Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akifungua mkutano wa wadau wa nishati ulioambatana na uzinduzi wa Jukwaa la Nishati Tanzania (TEP) kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu jijini Dar es Salaam tarehe 05 Aprili, 2017. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadili upatikanaji wa nishati endelevu ya kutosha kwa bei nafuu kwa ajili ya uchumi wa viwanda Tanzania.
Sehemu ya wadau wa nishati wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) katika mkutano huo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ( wa tatu kutoka kulia) na Balozi wa Uholanzi Nchini, Jaap Frederiks ( wa pili kutoka kushoto) wakifurahia uzinduzi wa Jukwaa la Nishati Tanzania (TEP). Kushoto kabisa ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya Nishati Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Florens Luoga (katikati) wakifurahia jambo katika mkutano huo . Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya Nishati Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na kulia ni Balozi wa Uholanzi Nchini, Jaap Frederiks
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa mwakilishi kutoka Chuo cha Twente kilichopo nchini Uholanzi, Profesa Tom Veldkamp (kulia) mara baada ya kumalizika kwa uzinduzi huo. Katikati ni Balozi wa Uholanzi Nchini, Jaap Frederiks
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati waliokaa mbele) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya Nishati Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo ( wa pili kutoka kushoto waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa mkutano huo.
Waziri wa Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo amesema nishati ya uhakika ya umeme itatokomeza umasikini nchini Tanzania ifikapo mwaka 2030.
Profesa Muhongo aliyasema hayo alipokuwa akizindua Jukwaa la Nishati Tanzania (TEP) pamoja na mkutano wa siku mbili kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu mapema leo jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo unaolenga kujadili upatikanaji wa nishati endelevu ya kutosha kwa bei nafuu kwa ajili ya uchumi wa viwanda Tanzania, unakutanisha wadau mbalimbali zikiwemo kampuni za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini kama vile Statoil, BG na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Wadau wengine ni pamoja na kampuni za kuzalisha umeme kama vile Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Songas pamoja na mabalozi wa nchi mbalimbali, taasisi za kifedha na viongozi wa kiserikali.
Profesa Muhongo alisema kuwa Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana itakayopelekea Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyofafanua.
Profesa Muhongo alisema kuwa nishati ya kutosha itapelekea uanzishwaji wa viwanda vidogo hususan katika maeneo ya vijijini na kuzalisha ajira hivyo kupunguza wimbi la vijana kuhamia mijini kutafuta maisha.
Akielezea mikakati ya upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini, Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imeandaa mpango wa matumizi ya vyanzo vya nishati ya umeme ambapo gesi ni asilimia 40, maji asilimia 25, makaa ya mawe asilimia 30 na nishati mbadala asilimia 5
Aliongeza kuwa serikali inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi katika sekta za nishati ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.
Akielezea maendeleo ya mipango ya Serikali, Profesa Muhongo alisema hadi sasa Serikali imeshakamilisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa ugunduzi wa gesi ya kutosha katika mikoa ya Mtwara na Lindi umepelekea uanzishwaji wa viwanda vya saruji na mbolea katika mikoa hiyo.
Alisema pia serikali ipo katika hatua ya mwisho ya majadiliano kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga, Tanzania na kusisitiza kuwa Serikali imeanza majadiliano kwa ajili ya mradi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka jijini Dar es Salaam hadi Ndola, Zambia.
Aliendelea kusema kuwa Serikali imekuwa ikikutana na wawekezaji kutoka kampuni za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini kila baada ya miezi mitatu ili kufahamu maendeleo na changamoto ya shughuli zake.
Aliendelea kutaja mipango mingine kuwa, ni pamoja na uanzishwaji wa kozi mbalimbali katika masuala ya gesi na mafuta katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Waziri Muhongo alisema kuwa Serikali imekuwa ikitoa ufadhili kwa wataalam wake kwa ajili ya kusomea masuala ya gesi na mafuta katika ngazi ya shahada za uzamili na uzamivu katika vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi.
Aidha, aliongeza kuwa serikali kupitia balozi mbalimbali imekuwa ikitoa ufadhili kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi kusomea masuala ya gesi katika vyuo vya ndani na nje ya nchi.
“Lengo letu kama Serikali, ni kuhakikisha kuwa tunazalisha wataalam wa kutosha watakaofanya kazi katika kampuni za mafuta na gesi na hivyo kuinua uchumi wa nchi,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Florens Luoga alisema kupitia Jukwaa la Nishati Tanzania linaloundwa na wataalam kutoka Tanzania na Uholanzi wanaangalia namna ya kushirikiana kupitia kubadilishana uzoefu kupitia program mbalimbali.
Mkutano huo unaoambatana na maonesho ya kampuni mbalimbali za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi pamoja na kampuni za uzalishaji wa umeme umeandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia na Sayansi ya Karume Nchini Zanzibar (KIST).
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269