Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka
kulia), akifunua kitambaa kilichofunika Jiwe la Msingi, kuashiria uzinduzi
rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya
Tatu (REA III), kwa Mkoa wa Shinyanga. Wanaoshuhudia kutoka
kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA),
Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa
Shinyanga ambaye pia ni Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na
Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, akiwahutubia
wananchi wa Kijiji cha Negezi, Wilaya ya Kishapu (hawako pichani),
wakati wa uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu (REA III), kwa Mkoa wa Shinyanga. Uzinduzi huo
ulifanyika hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, akiwatunza
na kujumuika kucheza ngoma pamoja na moja ya vikundi vya burudani
kutoka Shinyanga, kilichokuwa kikitumbuiza wakati wa hafla ya uzinduzi
wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA
III), kwa Mkoa wa Shinyanga hivi karibuni.
Na Veronica Simba – Shinyanga
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, amemtaka
Mkandarasi kutoka Kampuni ya M/s OK Electronics and Electric Limited,
atakayetekeleza kazi ya kusambaza umeme vijijini Awamu ya Tatu (REA
III) kwa Mkoa wa Shinyanga, kuhakikisha anaajiri wananchi wenye sifa
kutoka maeneo hayo badala ya kuleta wafanyakazi kutoka mbali.
Alitoa maagizo hayo hivi karibuni katika Kijiji cha Negezi, wilayani
Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi
Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kwa
Mkoa huo.
“Tumia wataalam/vibarua vijana kutoka maeneo haya. Hatutapenda
uajiri watu kutoka mbali wakati wafanyakazi wenye sifa wako
hapahapa,” alisema Naibu Waziri.
Aidha, Dkt. Kalemani, alimwagiza Mkandarasi huyo kuhakikisha
anawalipa vibarua mara moja kila wanapokamilisha kazi husika.
“Hakuna kulaza malipo kwa sababu sisi tunakulipa vizuri.”
Sambamba na maagizo hayo, Dkt Kalemani, aliutaka uongozi wa Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo, kujipanga na
kumsimamia Mkandarasi husika ili kuhakikisha anafanya kazi masaa 24
kwa siku.
Alisisitiza kuwa, Ofisa yeyote atakayelegalega kumsimamia Mkandarasi
husika kadri inavyotakiwa. Atawajibishwa kwa kuondolewa katika nafasi
yake.
Naibu Waziri pia, aliwaelekeza TANESCO kuhakikisha wanawafuata
wateja na kuwapatia huduma mahala walipo badala ya kusubiri wateja
wawafuate katika Ofisi zao, ambazo ni chache na ziko mbali na makazi
ya wananchi wengi hususan walioko vijijini.
Kufuatia maelekezo hayo; aliuomba uongozi wa Halmashauri mbalimbali
za Mkoa wa Shinyanga, kuanzisha vituo maalum ambavyo vitatumiwa
na Maofisa wa TANESCO kuwahudumia wateja walioko katika maeneo
yao.
“Hatuwezi kusubiri kujenga Ofisi, shughuli ambayo itachukua muda
mrefu, wakati wananchi wanahitaji umeme,” alisisitiza.
Kuhusu suala la wakandarasi binafsi, ambao hufanya kazi ya kutandaza
nyaya za umeme katika nyumba za wananchi mbalimbali na kuwatoza
kiasi kikubwa cha fedha; Naibu Waziri alitaka tabia hiyo ikome mara
moja.
Alitoa maelekezo kuwa ni marufuku kwa Mkandarasi binafsi, kufunga
nyaya kwenye nyumba ya mteja yeyote bila kwanza kupata idhini kutoka
TANESCO.
Naibu Waziri, aliagiza majina ya wakandarasi binafsi ambao
wataidhinishwa na TANESCO kufanya kazi ya kufunga nyaya za umeme
kwa wateja, yabandikwe katika Ofisi husika ili wananchi waweze
kuwatambua na pia iwe rahisi kuratibu gharama za kazi hiyo, hivyo
kuwaepusha wananchi na utapeli kwa kulipishwa gharama kubwa
isivyostahili.
Aidha, aliwashauri viongozi wa Halmashauri na Serikali za Vijiji, kutenga
hela katika bajeti zao, kwa ajili ya kuunganisha umeme kwenye Taasisi
mbalimbali muhimu zikiwemo Shule na Vituo vya Afya. Alikumbusha
kwamba, kazi ya kuweka umeme kwenye nyumba na taasisi mbalimbali
ni ya wahusika wenyewe, siyo Serikali.
Vilevile, Dkt Kalemani aliwataka wananchi kuwa na ufahamu wa
gharama za kuunganishiwa umeme kupitia Mradi wa REA, ambazo
alizitaja kuwa ni shilingi 27,000 tu. “Ole wake atakayepandisha gharama
hizo kwa maslahi binafsi, atakiona cha moto.”
Aliwahimiza wananchi ambao hawana uwezo wa kulipia gharama za
kufungiwa nyaya za umeme, kuomba kufungiwa kifaa cha Umeme
Tayari (UMETA) ambacho hakihitaji kutandaza nyaya katika nyumba
yote na ambacho kinaweza kufungwa katika nyumba isiyozidi vyumba
vinne.
Uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya
Tatu (REA III) kwa Mkoa wa Shinyanga; kama ilivyokuwa katika Mikoa
mingine ambayo Mradi huo umekwishazinduliwa; ulienda sambamba na
kumtambulisha kwa viongozi na wananchi, Mkandarasi atakayetekeleza
kazi hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269