Breaking News

Your Ad Spot

Jan 21, 2010

SAKATA LA AMBULANCE: IKULU YATOA UFAFANUZI

Jumatatu, Januari 18, 2010, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete hakuweza kumkabidhi gari la wagonjwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ngorogoro, Mkoani Arusha, Bwana Kayange Jacob kwa sababu gari hilo ni la Kijiji cha Engarenaibor, Wilaya ya Longido, katika mkoa huo huo wa Arusha.

Tunapenda kufafanua kuwa palifanyika makosa katika kupeleka taarifa kutoka Ikulu kwamba badala ya kumuita Mkurugenzi wa Wilaya ya Longido kuja kuchukua gari la wilaya yake akaitwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro. Makosa hayo yamerekebishwa, na jana, Januari 19, 2010 Katibu wa Rais, Ikulu, Bwana Prosper Mbena amekabidhiwa gari hilo Mkurugenzi wa Wilaya ya Longido, Bwana Christian Laizer.

Wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais wilayani Longido mwezi Agosti, 2009 kukagua athari za ukame ulioikumba wilaya hiyo, wananchi wa Engarenaibor walimweleza Mheshimiwa Rais kilio chao cha Kituo chao cha Afya kukosa gari la kubeba wagonjwa. Kijiji cha Engarenaibor kiko kilometa 196 kutoka hospitali ya Wilaya ya Monduli, na kiko kilometa 116 kutoka hospitali ya mkoa ya Mount Meru iliyoko Arusha. Wilaya ya Longido haina Hospitali ya Wilaya ina kituo cha afya ambacho nacho kipo kilomita 30 kutoka kijijini hapo ambapo unaangaliwa utaratibu wa kukifanya kituo hicho cha afya kuwa hospitali ya wilaya. Kutokana na umbali huo, imekuwa ni tabu kubwa kufikisha wagonjwa katika hospitali pale inapokuwa lazima kumpeleka mgonjwa kwa rufaa.

Hivyo, Mheshimiwa Rais alipopewa zawadi ya magari mawili ya kubeba wagonjwa na Ndugu Abdul Haji wa Cooper Motors Ltd, aliamua moja kati ya magari hayo lipelekwe Engaronaibor na lingine lipelekwe Kituo cha Afya cha Kamsamba, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Mbeya.

Gari la Kituo cha Afya cha Kamsamba lilikabidhiwa na Mheshimiwa Rais kwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Mbozi Bwana Levison Jeremiah Chilewa siku ile ya Jumatatu ya tarehe 18 Januari, 2010.

Tunachukua nafasi hii kuomba radhi kwa usumbufu uliompata Bwana Kayange Jacob na kwa jinsi tukio hilo lilivyomfanya aonekane kwa wananchi.

Rais Kikwete anatambua haja ya vituo vya afya katika Wilaya ya Ngongororo na wilaya nyingine nchini kupatiwa magari ya kubeba wagonjwa. Serikali inaendelea na juhudi za kununua magari hayo, na Rais anaahidi kuwa katika mgao ujao na Wilaya ya Ngorongoro watafikiriwa.

                                                                 Imetolewa na:

                                                 Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

                                                                      Ikulu,

                                                           DAR ES SALAAM.

                                                              20 Januari, 2010

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages