.

MPAMBANO WA WATANI WA JADI

Apr 18, 2010

SIMBA YAIKUNJA YANGA 4-3
* Yapokea kombe kishujaa
* Kapuya achekelea
TAMBO za mashabiki wa Yanga leo zimezimwa, baada ya timu yao kutandikwa mabao 4-3 na wapinzani wao wakubwa Simba, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
     Katika mchezo huo, Yanga ililazimika kucheza pungufu uwanjani baada ya wachezaji wake wawili tegemeo, Wisdom Ndhlovu na Amir Maftah kutolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi, Mathew Akrama wa Mwanza, baada ya kufanya makosa ya kizembe yaliyoigharimu timu hiyo.
   Ndhlovu alionyeshwa kadi nyekundu dakika 57 baada ya kumchezea rafu ya makusudi Mussa Hassan 'Mgosi', wakati Maftah alimpiga kichwa Juma Saidi 'Nyoso' mbele ya mwamuzi huyo. Akrama pia alimtoa kwa kadi nyekundu beki wa Simba, Joseph Owino kwa mchezo mbaya.
   Kipa Mserbia, Obren Curkovic, Nurdin Bakari, Ndhlovu na Maftah walicheza chini ya kiwango, hatua ambayo iliwaudhi maelfu ya mashabiki wa klabu hiyo ambao waliwazomea mara kadhaa wakati mchezo ukiendelea.
   Athuman Idd 'Chuji' na nahodha Abdi Kassim 'Babi', na Shadrack Nsajigwa waliocheza dakika 90 za mchezo huo, walikuwa kivutio kwa kuonyesha soka ya kiwango bora.
   Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi, alizima furaha ya mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao la nne dakika 92. Okwi aliyeingia kuchukua nafasi ya Mike Barasa, aliufumania mpira nje ya eneo la hatari ambapo alifumua shuti kali lililomshinda Curkovic kabla ya kujaa wavuni.
   Simba ilianza mchezo kwa kasi na dakika ya tatu ilipata bao la kwanza kupitia kwa Uhuru Selemani, aliyefunga kwa shuti baada ya Maftah kufanya makosa. Chuji aliyekuwa akihaha uwanja mzima, aliifungia Yanga bao la kusawazisha dakika ya 31 baada ya kutokea piga nikupige langoni kwa Simba.
   Kiungo huyo alifunga bao hilo baada ya Babi kuupiga mpira wa adhabu upande wa kulia kufuatia makosa ya Juma Jabu aliyemchezea rafu Nsajigwa, aliyekwenda mbele kusaidia mashambulizi.
   Mgosi alifunga bao la pili dakika 53 baada ya Ndlovu kumshindwa kumkaba kabla ya Jerry Tegete kusawazisha dakika 67 akimalizia kazi nzuri ya Babi. Dakika 73 Mgosi alifunga bao tatu kwa kichwa baada ya mabeki wa Yanga kuzembea.
   Dakika 89, Tegete aliwainua vitini mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao la tatu kwa mkwaju wa penalti kufuatia Kevin Yondani kumfanyia madhambi Babi ndani ya eneo la hatari.
   Awali, mchezo huo ulianza kwa kasi ambapo iliwachukua dakika ya kwanza Yanga kubisha hodi langoni kwa Simba, lakini Boniface Ambani alishindwa kufunga. Dakika ya 14, Chuji alikosa bao baada ya shuti lake kutoka nje kabla ya dakika mbili baadae Selemani kupiga shuti lililodakwa na Curkovic.
   Dakika 18 hadi 20, Yanga ilitawala mchezo baada ya kucheza pasi fupi fupi kabla ya kufanya mashambulizi ya kushitukiza. Dakika 21, Bakari alikosa bao akiwa ndani ya eneo la hatari ambapo kwa mashangao wa wengi alipiga shuti dhaifu akiwa ana kwa ana na kipa Juma Kaseja.
   Dakika ya 35, mpira ulisimama kwa muda baada ya wachezaji wa pande zote kumvamia mwamuzi baada ya Yondani kumfanyia madhambi Ngasa. Dakika ya 45, Nsajigwa alikosa bao baada ya shuti lake kupaa juu.
   Dakika moja kabla ya mpira kumalizika wachezaji wa timu hizo walitaka kuzichapa kavu kavu baada ya Kaseja kugongana na Ngasa. Vurugu hizo zilidumu kwa takriban dakika mbili kabla ya mwamuzi kupuliza filimbi ya mwisho sekunde chache baada ya mpira kuanza.
  Mwamuzi aliwaonyesha kadi za njano wachezaji Yondani, Okwi, Jabu wa Simba ambapo kwa upande wa Yanga walikuwa ni Tegete na Ndhlovu.
   Yanga: Obren Curkovic, Shadrack Nsajigwa, Amir Maftah, Nadir Haroub, Wisdom Ndlovu, Athuman Idd, Nurdin Bakari/Geofrey Bonny, Abdi Kassim, Boniface Ambani/Jerry Tegete, Mrisho Ngasa na Kigi Makasi/Steven Bengo.
    Simba: Juma Kaseja, Salum Kanoni, Juma Jabu/Ulimboka Mwakingwe, Kevin Yondani, Joseph Owino, Hilal Echesa, Uhuru Selemani, Mohamed Banka/Juma Nyoso, Musa Hassan, Mike Barasa/Emmanuel Okwi na Nico Nyagawa....
Wana-SimbaMashabiki wa YangaMCHEZAJI wa Simba Nico Nyagawa  akipambana na Amir Mftaha wa Yang timu hizo zilipomenyana leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Hilary Echesa (kushoto) akishangilia kwa kuvua jezi baada ya timu yake kupata bao la nne.Kocha wa Yanga na benchi lake wakiduwaa baada ya kuona tumu yake inaelemewaKocha Msaidizi wa  Simba Amri Saidi akibebwa na wachezaji na mashabiki wa timu hiyo baada ya mechi.Mashabiki wa Simba wakifurahia kombe baada ya timu yao kukabidhiwa.
MWENYEKITI wa Simba anayemaliza muda  wake, Hassan Dalali akilia kwa furaha baada ya mechi 

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª