Na Frank Mvungi, MAELEZO- Dodoma
Mamlaka ya Maji Safi na Maji
Taka Dar es Salaam (DAWASA) imeanza kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli la kuupatia maji
mji wa Kisarawe uliopo Mkoani Pwani kutoka katika mtambo wa Ruvu Juu.
Kwa mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya Habari iliyotolewa
naDAWASA inaonyesha kuwa kazi zilizofanyika hadi sasa kabla ya zabuni
kutangazwa ni pamoja na upembuzi yakinifu, usanifu wa kina wa mradi,
kuandaa makabrasha ya zabuni na
kutangaza zabuni .
“Kwa sasa Kazi ya uchambuzi wa zabuni zilizowasilishwa na
kufunguliwa mwishoni mwa wiki inaendelea ambapo Kampuni 12 za ndani na nje ya
nchi zimejitokeza kuomba kutekeleza mradi huo” inasisitiza sehemu ya Taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa mradi huo mkubwa kwa awamu yakwanza utahusisha ujenzi
wa kituo cha kusukuma maji kitakachokuwa na uwezo wa kusukuma maji kiasi cjha
lita 60 kwa sekunde na kujengwa kwa
kituo chenye uwezo wa kuhifadhi lita 480,000 za maji.
Mradi huo utahusisha ununuzi na ulazaji wa mabomba makuu kwa
umbali wa kilometa17 hadi Makao Makuu ya Wilaya ya Kisarawe.
Awamu ya Pili itahusisha ujenzi wa tenki la Vigungu ambalo
litahudumia eneo lililotengwa kwa ajili ya makazi mapya na nyongeza ya maji kwa
ajili ya Viwanda vitakavyojengwa.
Aidha DAWASA imechukua
hatua za muda mfupi kupunguza tatizo la maji katika mji huo ikiwemo Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia
DAWASA kutekeleza mradi wa maji wa Vigama kwa kuchimba Kisima kipya,Kufunga
Pampu, Kujenga mnara, kufunga tenki la kuhifadhia maji na kulaza mabomba ya
kusambaza maji hayo ambapo mkandarasi wa kutekeleza mradi huo amepatikana na
mradi utaanza mwezi Februari mwaka huu.
Hatua nyingine itakuwa DAWASA kukarabati kisima cha Shule ya
Sekondari Manneromango ikiwa ni mchango wake katika mkakati wa kuboresha miundo
mbinu ya shule ili kuongeza ufaulu katika Wilaya hiyo,mradi huo utaanza
kutekelezwa machi mwaka huu
DAWASA imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya Maji katika
Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuondoa
changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wake .
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269