongezi hizo, mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amewatuma
wasaidizi wake wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu
Bw. Gerson Msigwa kwenda Tandika Devis Kona katika Wilaya ya Temeke
Jijini Dar es Salaam kumuona Neema Mwita Wambura ambaye alipatiwa
hifadhi katika nyumba ya Mama Mjane aitwaye Mariam Amir (Bibi Mwanja)
baada ya kuona picha na kusoma taarifa za mkasa uliomkuta katika
mitandao ya kijamii.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa Shilingi laki 5 kwa Neema kwa ajili ya kumsaidia
chakula yeye na watoto wake waliohifadhiwa na rafiki yake huko Bunda
Mkoani Mara na pia ametoa Shilingi laki 5 kwa Mariam Amir aliyejitolea
kumsaidia na kumpa hifadhi nyumbani kwake. Pia ameahidi kumsaidia wakati
wote wa matibabu na pia familia yake.
Baada
ya kumpokea daktari bingwa wa magonjwa ya dharula na ajali katika
kitengo cha dharula cha Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Juma Mfinanga
amesema wameanza kumfanyia uchunguzi ili kujua maendeleo yake na kama
kumpa matibabu zaidi.
Nae
Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Ibrahim Mkoma ambaye amekuwa akimfanyia
matibabu Neema Mwita Wambura tangu Julai 2015 alipofikishwa hospitalini
hapo kwa mara ya kwanza amesema Neema anaendelea vizuri baada ya
kufanyiwa upasuaji mara nne.
Dkt.
Mkoma amesema baada ya upasuaji huo, sasa Neema anaweza kuinua na
kugeuza shingo yake na kwamba kwa sasa wataendelea kumfanyia uchunguzi
zaidi ili kujua maendeleo yake. Mhe. Rais Magufuli ameagiza vyombo vyote
vinavyohusika kufanyia kazi mkasa uliomkuta Neema Mwita Wambura na
kuhakikisha haki inatendeka.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269