Breaking News

Your Ad Spot

Jan 25, 2018

RAIS DK. MAGUFULI AKUTANA NA MJUMBE MAALUM WA RAIS KAGAME, AAGANA NA BALOZI WAZIMMBABWE, LEO

IKULU, DAR ES SALAAM
Rais Dk. John Magufuli (Pichani), leo Januari 25, 2018 amekutana na Mjumbe Maalum wa Rais wa Rwanda na aliyewahi kuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dk. Donald Kaberuka na kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Tanzania na umoja wa Afrika (AU).

Baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa Dk Kaberuka amesema uchumi wa Tanzania unakua vizuri na amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jinsi anavyosimamia ukuaji wa uchumi huo.

“Nimefurahi sana jinsi Tanzania inavyokwenda mbele, maendeleo yanakwenda kwa kasi na Mhe. Rais anafahamu kabisa kwamba katika Afrika nchi zetu zinahitaji kuwa na uchumi bora, ningependa kumpongeza Mhe. Rais na Watanzania wote kwa kazi nzuri wanayofanya” amesema Dk. Kaberuka.

Dk. Kaberuka amesema katika mazungumzo hayo pia amewasilisha ujumbe wa Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye kuanzia mwezi huu atakua Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), na ndiye aliyekabidhiwa majukumu ya kufanya mabadiliko ndani ya umoja huo.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Zimbabwe hapa nchini anayemaliza muda wake Mhe. Edzai Chimonyo na kumpongeza kwa uwakilishi mzuri alioufanya kwa miaka 10 aliyoiwakilisha Zimbabwe hapa nchini.

Rais Magufuli amemuomba Mhe. Chimonyo kumfikishia salamu za pongezi Emmerson Mnangagwa kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zimbabwe na amemuhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri wa kihistoria na kidugu uliopo kati yake na Zimbabwe.

“Naomba umwambie Mheshimiwa Rais Mnangagwa kuwa namkaribisha atembelee Tanzania na namtakia heri katika majukumu yake, natarajia ataendeleza uhusiano na ushirikiano wetu ili tuweze kujiimarisha zaidi kiuchumi kwa manufaa ya nchi hizi mbili” amesema Rais Magufuli.

Chimonyo ameshukuru kwa ushirikiano mkubwa alioupata katika kipindi chake cha Ubalozi hapa nchini na amempongeza Rais Magufuli kwa namna anavyoiongoza nchi, huku akitaja baadhi ya mambo yanayofanywa kwa mafanikio makubwa kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa, ujenzi wa miundombinu hususani barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Chimonyo ambaye alikuwa kiongozi wa Mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na Kaimu Kiongozi wa Mabalozi wote wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania amesema Mabalozi hao wanafurahishwa na wanaunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Mhe. Rais Magufuli ikiwemo kuhamia makao makuu Dodoma

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages